Kwa nini ubadilishe mswaki baada ya kupona Corona?
Wataalam wa afya wasema kuna uwezekano wa virusi vya ugonjwa huo kubaki kwenye mswaki wa zamani na kuibua maambukizi mapya.
- Virusi vinaweza kubaki kwenye mswaki wa zamani na kuibua maambukizi mapya.
- Endapo mtu hana uwezo wa kupata mswaki mpya anashauriwa kusafisha kwa maji ya moto.
Dar es Salaam. Kama ulishapata maambukizi ya virusi vya Corona (Uviko-19) na kupona unahitaji ufafanuzi juu ya dhana ya kuachana na mswaki uliokuwa ukiutumia wakati unaumwa ili kuepuka maambukizi mapya ya ugonjwa huo.
Hilo linatokana na kuwepo kwa mjadala kwenye mitandao ya kijamii ambao baadhi ya watu wanasema ni sahihi na wengine wakisema siyo sahihi kuacha kutumia mswaki ambao ulikuwa ukitumia wakati umepata Uviko-19.
Moja ya taarifa hizo zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii hasa Whatsapp imebeba kichwa cha habari “COVID RECOVERED SHOULD CHANGE TOOTHBRUSH” ikimaanisha kuwa “waliopona COVID-19 wabadilishe miswaki”
Moja ya ujumbe unaowataka watu kubadilisha miswaki mara baada ya kupona Uviko-19, njia mbayo imependekezwa na baadhi ya wataalam wa afya. Picha| Matandao.
Ni sahihi kutumia mswaki mpya baada ya kupona?
Kwa mujibu wa Dr Pravesh Mehra kutoka India anasema uwezekano wa mtu kupata maambukizi kwa mara nyingine endapo atatumia mswaki aliokua akitumia akiwa na maambukizi ni mkubwa kwa sababu vijidudu vinakua vimebaki kwenye kifaa hicho cha kusafishia meno.
Hivyo inashauriwa mtu kubadili mswaki mara baada ya kupona Corona.
“Kama wewe au yeyote kwenye familia yako amepata Corona, akipona hakikisha anabadilisha mswaki au vitakasa mdomo. Miswaki inaweza kubakisha virusi na njia sahihi ya kuwaondoa ni kwa kubadili mswaki,” anasema Dr Mehra.
Sababu kuu ya kutumia mswaki ni kuepuka virusi ambavyo zinaweza kuwa vimebaki kwenye mswaki, jambo linaloweza kumuweka mtu aliyepona katika hatari ya kupata tena maambukizi.
Daktari wa kinywa na meno kutoka hospitali ya Meno Yangu ya jijini Dar es Salaam, Dk Esther Emmanuel amesema hana uhakika na dhana hiyo ila anafikiri hiyo ni njia sahihi ya kukabiliana na maambukizi mapya ya Uviko-19 kwa mtu aliyepona.
“Tunashauri mgonjwa wa Corona atumie mswaki mpya pale anapoweza. Kama hatakua na uwezo huo ni vyema kusafisha mswaki wa awali kwa maji ya moto ili kuuwa virusi vinavyobaki kwenye mswaki wa zamani,” anasema Dk Esther.
Daktari huyo amesema ushauri huo hutolewa hata kwa watu waliopona magonjwa mengine ikiwemo ya kinywa ili kuwaweka salama zaidi.