May 18, 2024

Corona ilivyopukutisha mifuko ya wafanyabiashara wa samaki Kanda ya Ziwa

Walalamika kushuka kwa soko la samaki na dagaa kulikochangiwa na janga la Corona duniani.

  • Walalamika kushuka kwa soko la samaki na dagaa.
  • Masharti ya kujikinga na Corona yachangia kuzorotesha biashara.
  • Serikali yasema wafanyabiashara watumie soko la ndani kikamilifu.

Mwanza. Charles Kazuruga, mvuvi wa samaki mkoani Mwanza haoni tena matumaini ya rasilimali maji kuendelea kumtoa kimaisha.Kazuruga anategemea Ziwa Victoria kuvua samaki na kuwauza ili kujipatia kipato kwa ajili ya familia yake.

Lakini mambo yamebadilika, samaki anapata lakini changamoto inabaki kupata soko la uhakika la bidhaa hiyo inayotumika kama kitoweo na kutengeneza bidhaa nyingine za kusindika. 

Pamoja na sababu nyingine, kuyumba kwa soko la samaki kumechangiwa na janga la Corona (Uviko-19) kuathiri uuzaji wa samaki nje ya nchi kutokana kukazwa kwa masharti kwa mataifa hayo ili kukabiliana na janga hilo.

Kazuruga, baba wa watoto watano, anasema samaki wanaovua huwauza katika viwanda vya samaki vilivyomo jijini hapa kabla hajasafirishwa kwenda katika nchi mbalimbali hasa za bara la Ulaya ambazo zimeweka vizuizi vya usafiri wa watu na bidhaa.

“Kutokana na changamoto hiyo kwa kipindi cha mwezi mmoja sasa toka wimbi la tatu liingie nchini hali ya biashara imekuwa ngumu na wiki kadhaa tumekuwa tukidai fedha zetu viwandani  na tunapouliza tunaambiwa bado hawajapata ndege ya kusafirisha minofu hiyo,” anasema Abdulman Hamisi, mvuvi katika mwalo wa Mswahili jijini hapa. 

Kucheleweshwa kwa malipo ya wavuvi kunatokana na viwanda kukaa na samaki muda mrefu bila kupata ndege za kusafirisha kwenda nje ya nchi.

Baadhi ya viwanda vya samaki havikuweza kupatikana kwa wakati kueleza athari za Uviko-19 kwenye biashara zao na kujibu tuhuma hizo za wavuvi. 

Wavuvi hao wanasema shughuli zao zilianza kuyumba tangu Corona iingie Tanzania Machi 2020 na sasa hali inazidi kuwa ngumu na hawajui hatma yao kwa kuwa samaki wamekuwa wengi lakini soko hamna.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi mwaka 2020, sekta ya uvuvi ilichangia asilimia 1.7 ya pato la Taifa huku ukuaji wake ukiongezeka mara nne hadi asilimia 6.7 kutoka asilimia 1.5 mwaka juzi.

Sekta hiyo imetoa ajira za moja kwa moja kwa wavuvi wapatao 195,435 na wakuzaji viumbe maji 30,064 katika mwaka 2020/21. 

Corona inavyotibua biashara ya samaki

Licha ya ukuaji huo, Uviko-19 umechangia kwa kiwango kikubwa kushusha bei ya samaki jijini hapa kutoka Sh12,000 kwa samaki wenye kilo kati ya 5 na 9 na hadi wastani wa Sh9,000. 

Samaki wenye kilo kati ya moja na nne nao kwa sasa wanauzwa wastani wa Sh8,000 kutoka Sh10,000 ya awali. 

Pamoja na bei hizo kushuka upatikanaji wa samaki katika kipindi cha msimu wa mwezi Mei hadi Julai 2021 ulikuwa wa kiwango cha chini, jambo lililozidi  kupukutisha mapato ya wavuvi hao.

Hamisi anasema mara nyingi upatikanaji wa samaki huwa ni kuanzia mwishoni mwa Agosti hadi Aprili.

Wakati bei ya samaki ikishuka, tozo wanazotozwa wavuvi hao zimeendelea kubaki pale pale, jambo wanalolamikia kuwa faida wanayopata ni ndogo. 

Kwa samaki ambao wavuvi wanawapeleka viwandani jijini hapa, hutozwa ushuru wa Sh200 kwa kila kilo moja. 

“Suala hili linaumiza wavuvi kwa kuwa kwa kila tani moja ya samaki hulipiwa Sh200,000 tofauti na miaka iliyopita ambapo samaki mwenye kilo moja alitozwa Sh100 na hii yote ni kwa sababu ya wafanyabiashara wanakosa ndege zinazotua hapa nchini kusafirishia samaki,” anasema Kazuruga.

Wavuvi katika mwalo wa Mswahili wakiwa wameegesha vyombo vyao kabla ya kuingia katika Ziwa Victoria kusaka samaki ambao wanadai soko lake limeyumba. Picha| Mariam John.

Maumivu hadi kwa wafanyabiashara

Mwenyekiti  wa Soko la samaki la kimataifa Mwaloni la Mwanza, Magafu Fikiri anasema toka janga la Uviko-19 lilipoingia nchini limeathiri biashara ya samaki kwa kiwango kikubwa.

“Siwezi kusema ni kwa kiasi gani janga hili limeathiri shughuli hii lakini ukweli ni kwamba toka mwaka jana lilipoingia hadi sasa shughuli hii imekuwa nzito,” amesema Magafu.

Licha ya kubadilika kwa msimu wa samaki na dagaa na kulegezwa kwa masharti ya Uviko-19 katika nchi mbalimbali duniani hasa zile wanazotegemea kuuza bidhaa hizo lakini wafanyabiashara bado hawauzi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

“Kabla  ugonjwa huo haujaingia mwaka juzi tulikuwa na uwezo wa  kuuza gunia 50 hadi 100 zikaisha ndani ya siku 1 hadi 3 lakini kwa sasa hali ni tofauti ambapo tunauza kati ya gunia 10 hadi 20 kwa muda huo na zaidi ya muda huo,” anasema Fikiri.

Kwa mujibu wa mfanyabiashara huyo, wafanyabiashara wa nje ya nchi hawaji tena Tanzania badala yake huagiza mizigo ya samaki, jambo linalopunguza mzunguko wa biashara na hivyo kutegemea soko la ndani ambalo mahitaji yake ni ya chini.

Kauli ya mwenyekiti huyo inafungamana na mfanyabiashara, Octavian Bashaya anayesafirisha dagaa wa Ziwa Victoria kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) anayedai shughuli hiyo imekuwa na mlolongo mrefu na sheria kali mipakani.

Anasema taratibu za uthibitishaji vipimo na vyeti vya Uviko-19  huwafanya wafanyabishara wengi kukaa siku tatu na zaidi mipakani, jambo linalopunguza kasi ya usafirishaji wa bidhaa zao na kuongeza gharama za biashara.

“Ugumu wa biashara umeongezeka zamani ilikuwa ni ukaguzi wa mizigo pekee mpakani kama umekamilisha taratibu za usafirishaji. Lakini sasa agenda Corona imeongeza ukaguzi zaidi na hawaruhusu watu kuingia ama kutoka hovyo hovyo kutokana na sheria za kujikinga na Uviko-19 zilizowekwa,” anasema Bashaya.

Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara wana matumaini kuwa shughuli zao zitarejea kama kawaida kwa sababu nchi zinachukua hatua mbalimbali ikiwemo kutoa chanjo kutokomeza janga hilo.

“Hatuwezi kulaumu kwa kuwa ni mipango ya Mungu tuendelee kumwamini na kumuomba atuepushie ili hali za biashara zirejee kama zamani,” ana sema Omary Hussen, mfanyabiashara wa dagaa kwenda DRC. 

Kwa mujibu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, samaki katika Ziwa Victoria wameongezeka hadi kufikia tani milioni 3.5 kwa mwaka 2020 kutoka tani milioni 2.6 mwaka 2019.

Wavuvi na wafanyabiashara wa samaki dagaa wakiendelea na shughuli kuuza na kununua bidhaa hizo mwalo wa Mswahili na soko la samaki la kimataifa Kirumba. Picha| Mariam John.

Serikali yakataa kushindwa

Serikali nayo ni miongoni mwa waathirika wa janga hilo kutokana kukosa mapato yatokanayo na kodi na ushuru wa biashara ya samaki hivyo kupunguza kasi ya uboreshaji wa miundombinu na huduma za kijamii.

Meneja wa Uvuvi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Antony Ndaba anakiri kuwa biashara ya samaki na dagaa imeyumba baada ya ugonjwa huo kuingia nchini.

Anasema kabla ya ugonjwa huo halmshauri ilikuwa na uwezo wa kuingiza asilimia 70 ya mapato yote yanayotokana na zao la samaki, lakini kwa sasa yameshuka na kufikia asilimia 50.

“Mara nyingi mzunguko umebaki kuwa ndani ya nchi na nje ya nchi mara moja moja,” anasema Ndaba.

Pamoja na kukiri kushuka kwa biashara hiyo, Ndaba anasema ipo misimu ambayo kunakuwa na ongezeko la mazao hayo kwa wingi hasa kipindi cha kiangazi ambacho mapato huongezeka. 

Kuhakikisha biashara ya samaki inaimarika licha ya tishio la Uviko-19, mtaalam huyo anasema wanaendelea kuwaunganisha wafanyabiashara wa ndani na masoko ya kimataifa ili kuendelea kusafirisha mizigo ya samaki.

Mkakati mwingine wa Serikali ni kujenga viwanda na kuimarisha soko la ndani la samaki kwa kuhimiza ulaji wa samaki na matumizi ya bidhaa zake.