May 18, 2024

Ujenzi wa nyumba unaoweza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

Ni mtindo wa ujenzi wa nyumba unaoendana na athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo upepo mkali, ongezeko la joto, mafuriko na baridi.

  • Ni mtindo wa ujenzi wa nyumba unaoendana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
  • Kujenga nyumba zinastahimili upepo mkali, joto na baridi.
  • Kuzuia ukataji miti na kupata mipya inaweza kuwa suluhisho.

Dar es Salaam. Tishio ambalo dunia inakabiliana nalo kwa sasa ni mabadiliko ya tabianchi. Mabadiliko hayo ambayo huchangiwa na shughuli za kibinadamu husababisha kupanda kwa viwango vya joto, kina cha bahari, ukame, na vimbunga.

Wakati dunia ikiendelea kutafuta suluhu ya changamoto hizo, tafiti mbalimbali zinaeleza kuwa tuko mbioni kuishi kuambatana na mabadliko ya tabianchi.

Ripoti mpya ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) inaeleza jinsi nyumba zinavyoweza kujengwa hasa kwenye nchini zinazoendelea duniani ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Katika ripoti hiyo ya masuala ya tabianchi, UNEP imeeleza kwa kina njia tano za ujenzi wa majengo yanayoweza kuhimili mabadiliko ya tabianchi:

Kujenga kwa kuzingatia viwango vya joto

Utafiti uliofanywa na muungano wa majiji makubwa duniani yanayopambana na mabadiliko ya tabianchi mwaka 2018  unaonesha kuwa ifikapo mwaka 2050 watu bilioni 1.6 wanaoishi katika miji 970, mara kwa mara watakumbwa  na viwango vya juu vya joto.

Hali hiyo inaweza kuyaweka maisha ya wakazi wa miji hiyo katika hatari kubwa.

Ili kukabiliana na hali hiyo, watu wanaweza kubuni misitu ya mijini na maeneo yenye miti kupunguzua joto kwa kuwa miti huleta kivuli na hali ya ubaridi.

Miundo ya majengo pia nayo  inaweza kuchangia kupunguza joto ndani ya majengo. Kwa mfano nyumba zinazojengwa kwa saruji nzito na kwa vifaa vingine vizito hutumiwa China, Chile na Misri kupunguza joto.

Makazi haya ya kuhamia waathirika wa mabadiliko ya tabianchi katika eneo la Nakai,jimbo la Khammoune nchini Laos. Picha| World Bank/Stanislas Fradelizi.

 Kujenga kwa kuzingatia ukame

Mabadiliko ya tabianchi yameathiri misimu ya mvua kote duniani.

Uhifadhi ya maji ya mvua na mifumo inayotumiwa kuyakusanya maji ni njia kuu za kuhifadhi maji wakati wa ukame na kupunguza hatari ya kutokea mafuriko wakati misimu ya mvua nyingi.

Maji yaliyokusanywa yanaweza kuhifadhiwa kwenye matanki na kutumiwa nyumbani wakati wa ukame.

Njia nyingine rahisi ya kukabalina na ukame na mafuriko ni kwa kupanda miti au mimea mingine nje ya majengo. Mizizi ya miti hii husadia maji kufyonzwa kwenye udongo na hivyo hupunguza hatari ya kutokea mafuriko.

Maeneo yenye ukame, ni vema miti ikapandwa ili kuimarisha uoto na kuepusha mafuriko wakati wa mvua. Picha| Micato Safaris. 

Ujenzi wa nyumba juu ya nguzo

UNEP inaeleza kuwa mwaka 2025 watu milioni 410 walio maeneo ya pwani watakuwa katika hatari ya mafuriko na kuongeza viwango vya maji ya bahari.

Huko Kerala, India nyumba zinazoweza kustahimili mafuriko zinajengwa juu ya nguzo ili kuruhusu maji ya mafuriko kupita chini yake.

Kwenye pwani ya nchi ya Malaysia, nyumba zimeinuliwa mita mbili juu kuruhusu maji kupita na miti kumea  chini yake.

Mbinu moja iliyopendekezwa Bangladesh ni kujengwa nyumba ambayo itakalia nguzo zenye matanki yanayoweza kuelea wakati wa mafuriko.

Jengo hilo linaweza kutumiwa kama kituo cha kijamii na kama makazi ya dharura wakati wa mafuriko.

Jengo hili lililopo Bangladesh, Indonesia limejengwa juu ya nguzo ili kulikinga dhidi ya mafuriko wakati wa mvua. Picha| Giant Grass.

Nyumba zinazostahimili upepo mkali

Vimbunga na mawimbi vinatarajiwa kutokea mara kwa mara kufuatia mabadiliko ya tabianchi, inaeleza UNEP.

Vinaweza kuathiri majengo kwa njia tofauti ikiwemo kwa kung’oa mapaa na hata kuharibu misingi ya majengo. Miundo ya mapaa huwa na umuhimu mkubwa. 

Uthabiti kutoka msingi wa nyumba hadi kwenye paa ni kati ya njia za kuhakikisha mapaa yanastahimili upepo.

Nyumba za kuhimili vimbunga zilizojengwa nchini Ufulipino. Picha| Rappler.com. 

Kujenga kwa kuzingatia baridi

Hii inahusu kujenga nyumba ambayo inaweza kupata joto na kuhifadhi joto la ndani. Mapaa, kuta na madirisha yajengwe kwa namna ambayo yatazuia kupotea kwa joto.

Majengo pia yanaweza kujengwa wa kwa njia ambayo yatakuwa rahisi kumulikwa na jua huku kuta zinaweza kupakwa rangi nyeusi ili kuvuta joto ndani ya nyumba.

Mapaa yanayoweza kusaidia mimea kumea juu yake hutumiwa kwenye miji mingi duniani na huonekana kuwa suluhu kwa kuleta ubaridi msimu wa joto na joto wakati wa msimu wa baridi.

Katika eneo lako unatumia mbinu gani kukabiliana na mabadiliko ya tabinchi? Anza leo, punguza shughuli hatarishi ikiwemo ukataji wa miti ambazo zinachochea uharibifu wa mazingira.