Fahamu ambayo huambiwi kuhusu chanjo ya Johnson and Johnson
Ni pamoja na ukweli wa kuwa chanjo hiyo imethibitishwa kuwa na matokeo mazuri na kirusi cha Delta ambacho ni anuai ya kirusi cha Corona.
- Chanjo hii ni kati ya chanjo tatu zinazotolewa nchini Marekani.
- Hadi sasa nchi zaidi ya 30 zinatumia Johnson & Johnson kama chanjo ya dharula.
- Ni kweli awali Marekani ilisitisha chanjo hii lakini iliruhusiwa tena nchini baada ya kujiridhisha usalama wake.
Dar es Salaam. Mengi yanazungumzwa mtandaoni kuhusu chanjo ya Johnson & Johnson ambayo ni moja ya chanjo zilizopendekezwa kutumika Tanzania.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto chanjo hiyo ya Johnson & Johnson mashuhuri kama Janssen ni miongoni mwa aina tano ya chanjo zilizopendekezwa kutumika Tanzania ikiwa pamoja na Moderna, Pfizer, Sinopharm, na Sinovac.
Julai 24, Tanzania ilipokea dozi ya chanjo ya Johnson & Johnson dozi zaidi ya milioni moja kutoka kwa Marekani kama msaada kupitia mpango wa chanjo kwa nchi za kipato cha chini ujulikanao kama Covax.
Serikali imesema imelenga kuchanja asilimia 60 ya watu na kwamba itakuwa ni hiari ya mtu kuchanja ama la.
Hata hivyo, tangu chanjo hiyo iingie kuna baadhi ya watu wameachwa kwenye lindi la habari zinazopotosha kuhusu chanjo kwa ujumla ikiwemo ya Johnson & Johnson.
Chanjo ya Johnson & Johnson inatolewa kwa zaidi ya nchi 30 duniani. Picha| Dreamstime.
Mathalani katika mitandao wa WhatsApp, baadhi wanaisema chanjo hiyo kuwa na uwezo mdogo kulinganishwa na nyingine zilizopitishwa na kuthibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), jambo ambalo si kweli.
Wasichofahamu ni kuwa chanjo ya Johnson & Johnson ni kati ya chanjo zilizofanya vizuri zaidi katika baadhi ya nchi ikiwemo Marekani na Brazil katika kukabiliana na Uviko-19.
Kwa Marekani ambayo inatoa chanjo aina tatu kwa raia wake, chanjo ya Johnson & Johnson imethibitishwa kufanya kazi zaidi kuliko chanjo nyingine.
Chanjo hiyo, inayotolewa kwa dozi moja kwa mpokeaji kuchomwa sindano ya kwenye misuli, imethibitishwa kufanya kazi kwa 72% nchini Marekani, 68% nchini Brazil na 64% nchini Afrika Kusini.
Baada ya kuwa na taarifa zisizo sahihi kuhusu chanjo hii, tazama video hii kufahamu vitu ambavyo wapotoshaji hawakuambii.