Filamu ya safari ya kuutafuta mti unaofufua waliokufa
Safari hiyo inawasogeza watafiti watatu wenye lengo la kukomboa maisha ya wanadamu karibu na vifo vyao.
- Dada na mdogo wake wanaanza safari ya kuutafuta mti wa maajabu.
- Mti huo unadaiwa kuwa na dawa ya kuponya kila aina ya ugonjwa na kumrudishia mfu uhai wake.
- Wakidhani ni safari ya kawaida, wanajikuta wakihitaji msaada unaobadilisha maisha yao.
Baada ya kusikia soga za kale ya kuwa kuna mti wa maajabu unaoweza kuponya kila ugonjwa na hata kumrudisha duniani yule aliyetangulia mbele za haki, Lily anamshawishi kaka yake kuungana naye kuutafuta mti huo.
Kabla haujaanza safari hii, nakushauri ufunge mkanda na uvalie mabuti yako kwani haitokuwa safari nyepesi. Ni safari ya mbugani ambayo ugumu wake ni sawa na kuambiwa uogelee katika mto wenye mamba ambao hawajaona chakula kwa wiki nzima.
Safari yetu inaanza na Lily Houghton ambaye maono yake ni kutafuta kitu cha kuokoa dunia na madhira ya kiafya yanayowakumba wanadamu.
Kwa kumtazama, Lilly ni mwana dada ambaye anapenda mishe mishe kwa muktadha huu, wazungu wanaweza sema anapenda “adventure” hivyo anaamua yeye na kaka yake kuutafuta mti unaoweza kubadili tasnia ya famasi daima.
Wasicho kijua ni kuwa, safari ya kuufata mti huo siyo rahisi kama walivyodhani. Ni safari ya uzima na mauti inayohitaji siyo akili tu, bali mkono unaoweza kurusha ngumi na viganja vinavyoweza kushika mapanga.
Wakati wakidhani safari yao ni rahisi, wanakutana na wasiyoyatarajia. Picha| Unlimited Viral News.
Lily akutana na nguvu za ziada.
Mti ambao watoto wa Houghton wanautafuta upo chini ya mto wa maajabu na wawili hao sio wa kwanza kuutafuta kwani ni mamia waliojaribu na kuishia njiani huku uhai wao ukimrudia yule aliyewapatia. Kuufikia, wanahitaji mtu ambaye anaujua mto huo kinaga ubaga.
“Kilicho nje huko, siyo safari ya kufurahia,” ni sauti ya Frank ambaye ndiye Lilly na kaka yake McGregor wanamhitaji kufanikisha safari yao.
Ipo hivi, ukimtazama Lilly unaweza kudhani Lilly ni mwanadada poa, mlimbwende ambaye anapenda kujipodoa lakini chini ya ngozi ya binti huyo ni mpiganaji ambaye Frank anabaki akimshangaa tena kwa mdomo wazi.
Mateke na ngumi kama za “Jean-Claude Van Damme” pamoja na sarakasi kama za mwanamuziki “Pink” ni vionjo vya hapa na pale unavyoweza kuviona kwake.
Nilikuambia awali, kuwa unahitaji buti zako kwa ajili ya safari hii. Zivae sasa kwani safari ndiyo inaanza.
Wakiwa safarini, watatu hao wanaanza kuona wasiyoyatarajia. Viumbe vilivyokufa vikirejea uhai wake vikitaka kuangamiza kila kilicho mbele yake, wanyama wa ajabu ambao mguso mmoja tu unatosha kukukutanisha na malaika mtoa roho na mengine mengi ambayo sihitaji kukumalizia uhondo wake nikisimulia.
Safari ya mwanzo wa penzi changa, umbali unaochochea watu kufahamiana, silaha za maangamizi na mahusiano yafaayo kutunzwa ni sehemu ya filamu hii ya Jungle Cruize.
Kama ulimmiss The Rock na filamu zake za “adventure”, hii itakufaa. Ukiitazama, tupe mrejesho wa kiasi ulichofurahia.
Kwa leo, tuishie hapa, hadi wiki ijayo.