November 24, 2024

Serikali ya Tanzania yaanza manunuzi ya treni za umeme

Wakati Serikali ikiendelea na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, imeanza mchakato wa ununuzi wa vichwa na jozi za treni za umeme ambazo zitapita katika reli hiyo itakapokamilika.

  • Imeingia mkataba na kampuni ya Hyundai Rotem ya Korea Kusini ya ununuzi wa vichwa 17 vya treni ya umeme na jozi 10 za treni za abiria.
  • Manunuzi hayo yatakagharimu zaidi ya Sh685 bilioni.
  • Treni hizo zitapita katika reli ya kisasa ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza. 

Mwanza. Wakati Serikali ikiendelea na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, imeanza mchakato wa ununuzi wa vichwa na jozi za treni za umeme ambazo zitapita katika reli hiyo itakapokamilika.

Shirika la Reli Tanzania  (TRC)  limetiliana saini na kampuni ya Hyundai Rotem ya Korea Kusini mkataba wa manunuzi ya vichwa 17 vya treni ya umeme na jozi 10 za treni za abiria zinazotumia umeme (Electrical Multiple  Unit (EMU).

Mkataba huo umesainiwa na pande zote mbili jana Julai 14, 2021 makao makuu ya TRC Dar es Salaam  ambapo gharama yake ni zaidi ya  Dola  za Marekani milioni 295.6 (zaidi ya Sh685 bilioni) ambapo kampuni hiyo itasanifu, kutengeneza na kuleta nchini. 

Aidha, TRC imesema kazi za mradi wa SGR zinaendela kwa awamu ya kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza. 

“Kwa kipande cha Dar es Salaam ujenzi umefikia asilimka 92, kwa kipande cha pili cha Morogoro – Makutupora ujenzi umefikia asilimia 65 na  kipande cha tano kutoka Mwanza hadi Isaka ujenzi umeshaanza” imeeleza taarifa ya TRC. 

Kulingana na mkataba wa ujenzi,  kipande cha kwanza kinatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi November 2021.

“Majaribio ya uendeshaji wa treni ya umeme yanatarajiwa kuanza  mwezi Desemba 2021 baada ya treni za umeme za majaribio na uendeshaji wa awali kuwasili,” imeeleza taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha TRC, Jamila Mbarouk.

Reli hiyo ya kisasa itakuwa na urefu usiopungua kilomita  2,561 ikiunganisha mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Kigoma, Katavi na nchi zinazokuwa na bandari za Rwanda, Burundi na Congo DRC.

Kwa mujibu wa TRC reli hiyo ambayo itakayokuwa na uwezo wa kupitisha treni zitakazoendeshwa kwa nishati ya umeme na yenye mwendo kasi usiopungua kilometa 160 kwa saa itasaidia kuongeza ajira kwa wazawa katika sekta na fani mbalimbali.

“Ongezeko la usafirishaji wa mizigo ambapo reli itabeba mzigo wa mpaka tani 10,000 kwa mkupuo sawa na uwezo wa maroli 500 ya mizigo,” imeeleza TRC na kubainisha kuwa itaokoa muda kwa usafiri wa abiria na mizigo ambapo itasaidia kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.