Hii ndiyo suluhu ya muwasho wa koo lako
muwasho huo husababishwa na mzio wa chakula au maambukizi yanayotokana na bakteria au virusi.
- Muwasho huo unasababishwa na mzio wa chakula au maambukizi ya kwenye koo.
- Kupata ahueni, unaweza kunywa maji ya moto huku ukienda hospitali.
- Unashauliwa kumuona mtaalamu wa afya kupata matibabu sahihi.
Dar es Salaam. Nikiwa nyumbani, kumsikia dada yangu akihangaika na koo lake asubuhi anapoamka ni jambo la kawaida.
Aamkapo, hutuamsha na wengine wote kwa sauti fulani ambayo husikika pale anapokuwa anatafuta suluhu ya muwasho wa koo lake.
“Koo linaniwasha” huniambia kila nimuulizapo kinachomsibu. Akijaribu kutafuta ahueni, kuna namna anafanya inayompa ahueni ya muda mfupi.
Ni vigumu kuiandika sauti hiyo lakini hutokana na kuvuta hewa kwa ndani huku akilazimisha ulimi ugusane na paa la kinywa chake, na kisha kitendo hicho hutengeneza mtetemo fulani kwenye sehemu ya koo inayowasha.
Baada ya kumfuatilia kwa muda mrefu, niligudua kuwa mara zote anazokuwa anafanya hayo, inakuwa ni usiku au siku ambayo nyumbani wamepika dagaa.
Kwa mujibu wa tovuti inayoandika masuala ya afya ya webmd muwasho wa koo husababishwa na mzio (alergies) au maambukizi katika eneo la koo yanayotokana na bakteria au virusi.
“Unaweza kuwashwa koo baada ya kukaa sehemu yenye moshi kwa muda mrefu, kuongea kwa muda mrefu au mwili kuishiwa maji,” inaeeleza webmd.
Ukiwa nyumbani, unaweza kunywa vinyaji vya moto kama chai au asali (vijiko viwili vya chai). Picha| Good Hoouse Keeping.
Unavyoweza kukabiliana na muwasho wa koo
Suluhu ya tatizo hilo hutofautiana kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kutokana visababishi vilivyochangia hali hiyo; moshi, kuishiwa maji au kuongea kwa muda mrefu.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo, unashauriwa kuonana na mtaalamu wa afya ili upate matibabu stahiki.
Wakati ukijiandaa kumuona daktari unaweza kujipatia msaada wa haraka ili kupunguza maumivu.
Tovuti ya masuala ya afya ya Healthline imeandika kuwa unapokuwa nyumbani, na kukutwa na hali hiyo, kunywa maji mengi na vimimiinika au kusukutua kwa maji ya vuguvugu yenye mchanganyiko wa chumvi.
“Kutumia bidhaa ambazo zinaweza kukupatia ganzi ya muda katika eno la koo zinaweza kukupa ahueni,” imeandika Healthline ikishauri mtu kwenda kumuona daktari baada ya kutumia njia hizo.
Kati ya bidhaa za kumpatia mtu ganzi ni pamoja na mafuta ya mkaratusi na dawa aina ya“benzocaine” na “menthol” ambazo kabla ya kutumia, inashauriwa kupata ruhusa kutoka kwa mtaalamu wa afya.
Pia unaweza kutumia maji ya moto au mchuzi kama njia ya kutafuta ahueni ya muwasho wa koo. Kama unajua una mzio na chakula fulani, haitokuwa busara kutumia mchuzi wake kupata ahueni.
Vitu vingine vinavyoshauliwa kwa matumizi ni vijiko viwili vya chai vya asali au vyakula vya baridi ikiwemo barafu na “icecream”.
Kwa atakayetumia asali, anashauriwa kutokumpatia mtoto wa chini ya mwaka mmoja kwani inaweza kumsababishia changamoto ya kiafya ya sumu ya chakula (food poisoing).
Siyo kila muwasho wa koo utaisha wenyewe, endapo muwasho huo utaendelea, unashauriwa kuonana na mtaalamu wa afya na umwambie kila kitu ulichotumia kabla na baada ya kupata muwasho.
Ukifahamu kitu kinachokusababishia muwasho, unashauriwa kuacha kukitumia. Inaweza kuwa chakula au mazingira. Pia inashauriwa kuwa na tabia ya kunawa mikono mara kwa mara ili kuepuk maambukizi yanayoweza kusababishwa na kula chakula chenye vimelea.
Vyanzo| WebMD na Helathline
Uthibitishaji, Dk Joshua Sultan.