November 24, 2024

Wafanyabiashara wana la kujifunza kuungua soko la Kariakoo?

wafanyabiashara jiji humu wamesema kuungua kwa soko hilo kumewaachia funzo kubwa hasa umuhimu wa kukata bima kwa ajili ya biashara zao.

  • Wamesema kuna umuhimu wa kukata bima ya biashara.
  • Waiomba Serikali kujenga miundmbinu ya kuzimia moto katika masoko yote.
  • Serikali yatoa maagizo mapya kuhusu usalama wa masoko nchini. 

Mwanza. Siku moja baada ya kuungua kwa soko kuu la Kariakoo jijini Dar es Salaam, wafanyabiashara wameiomba Serikali kuhakikisha wanaweka miundombinu ya kuzimia moto katika masoko ya jijini Mwanza ili kuepusha vifo na uharibufu wa bidhaa.

Pia wafanyabiashara jiji humu wamesema kuungua kwa soko hilo kumewaachia funzo kubwa hasa kukata bima kwa ajili ya biashara zao.

Mwenyekiti wa Soko Kuu mkoani Mwanza, Khamad Nchora amesema masoko mengi mkoani humo hayana miundombinu ya kuzimia moto ikiwemo mifumo ya maji, hali inayotishia usalama wa bidhaa zao pale jango la moto linapojitokeza.

“Nikiri kuwa hata hapa Mwanza masoko hayana mifumo ya miundombinu ya maji, hivyo ni vema Serikali inapojenga masoko makubwa kama haya wazingatie suala hilo ili kupunguza adha inayojitokeza,”amesema Nchora

Pia amependekeza kuboreshwa kwa mifumo ya umeme kila baada ya muda kwa kuwa inaweza kuchangia matukio kama hayo.

“Mifumo ya njia za umeme na maji huwa inafikia wakati inazeeka na kuchoka, mfano hilo soko la Kariakoo limejengwa miaka 1975 ni takribani miaka 45 kwa maana hiyo mifumo yake ilikua ishaanza kuzeeka,” amesema.

Mwenyekiti huyo pia ameiomba Serikali kuzingatia kutengeneza barabara zinazofikika kirahisi sokoni ili kupunguza changamoto hiyo.

Muonekano wa juu wa soko kuu la Kariakoo baada ya kuungua Julai 10, 2021. Picha| Global Publishers.

Wafanyabiashara wana la kujifunza?

Juma Hamsini ni mfanyabaishara wa mazao ya chakula katika Soko Kuu la Mwanza, amesema lipo la kujifunza kwenye janga la moto uliotokea Kariakoo. 

Amesema wafanyabaishara wengi hawana bima ya biashara zao na kuwa linapotokea tatizo kama hilo huanza upya na wengine kushindwa kuendelea kufanya biashara.

“Ni kuanza upya,   wafanyabiashara wengi bado tunaendesha biashara zetu kimazoea hatukati bima inapotokea tatizo kama hili ni kuanza upya,” amesema Hamsini huku akisema ataangalia namna ya kutafuta bima ya biashara.

Jafari Rashidi yeye anaungana na Hamsini kuwa wazo la kukatia bima biashara ni la msingi na ni msaada kwa siku za baadae. 

“Sote tunaishi bila kuijua kesho yetu hivyo ni vyema sana kuchukua hatua kabla ya ajali,” amesema.Sehemu ya soko kuu la Kimataifa la Samaki-Kirumba Mwaloni jijini Mwanza. Picha| Michuzi Blog.

Soko kuu la Kariakoo liliungua Julai 10 usiku, ambapo chanzo chake hakijajulikana mpaka sasa huku  wafanyabaishara 224 wakipoteza bidhaa zao.

Kutokana na changamoto hiyo, Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Ummy Mwalimu aliziagiza halmashauri zote kuhakikisha wanaweka miundombinu katika masoko yote itakayoweza kusaidia pindi ajali hizo zinapotokea.

Naye Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea soko hilo jana, amesema Serikali itaongea na benki ambazo baadhi ya wafanyabiashara walichukua mikopo ili kurefusha muda wa kulipa wakati wakitafuta namna ya kuinuka. 

“Tume itapata taarifa za kila mmoja mwenye mkopo rasmi kwenye taasisi za fedha ili tuzungumze nao waongeze muda waache kipindi hiki ili uweze kulipa hapo baadae utakapo kuwa umetulia,biashara imeungua naamini mabenki yatatuelewa na kuweka utaratibu mzuri,” alisema Majaliwa jana.