November 24, 2024

Wagonjwa 408 wa Corona wagundulika Tanzania

Hii ni mara ya pili kwa Tanzania kuweka hadharani takwimu za wagonjwa wa Corona tangu ilipositisha kutoa Mei mwaka 2020 ambapo ilikuwa imerekodi wagonjwa 509 na vifo 21.

  • Visa hivyo ni hadi Julai 8 mwaka huu.
  • Kati ya wagonjwa hao, 284 wanatumia mitungi ya oksijeni.
  • Serikali yawataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari.

Mwanza. Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema Tanzania imerekodi visa 408 vya wagonjwa wa Corona hadi kufikia Julai 8 mwaka huu.

Hii ni mara ya pili kwa Tanzania kuweka hadharani takwimu za wagonjwa wa Corona tangu ilipositisha kutoa Mei mwaka 2020 ambapo ilikuwa imerekodi wagonjwa 509 na vifo 21.  

Juni 25, 2021, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam alisema  Tanzania ina wagonjwa zaidi ya 100 wa wimbi la tatu la ugonjwa wa virusi vya corona.

Waziri wa wizara hiyo, Dk Dorothy Gwajima aliyekuwa akizungumza leo Julai 10, 2021 jijini Dodoma wakati akitoa elimu ya kujikinga na ugonjwa huo amesema kati ya wagonjwa hao 408 waliobanika, 284 wanatumia mitungi ya oksijeni. 

Dk Gwajima amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ikiwemo kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka ili kuushinda ugonjwa huo.