Simulizi ya kijana aliyeitosa ajira na kuzamia kwenye uchoraji
Baada ya kumaliza masomo yake ngazi ya shahada ya kwanza alipata ajira ambayo aliifanya kwa miezi mitatu na kubaini kuwa hayupo mahali sahihi.
- Ni Undare Mtaki aliyeajiriwa kama msanifu majengo.
- Anasema kazi ya uchoraji inampa furaha kuifanya na inamlipa kuliko taaluma yake.
- Anaamini katika kufanyia kazi ndoto na kusudi la kuishi duniani.
Dar es Salaam. “Ajira ngumu” ni sentensi ambayo utaipata kwa vijana waliohitimu vyuoni na kuingia mtaani wakitegemea kuokolewa na vyeti vyao.
Watakuambia wamezunguka ofisini, wameandika barua pepe na barua za kawaida bila mafanikio ya kufikia hata usaili.
Kwa Undare Mtaki, mhitimu kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) mwaka 2019, mambo yalikuwa tofauti baada ya kupata ajira na kisha kuitosa ndani ya miezimitatu ili afuate kule moyo wake ulipoelemea.
Baada ya kuhitimu elimu ya juu, Mtaki (28) aliajiriwa kwenye moja ya kampuni kama msanifu majengo lakini kazi hiyo ilimnyima muda wa kukinoa kipaji chake cha uchoraji wa picha.
“Kazi ile ilihitaji muda wangu mwingi kiasi cha kukosa nafasi ya kuchora. Niliifanya kwa kipindi kifupi nikaacha ili nifanye kazi ya uchoraji muda wote,” anasema Undare ambaye alipenda kuchora tangu akiwa mdogo.
Undare ni miongoni mwa vijana ambao fikra zao zimebadilika kuhusu ajira. Anafanya kile anachokipenda na siyo kusubiri kuajiriwa.
Kijana huyo ameamua kuchora picha za watu ambazo kitaaluma zinajulikana kama potraits kwa kutumia rangi, mchanga na mawe. Picha hizo huhusisha mchoro wa mtu kwa uhalisia na mfanano kiasi cha kuuliza kama ni picha ya kamera au ni mkono wa mtu ndio umechora.
Picha ya “Pamoja Rohoni” ni picha iliyochukua miezi mitatu kukamilika. Undare amesema “picha hii inakumbusha Watanzania kuwa licya ya baadhi ya viongozi wa nchi kututoka, bado hekima na waliyoyafanya yako pamoja nasi,”. Picha| Rodgers George.
Mwanzo wa safari ya uchoraji
Hatua aliyofikia Undare katika fani ya uchoraji imechangiwa na wazazi wake. Walipenda kuona mtoto wao akikua na kutafuta njia ya mafanikio inayompendeza. Kwao, furaha ya Undare ndiyo ilikua jambo la msingi kuliko kitu kingine chochote.
“Walikuwa wakininunulia vifaa vya kuchorea. Rangi, vitabu, karatasi na saa zingine walinunua picha zangu ili kunipa motisha,” Undare anasema huku akiweka wazi kuwa soko la kazi zake lilifunguka akiwa na miaka mitano na lilitoka kwa ndugu na marafiki.
Umaarufu wa uchoraji ulimfuata hadi alipokuwa shuleni kwani walimu nao walinufaika na kipaji chake hasa katika michoro ambayo ilipaswa kuchorwa ubaoni kwa ajili ya kufundishia wanafunzi.
“Nilikuwa ni yule mwanafunzi ambaye mwalimu akihitaji mchoro ubaoni ninaitwa mimi tu,” Undare anasema huku uso wake ukiwa na tabasamu la kujiamini.
Ajira yenye tabasamu
Baada ya kuacha ajira ya taaluma yake na kuanza kufanya uchoraji kama kazi yake rasmi, kijana huyo mwenye Shahada ya kwanza ya Usanifu Majengo amekiri kuwa uchoraji ni kazi ambayo anaifanya bila kuchoka.
Furaha yake ni kubadili rangi, brashi, na kanvasi za kucholea kuwa picha inayoweza kuibua hisia kwa mtu ambaye ataitazama.
“Bado nafanya kazi za usanifu lakini ni zile za mara moja moja ambazo pesa yake kweli inaridhisha kuzipatia muda wangu,” anasema Undare ambaye ich zake za #Shades of magufuli zimewaliza watu zaidi ya wanne.
Anasema sahada yake ya kwanza imempatia uwezo wa kufanya kazi zake za uchoraji kwa ufanisi zaidi kwa kujua malighafi nzuri na njia za kuandaa michoro yake ionekane kwa unadhifu mbele ya macho ya wateja wake.
Anatumia malighafi mbalimbali ikiwemo rangi za mafuta (acrylic paints), brashi kwa ajili ya kuchorea, penseli, vifutio, maji, mchanga pamoja na mawe.
“Mchanga ninaoutumia ni wa fukwe za Ziwa Victoria. Kwetu kuna mawe mengi sana hivyo ninatumia mawe pia kuongeza nakshi kwenye picha zangu,” anasema Undare.
Undani wa sanaa yake
Kazi aliyoichagua ni ya msimu. Upo msimu ambapo mwili wake unamtaka achore na hapo ndipo hujifungia kwenye studio yake iliyopo Mwanza na kuanza kuchora picha moja hadi nyingine.
Katika picha hizo, zipo ambazo huchukua hadi saa tatu, zipo zinazochukua siku mbili lakini zingine hutumia miezi mitatu kuzikamilisha.
“Kuna picha natumia brashi kuchora lakini zipo ambazo natumia mikono yangu mwenyewe. Hiyo hunipatia hisia kamili na picha hizo huwa na mguso wa aina yake,” anasema Undare.
Moja ya kazi kubwa aliyofanya ni kuchora picha za Hayati Rais John Magufuli ambazo zimetumika katika maonyesho yaliyojulikana kama “Shades of Magufuli” yaliyofanyika kwenye ukumbi wa The Drum uliopo Masaki Mkoani Dar es Salaam kuanzia Juni 28 na kufungwa Julai10, 2021.
Milima na mabonde ya safari ya sanaa
Haijalishi tabasamu linaloambatana na safari yeyote, kila safari huwa na mabonde na milima yake. Nyakati za furaha na zingine ambazo ni maumivu moyoni.
Kwa Undare Mtaki, mabonde na milima yake imekuwa ni upatikanaji wa malighafi zenye kiwango kizuri kwa ajili ya kuchora pamoja na gharama za rangi.
“Huwa ninatumia rangi nyingi sana hivyo picha moja pekee inaweza nigharimu rangi kuanzia Sh100,000. Hapo bado vitu vingine.” anasema kijana huyo ambaye soko la kazi zake ni ndani na nje ya nchi.
Mtaki huuza zaidi picha zake kwa watu binafsi, wasanii na mara kadhaa, amefanya kazi za sanaa katika ofisi mashughuli nchini.
Hata hivyo, sanaa imeendelea kuwa mlango wa kumfungulia Mtaki ndoto zake kwani kazi hiyo inamuingizia kipato kuliko hata mshahara wake wakati ameajiriwa.
“Nimefanya kazi za sanaa sehemu mbalimbali nchini ikiwemo moja ya hospitali za kimataifa, nimefanya maonyesho yangu na ninafurahi mwitikio wa watu kwenye kazi zangu umeendelea kunitia moyo,” anasema.
Matarajio yake ni kuwa na maonyesho yake walau mara mbili kila mwaka.
Tangazo