Serikali ya Tanzania kupitia upya mfumo wa kodi
Serikali imesema iko mbioni kufanya marekebisho ya sheria za kodi zikiwezo za taasisi za dini ili kutoa unafuu kwa walipaji.
- Hiyo ni kutokana na malalamiko ya watu zikiwemo taasisi za dini.
Mwanza.Serikali imesema iko mbioni kufanya marekebisho ya sheria za kodi zikiwezo za taasisi za dini ili kutoa unafuu kwa walipaji.
Akizungumza kwenye mkutano wa 31 wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) leo Julai 8, 2021 mjini Morogoro, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema amekuwa akipokea malalamiko mengi kuhusu kodi kwenye taasisi mbalimbali anazokutana nazo zikiwemo za dini.
Amesema toka aanze kukutana na taasisi za kidini kero kubwa imekuwa hiyo ya kodi.
Kiongozi huyo amesema wanalazimika kuzitoza kodi kutokana na baadhi kugeuza taasisi zao kuwa za kibiashara na si kutoa huduma kama zilivyosajiliwa.
“Suluhisho la hili ni kufanya kazi kwa uwazi na kuaminiana hili litasaidia kwa sekta inayojishughulisha na masuala ya kodi kukusanya kodi bila kikwazo chochote na kwa kuzingatia sheria,” amesema Rais Samia
Amesema tayari Serikali imeshaanza kuchukua hatua za kufanya marekebisho ya sheria ya kodi ambapo tayari imefuta baadhi ya tozo kwenye sekta ya elimu na ufundi stadi na kwamba wanaenda kuangalia mfumo wote wa kodi ili waweze kuzipunguza na kuzisamehe.
Amesema Serikali imekuwa na ushirikiano wa dhati na sekta binafsi katika kukuza uchumi pamoja na kuboresha mazingira ya kazi.
Serikali imeshaanza kuchukua hatua za kufanya marekebisho ya sheria ya kodi ambapo tayari imefuta baadhi ya tozo kwenye sekta ya elimu na ufundi stadi. Picha| Daily Sabah.
Na katika hilo amesema ndani ya miaka mitano, Serikali itahakikisha inaboresha uchumi shindani na shirikishi kwa taasisi zote binafsi na za dini.
Pia, itahakikisha inakuza uchumi wa viwandani, kuimarisha mazingira bora, kuimarisha uwekezaji pamoja na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja.
Rais Samia ameyasema hayo baada ya kupokea changamoto kutoka kwa Mwenyekiti wa CCT, Askofu Alinikisa Cheyo ambaye amebainisha kuwepo kwa mlundikano mkubwa wa kodi kwenye taasisi za dini.
Askofu Cheyo amesema taasisi zinazokusanya kodi zinaamini kuwa taasisi za kidini zinapata fedha kutoka kwa wananchi na hazifanyi kazi.
Amesema suala hilo si la kweli kwakuwa fedha zinazopatikana kwenye taasisi hiyo hutumika kulipa mishahara viongozi wanaotoa huduma.
“Siyo kweli kwamba fedha zinazopatikana hapo hazina kazi ya kufanya, zinatumika kulipa mishahara kwa viongozi wanaofanya huduma ya kiroho ili waweze kutoa cha rohoni na wao wapate cha mwilini, “amesema Askofu Cheyo