Bomoa bomoa vibanda vya wafanyabiashara ilivyoacha maumivu Mwanza
Ni vibanda vilivyopo katika mtaa wa Kirumba kati ambapo wamiliki wake wamepoteza uwekezaji waliofanya kwa muda mrefu.
- Ni vibanda vilivyopo katika mtaa wa Kirumba kati.
- Inadaiwa wafanyabiashara walikuwa wamepangishwa kinyume cha sheria.
- Waliobomolewa wabaki na maumivu kutokana na hasara waliyopata.
Mwanza. Wafanyabiashara wadogo wadogo katika Mkoa wa Mwanza leo wameamka na maumivu baada ya vibanda vyao vilivyopo katika mtaa wa Kirumba kati kubomolewa kwa madai ya amri ya Mahakama ya Baraza la Nyumba jiji hapa.
Vibanda hivyo vinavyotazamana na soko la Rock City Mall vimebomolewa baada ya baraza hilo la ardhi kuwaamuru wamachinga kuondoa vibanda na vifaa vyao ndani ya siku 14 kuanzia Juni 5, 2021
Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya mmiliki wa eneo ambalo vibanda vimevunjwa, Lauwrence Sandawe amesema wafanyabiashara hao walikuwa wamepangishwa kinyume cha sheria.
Amesema kwa miaka mingi mmiliki amekuwa akidai eneo lake ili aliendeleze lakini mtu aliyepewa kusimamia aliligomea hivyo kusababisha kwenda mahakamani.
Sandawe amesema baada ya mahakama kujiridhisha ilitoa notisi ya kuwaondoa wapangaji hao sita ambao wanadaiwa kufanya biashara katika eneo hilo isivyo halali.
“Kimsingi eneo lilikuwa na mvutano ambapo yule aliyekuwa anadai eneo ni la kwake alipangisha watu sita ambao nao waliongeza wapangaji wengine, Mahakama iliamuru waondolewe na ikaomba usimamizi wa polisi wakati zoezi likifanyika,” amesema Sandawe baada ya zoezi la ubomoaji kukamilika.
Baadhi ya vifaa vya wafanyabiashara wa mtaa wa Kirumba Kati vikiwa nje baada ya zoezi la kubomoa vibanda vyao. Picha| Mwananchi.
Ubomoaji ulivyoacha maumivu
Wafanyabiashara waliovunjiwa vibanda vyao wamedai kuwa wameonewa, jambo lililosababisha wapate hasara ya mamilioni ya fedha.
Mfanyabiashara, Yarid Athuman anayejishugulisha na banda la chakula ikiwemo kuchoma chipsi amesema amewekeza hapo kwa miaka sita na kabla ya kupata kitambulisho cha mjasirimali alikuwa anafuata sheria zote za wafanyabiashara.
Amesema eneo hilo alipangishiwa kwa gharama ya Sh4 milioni na amefanyi matengenezo ambapo hadi bomoa bomoa inaanza amepata hasara ya tatriban Sh9 milioni.
“Nimewekeza vitu vingi hapa gharama ambayo ni zaidi ya Sh9 milioni, lakini pia kuna ujanja umefanyika wa kuhamisha bikoni za zamani na kuleta mpya,” amesema Athuman.
Mnyabiashara mwingine, Fatuma Balele ambaye anadai amepata hasara ya Sh2 milioni kutokana na vitu alivyokuwa amewekeza amesema hakuwa miongoni mwa wanaodaiwa kuvamia eneo la mtu isipokuwa alikuwa kwenye kingo za barabara.
Hata wakati, zoezi hilo la ubomoaji likiendelea, wafanyakazi wanne wa kampuni ya kubeba mizigo ya Khimji walijeruhiwa baada ya kupigwa na shoti na umeme wakati wakihamisha moja ya kontena la wafanyabiashara hao.
Wafanyakazi hao walipata majeraha hayo baada ya winchi walilokuwa wamepanda kugusa nyaya za nishati hiyo na baadaye kukimbizwa hospitali.
Hata hivyo, viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza hawajasema chochote ikizingatiwa kuwa zoezi hilo ni utekelezaji wa hukumu iliyotolewa na mahakama.