November 24, 2024

Dhana potofu kuhusu na ugonjwa wa kipandauso

Baadhi ya watu wameendelea kuwa na dhana potofu dhidi ya ugonjwa huo ikiwemo kuhusisha na imani za kishirikina.

  • Ni pamoja na baadhi ya watu kuhusisha ugonjwa huo na ushirikina.
  • Wengine hufikiri kuwa ugonjwa huo ni wa mara moja tu.
  • Hata hivyo, ugonjwa huo hauna tiba bali mgonjwa hutibiwa kulingana na dalili anazopata.

Dar es Salaam. Licha ya kuwa ugonjwa wa kipandauso siyo kati ya magonjwa yanayozungumziwa sana kama ilivyo malaria na Ukimwi, ugonjwa huo umeendelea kusumbua watu wengi huku tiba yake ikiwa bado ni kitendawili.

Katika andiko lilopita, tumeelezea ugonjwa wa kipandauso na changamoto ambazo wahanga wake wanazipitia katika maisha yao ya kila siku. Katika andiko hili, kitakachozungumziwa ni imani na mtazamo wa jamii kuhusu ugonjwa huo.

Hata hivyo, baadhi ya watu wameendelea kuwa na dhana potofu dhidi ya ugonjwa huo ikiwemo kuhusisha na imani za kishirikina.

Balozi Togolani Mavura, msaidizi binafsi wa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete aliyekuwa akiongea katika uzinduzi wa kitabu cha “The Wave” cha mjasiriamali Rahma Baijun alisema baadhi ya watu umehusishwa ugonjwa huo na imani za kishirikina kwa sababu ya kujirudia rudia.

Kitabu hicho cha “The Wave” kinaelezea safari ya Rahma katika kukabiliana na kipandauso. 

Wapo wagonjwa wa kipandauso ambao wakiumwa hulazwa hospitalini kwa hadi mwezi mzima. Picha| High Mountain Health.

Hizi ni baadhi ya dhana potofu zinazozunguka ugonjwa wa kipandauso:

1. Kipandauso ni maumivu ya kichwa ya kawaida

Kwa baadhi, pale wanapoambiwa kuwa kuna kitu hakijafanyika kwa sababu mtu aliyetakiwa kukifanya alikuwa anaumwa kichwa, wanafikiri mtu huyo ni mzembe kwani maumivu ya kichwa yanahitaji kupoozwa na dawa za kutuliza maumivu na kisha kazi ziendelee kufanyika.

Kwa mujibu wa Mtaalam wa afya kutoka kituo cha afya cha TMH kilichopo Mwenge jijini Dar es Salaam, Dk Isaac Maro, maumivu ya kipandauso siyo ya kawaida na kwa baadhi, dawa za kutuliza maumivu hazifui dafu.

Dk Maro amesema asilimia 90 ya wagonjwa wa kipandauso wanashindwa kufanya kazi zao na hivyo kuathiri shughuli zao za kiuchumi.

“Kuna watoto wanashindwa kufanya vizuri darasani na wazazi wanadhani watoto hao hawana akili lakini kumbe wanaumwa kipandauso,” amesema Dk Maro.


2: Wagonjwa wa kipandauso wote ni sawa

Kama ilivyo kwa baadhi ya magojwa mengine kama malaria, ugonjwa wa kipandauso hutofautiana kiwango cha madhara kutoka kwa mtu mmoja na mwingine.

Kwa wengine wanaweza kuumwa kipandauso mara moja kwa mwaka, mara mbili na wengine wakipatwa na hali hiyo hadi mara nne kwa mwezi, jambo ambalo linakwamisha maendeleo ya shughuli zao.

Dk Maro amesema wapo watu ambao wakiumwa kipandauso, inawachukua hadi wiki nzima au zaidi kupona.

“Kikimshika kipandauso, anajifungia kwenye chumba chenye giza kwa hadi wiki nzima,” amesema Dk Maro akimuelezea mtu anayemfahamu anayeteseka na ugonjwa huo.

Wagonjwa wa kipandauso hushhindwa kutimiza majukumu yao kutokana na maumivu makali ya kichwa yanayochukua  muda mrefu kupona. Picha| Forbes.

3: Kipandauso kinatibika

Kwa jamii ya Tanzania, baadhi ya magonjwa yanasemekana kutokutibika kwa sababu ya kukosekana kwa teknolojia ambayo inaweza kung’amua ugonjwa unaosababisha baadhi ya dalili zinazoonekana.

Katika baadhi ya hospitali, wagonjwa huenda na kuambiwa kuwa hawaumwi chochote kwani vipimo vilivyochukuliwa vikiwemo vya damu, kinyesi na mkojo havionyeshi ugonjwa wowote.

Hivyo hivyo kwa ugonjwa wa kipandauso ambao baadhi ya watalamu wa afya hushindwa kuutambua na hivyo kuwapatia wagonjwa dawa za kutuliza maumivu ambazo zinaweza zisiwasaidie.

Mtaalamu wa afya kutoka moja ya hospitali jijini Dar es Salaam Dk Brendavida Kaseko amesema kwa ugonjwa wa kipandauso, kinachotibiwa ni dalili zinazoonekana lakini tiba ya ugonjwa wenyewe bado haijapatikana.

“Tunajaribu kumshauri mgonjwa njia za kuepukana na ugonjwa huo ikiwemo kumshauri kuonana na mwanasaikolojia endapo ana tatizo la msongo wa mawazo,” amesema Kaseko.

Dhana zingine ambazo zipo katika jamii ni kuwa ugonjwa wa kipandauso ni maumivuya kichwa tu lakini ukweli ni kuwa, ugonjwa huo huambatana na changamoto zingine za kiafya ikiwemo kutapika, upofu wa muda mfupi na upofu wa maisha.

“Wapo watu ambao wamepata kiharusi ikiwa sababu ya kipandauso,” amesema Dk Maro.

Katika andiko linalofuata, tutaangazia matibabu yanayomfaa mtu ambaye anaumwa kipandauso na njia nzuri za kujiepusha na ugonjwa huo usikupate.