November 24, 2024

Mwongozo wa utoaji wa chanjo ya Corona kwa watoto

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema majaribio ya chanjo ya ugonjwa huo kwa watoto wadogo yanaendelea na itatoa mwongozo wa utoaji kwa kundi hilo itakapokamilisha utafiti wa kisayansi.

  • Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema linafanya majaribio ya chanjo ya Corona kwa watoto.
  • Zikikamilika litatoa mwongozo wa utoaji wa chanjo hizo.
  • Lashauri watoto wa kuanzia miaka 12 waendelea kupewa chanjo ya Pfizer/BionTech. 

Mwanza. Wakati dunia akiendelea kutengeneza na kusambaza chanjo za Corona, Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema majaribio ya chanjo ya ugonjwa huo kwa watoto wadogo yanaendelea na itatoa mwongozo wa utoaji kwa kundi hilo itakapokamilisha utafiti wa kisayansi. 

WHO katika taarifa yake kuhusu mwongozo wa utoaji wa chanjo za Corona kwa watoto iliyotolewa Juni 22, 2021 imeeleza kuwa kwa sasa hakuna uharaka wa kuwapatia watoto wadogo chanjo kwa sababu hawako katika hatari kubwa ya kupata COVID-19 kama wazee.

Wengine ambao wanapewa kipaumbele kwa sasa ni watu ambao wako kwenye mazingira hatarishi ya kuwahudumia wagonjwa wakiwemo wahudumu wa afya. 

“Ushahidi zaidi unahitajika kabla ya kupendekeza watoto kupewa chanjo za Corona za aina tofauti kupambana na ugonjwa huo,” imesema sehemu ya taarifa ya WHO. 

Hata hivyo, timu ya wataalam washauri wa WHO (SUGE) imethibitisha kuwa chanjo aina ya Pfizer/BionTech inawafaa watu wenye umri kuanzia miaka 12 na kuendelea.

“Watoto wenye umri kati ya miaka 12 na 15 ambao wako katika hatari wanaweza kupewa hii chanjo sambamba na makundi mengine yaliyopewa kipaumbele,” imeeleza WHO ikitoa ufanunuzi kuhusu chanjo ya Corona kwa watoto. 

Shirika hilo limesisitiza kuwa majaribio ya chanjo kwa watoto yanaendelea na itatoa taarifa kamili ya mwongozo wa utoaji chanjo kwa kundi hilo baada ya kukamilika kwa ushahidi wa kisayansi na mabadiliko ya sera za chanjo za Corona. 

Kwa sasa, imeshauri watoto wa kuanzia miaka 12 waendelee kupewa chanjo ya Pfizer/BionTech ambayo ndiyo imependekezwa kwa kundi hilo. 

Hadi kufikia Juni 22, 2021, dozi bilioni 2.5 za chanjo dhidi ya Corona zimetolewa na kusambazwa katika maeneo mbalimbali duniani ili kuwakinga watu na ugonjwa huo ambao maambukizi yake yanaongezeka kila siku.

Takwimu za WHO za hadi Juni 23 zinaeleza kuwa watu milioni 178.8 wameambukizwa ugonjwa huo na kusababisha vifo vya watu milioni 3.8 duniani kote.