November 24, 2024

Ubunifu kwa wanahabari utakavyosaidia kupunguza ukatili wa kijinsia Tanzania

Watakiwa kushirikiana na wadau wa maendeleo katika mapambano hayo.

  • Ni kwa wanahabari kuwa wabunifu wakati kuandaa habari zao.
  • Kujikita katika uandishi wa masuala na takwimu.
  • Pia watakiwa kushirikiana na wadau wa maendeleo katika mapambano hayo.

Waandishi wa habari wa Tanzania wametakiwa kuwa wabunifu ili kuandika na kutoa habari zenye mchango wa kutokomeza vitendo vya ukatili hasa wanavyofanyiwa wanawake na watoto nchini.

Mkurugenzi Mtendaji na Mhariri Mkuu wa wa kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa, Nuzulack Dausen amesema moja ya mbinu zinazoweza kutumiwa na wanahabari kutokomeza ukatili wa kijinsia kwenye jamii ni kuwa wabunifu katika uandaaji wa maudhui yanayotumiwa kwenye vyombo vya habari.

“Mbinu muhimu tunayoweza kutumia kama wanahabari ni kuwa wabunifu katika kuandaa maudhui yetu kwenye magazeti, televisheni, radio au hata mtandaoni ili kuwa viungo muhimu cha kutokomeza ukatili wa kijinsia kwenye jamii zetu,” amesema Dausen.

Amesema mbinu mbalimbali kama matumizi ya takwimu, masimulizi yanayoonyesha uhalisia na utengenezaji wa maudhui ya kidigitali “multimedia content”  yanaweza kusaidia habari kueleweka na Watanzania na hivyo kupunguza ukatili wa kijnsia.

Dausen alikuwa akizungumza leo Juni 23, 2021 mkoani Morogoro katika mkutano uliowakutanisha wadau mbalimbali kujadili namna ya kuimarisha utendaji wa vyombo vya habari katika kuripoti ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto nchini.

Mjumbe wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena amesisitiza wanahabari kujikita katika uchambuzi wa matukio na habari kuliko kufanya uandishi uliozoeleka hasa katika kuripoti matukio ya unyanyasaji wa kijinsia.

“Waandishi wanapaswa kujua masimulizi ni muhimu sana katika kuripoti matukio. Ukiripoti habari bila kuweka uchambuzi na kueleza kwa kina maana ya unachoandika huo sio uandishi wa kisasa”, amesema Meena.

Wadau hao wamesema vyombo vya habari ni nyenzo muhimu ya kutokomeza ukatili wa kijinsia ikiwa wanahabari watajengewa uwezo wa kuripoti kwa usahihi habari hizo.

Ukatili wa kijinsia umekuwa ukiwarudisha nyuma wanawake kiuchumi na kielimu na hivyo kuchangia kuendeleza umaskini kwenye jamii.

Mkutano huo ulioanza Juni 22, 2021pia unalenga kuhamasisha wadau wa maendeleo kufanya kazi kwa karibu na vyombo vya habari ili kutokomeza ukatili wa kijinsia, tatizo ambalo limeshamiri kwenye jamii.

Nukta Africa ni miongoni mwa wahudhuriaji wa mkutano huo uliondaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) ukihusisha wadau mbalimbali ikiwemo Wizara ya Habari, Utamaduni, Sana’a na Michezo, TEF, Twaweza na Chama cha Waandishi Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa).