November 24, 2024

Tabia zitakazokusaidia kuepuka madhara ya unywaji wa pombe uliopitiliza-2

Licha ya kuwa pombe ni sehemu ya starehe, kinywaji hicho kinaambatana na madhara mbalimbali ya kiafya kama itatumiwa isivyo.

  • Madhara  ya matumizi ya pombe yaliyokithiri ni pamoja na saratani na vidonda vya tumbo.
  • Inashauriwa kutumia kiwango kidogo cha pombe yenye manufaa kiafya.
  • Kuacha pombe inawezekana kwa mtu ambaye ana nia ya dhati.

Dar es Salaam. Katika makala iliyopita, tuliangazia tabia ambazo mtu anaweza kuzifuata ili kuepuka matumizi ya pombe yaliyopitiliza. 

Licha ya kuwa pombe ni sehemu ya starehe, kinywaji hicho kinaambatana na madhara mbalimbali ya kiafya kama itatumiwa isivyo.

Katika makala haya, tunaangazia madhara ya matumizi ya pombe kiafya na kwa ambao tayari wameathirika na unywaji wa pombe, nini wafanye ili kurudi katika hali ya kawaida.

Mtaalamu wa masuala ya afya kutoka kliniki ya utunzaji wa afya kwa njia za asili ya Cornwell iliyopo Victoria jijini Dar es Salaam Dk Elizabeth Lema, amesema matumizi ya pombe kupita kiasi ni hatari kwa afya ya mtumiaji kwani yanaambatana na changamoto za kiafya za kudumu ikiwemo kisukari.

Dk Lema amesema, matumizi ya kitu chochote kuzidi kiasi ni hatari ikiwemo pombe ambayo matumizi yake kuzidi kiwango ni sababu ya magonjwa ya moyo, matatizo ya figo na kongosho.

“Matumizi ya pombe kwa muda mrefu yaani kila siku yanasababisha kupungua kwa uwezo wa ubongo, kwa mujibu wa tafiti mbalimbali duniani. Pia ni chanzo kikuu cha kuharibika kwa kongosho na ini ambayo itaharibu uwiano wa sukari mwilini,” amesema Dk Lema wakati akiongea  na Nukta Habari (www.nukta.co.tz).

Kunywa pombe uiendeshe na siyopombe ikuendeshe. Picha| Freepik.

Uchovu na matatizo yasiyokoma

Kutumia pombe kupita kiasi pia ni sababu ya watumiaji wake kuhisi uchovu usio kuwa wa kawaida, jambo ambalo linaweza kuathiri utendaji kazi wao wa kila siku.

Mfano kwa mtu ambaye ametumia pombe nyingi kabla ya kulala, kuna uwezekano mkubwa wa mtu huyo kuchelewa kuamka au kuona uvivu wakati wa kuamka na hata kusinzia kazini na katika vyombo vya usafiri.

“Kuna wengine wanafikia hali kama hajanywa pombe hajisikii vizuri. Hiyo siyo hatua nzuri,” amesema daktari huyo. 

Matatizo mengine yanayoambatana na matumizi ya kukithiri ya pombe ni pamoja na tumbo kujaa gesi na vidonda vya tumbo na kwa wengine hufikia hali ya kupata saratani ya ini.

Siyo kila pombe ni mbaya

Wakati wataalamu wa afya wakisisitiza watu kuacha matumizi ya pombe, kituo cha matibabu cha Garden State cha New Jersey cha nchini Marekani kupitia tovuti yake kimeainisha kuwa pombe ziko katika madaraja mbalimbali kutoka zile za kawaida hadi kali zaidi.

Na kila pombe ina kiwango chake cha kilevi ambacho kama mtu hatazingatia basi anaweza kupata madhara makubwa ya kiafya. 

Kwa kawaida, pombe ambayo ina kiwango cha kilevi zaidi ya asilimia 40 inahitaji umakini katika matumizi yake, hivyo siyo ya kuparamia kwani zipo pombe ambazo zina hadi asilimia 95.

Mkazi wa Dar es Salaam, Fredrick Kiula amesema zipo pombe ambazo hulipuka pale zinapokuwa karibu na moto hivyo ni vyema kufahamu pombe ambayo unatumia na kuepuka kujaribu jaribu vitu bila kuwa na wataalamu.

“Muda mwingine mtu una mawazo hivyo ukienda sehemu ya kunywa unataka kulewa mapema. Utasikia mtu anamuambia bartender (mhudumu) ampe kali kuliko zote, kama mhudumu huyo naye hajui mambo, ataendelea kumpa tu mtu pombe kwa sababu yeye anaingiza hela,” amesema Kiula.

Mdau huyo wa pombe ameshauri kusoma kiwango cha kilevi ambacho kinaambatana na pombe utakayoagizia kabla ya kunywa.

Kwa watumiaji wa wine, glasi moja wakati wa chakula inashauriwa kiafya. Picha| Freepik.com

Pombe nzuri ni ipi?

Licha ya kuwa kila mtu ana mapendeleo yake, siyo kila pombe ni salama na siyo kila pombe ni mbaya endapo itanyweka kwa utaratibu na kwa kuzingatia kilevi chake. 

Dk Elizabeth amesema inashauriwa mtu anywe mvinyo (wine) mwekundu kwa wastani kwa ajili ya faida za kiafya ikiwemo kuepusha magonjwa ya moyo, kupunguza uwezekano wa kupata kiharusi na baadhi ya saratani ikiwemo ya mapafu.

“Kwa wiki ukinywa glasi mbili au glasi moja wakati wa chakula siyo mbaya,” amesema Dk Lema.

Ni muhimu kufahamu kuwa matumizi ya pombe yanatakiwa kuwa ya wastani kwa kiasi ambacho mtu anayekunywa aweze kujisimamia bila kuathiri afya yake na shughuli za watu wengine. 

Kwa lugha nyingine ni sawa na kusema, mnywaji aiendeshe pombe na siyo pombe imuendeshe mnywaji.