November 27, 2024

Maoni mchanganyiko pendekezo la tozo kwenye laini za simu Tanzania

Watanzania wamesema mapendekezo hayo yanaweza kuathiri biashara na sekta ya elimu.

  • Baadhi wasema tozo hizo zinaambatana na tamu na chungu kwa Watanzania.
  • Huenda tozo hizo zikapunguza uhalifu wa njia ya simu.
  • Serikali imeshuriwa kuangazia vyanzo vingine vya kukusanya mapato.

Dar es Salaam. Siku chache baada ya Serikali kutoa mapendekezo juu ya kuanza kukata tozo kwenye kila laini kila siku, baadhi ya Watanzania wamesema uamuzi huo utawazidishia maumivu kutokana na kuongeza gharama za huku baadhi wakisema wameachwa gizani juu ya namna tozo hiyo itakavyotekelezwa. 

Wakati akisilisha Bajeti Kuu ya Serikali Juni10, 2021, Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba alisema Serikali inapendekeza kutoza kiasi cha Sh10 hadi Sh200 kwa siku kwa kila laini ya simu kulingana na uwezo wa kuongeza salio kwa watumiaji. 

“Pendekezo hili litapelekea kuongeza mapato ya Serikali kiasi cha Sh396.3 bilioni,” alisema Dk Nchemba. 

Pendekezo hilo ni miongoni mwa mapendekezo yaliyojumuishwa kwenye muswada wa Sheria ya Fedha mwaka 2021 unaotarajiwa kupitishwa na Bunge kabla ya shughuli za bunge kumalizika mwezi huu. 

Serikali imependekeza kuboresha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Epoca)  ya mwaka 2010 ili kuanzisha tozo hiyo mpya katika mawasiliano ya simu ambayo ni muhimu katika shughuli za kijamii na uchumi. 

Hata hivyo, mapendekezo hayo yameibua upinzani na maswali lukuki miongoni mwa watumiaji wa simu za mkononi huku wengine wakiainisha mazuri yatakayoambatana na kupitishwa kwa mapendekezo hayo na mambo ambayo huenda yakasumbua Watanzania.

Mkazi wa Dar es Salaam Mike Roosevelt amesema yupo njiapanda juu ya njia itakayotumiaka kupata fedha hiyo kila siku hasa ikizingatiwa kuwa watu wengi hununua vifurushi vya wiki, siku tatu hadi mwezi ili kuweza kumudu gharama za mawasiliano. 

“Zipo sehemu ambako vocha ya Sh500 inauzwa Sh600 ili walau muuzaje atengeneze faida kutokana na umbali anaofuata vocha. Serikali ikisema gharama ya vocha iongezeke, itawaumiza watu kama hao waliopo maeneo ya vijijini kwa kuwa bei itapanda zaidi ya hapo,” amesema Roosevelt.

Roosevelt amesema haitokuwa na maana kwa mtu kuanza kulipia umiliki wa laini ya simu ambayo tayari anaigharamia kwa kununua vocha mara kwa mara huku kwa mwaka huu ikiwa tayari bei za vifurushi nayo ikiwa imepanda.

Mawasilianoya simu ni chachu kwa biashara. Kuyabana kwa kodi itayumbisha biashara za baadhi. Picha| Google Images.

Itaongeza gharama ufanyaji biashara wajasiriamali

Kwa mapendekezo hayo ya Serikali kulipitia tozo ya laini ya Sh10 hadi 200 kulingana na uwezo wa mtu kuweka salio ina maana kuwa watu ambao huweka salio kubwa au mara kwa mara, huenda wakalipa fedha nyingi zaidi kuliko ambaye huweka mara moja moja.

Mjasiliamali wa mtandaoni kutoka jijini Dar es Salaam MaryAnn Segese ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa yeye huweka salio mara  kwa mara ili kuwasiliana na wateja na kwa aina ya biashara yake hapaswi kukosa mtandao hata kwa dakika moja.

Muuzaji huyo wa vitu vya urembo na vipodozi amesema iwapo  laini yake itachaguliwa kuingia katika kundi la kulipa Sh200 itamuongezea gharama za kuendesha biashara yake tofauti na ilivyosasa. 

“Sasa wakisema wanikate Sh200 kwa siku inamaanisha ndani ya siku 10, nimelipa Sh2,000 na kwa mwaka Serikali nitatakiwa kuilipa Sh73,000. Haya una laini mbili hapo inakuaje?” amehoji Segese.

Itasaidia kupungua kwa uhalifu

Baadhi ya watumiaji wa mawasiliano wanaamini kuwa uamuzi huo wa Serikali utasaidia kupunguza uhalifu mtandaoni kwa kuwa watu hawatapenda kuwa na laini nyingi zitakazowagharimu kila siku. 

Licha ya Serikali kuweka sheria ya kusajili laini kwa alama za vidole, bado uhalifu umeendelea ukiwemo utapeli wa “tuna hiyo hela kwa namba hii” ambao umesababisha baadhi ya watu kutapeliwa pesa. 

Mkazi wa Shinyanga, Monica Meshack amesema pale kila mtu atakapoanza kulipia laini yake, itakuwa ni vyema kwa kuwa uhalifu utapungua.

Meshack ambaye ni mjasiriamali wa kusaga nafaka ameiambia Nukta Habari kuwa kwa sasa watu wanamiliki laini kiholela kwa sababu ni bure na wana uwezo wa kumiliki laini zaidi ya moja bila shida yoyote.

“Sheria ni kumiliki laini moja kwa kila mtandao. Tuna Tigo, Voda, Halotel, Zantel, Airtel na wapo wanaomiliki laini kote huko kazi kuchagua tu ipi ikae kwenye simu. Wakianza kulipia ndio wataona umuhimu wa kuwa na laini moja na kutulia na mtandao mmoja,” amesema Meshack.

Wapo wasionunua vocha wenyewe, itakuwaje?

Baadhi ya watumiaji wana hofu kuwa wale wenye wategemezi wengi kama watoto na wazee wao watalazimika kutoboa zaidi mifuko yao kuhakikisha wapendwa wanabaki kwenye mawasiliano kwa kuwa wao ndiyo huwanunulia vocha mara kwa mara. 

Kwa Kennedy Luhende Mkazi wa Morogoro amesema tozo hizo zitaongeza gharama ya maisha kwa wengi ambao wanahudumia wanafamilia ikiwemo wazazi na wanafunzi.

Luhende amesema vifurushi vya intaneti kwa wanafunzi tayari ni ghali  na pale mwanafunzi anapolazimika kulipia tozo ya kumiliki laini tena kila siku, huenda ikaathiri hata kwenye sekta ya elimu.

“Wapo wazazi wananunulia salio wazazi wao, watoto wao na wazazi wenzao sasa hapo ikija gharama ya kulipia laini nazo watalipa wao,” amesema Luhende.

Kwa wasionunua vocha wenyewe, huenda mapendekezo hayo yakawakandamiza wanaowategemea. Picha| Google Images.

Umuhimu wa makato hayo uwekwe wazi

Mfanyabiashara wa viatu jijini Dar es Salaam Zipporah Zealot amesema watu wengi hawajui wananufaikaje na tozo hizo zilizoanishwa kwenye mapendekezo ya bajeti hivyo waelimishwe ipasavyo. 

“Watu wajue zaidi nini kinalengwa na wao wanafaidika vipi au wanachangia nini hasa wanapolipia hiyo Sh200. Waelekezwe faida ya kulipia ni ipi ikilinganishwa na zamani,” amesema. 

Serikali iangazie vyanzo vingine vya kukusanya pato

Kwa dunia ya sasa ambayo teknolojia ya mawasiliano ni muhimu kwa biashara na maendeleo ya uchumi, baadhi wanaishauri Serikali kuangazia vyanzo vingine vya mapato ili kurahisisha mawasiliano badala ya kuyabana kwa kuongeza kodi na tozo.

Mchambuzi wa masuala ya kiuchumi Walter Nguma ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa Serikali inaweza kuangazia vyanzo vingine vya mapato na kuacha mawasiliano yawe huru.

Mchumi huyo amesema hivi karibuni mkutano wa mataifa saba yanayoongoza kiuchumi ulimwenguni (G7) yamependekeza makampuni makubwa ya teknolojia kulipa asilimia 10 ya mapato yake katika nchi amabazo yanatoa huduma.

Mfano, kwa Tanzania ambayo inahudumiwa na Google, Instagram, Facebook ambazo pia hujiingizia kipato kwa matangazo zitatakiwa kulilipa taifa asilimia 10 ya mapato yake katika nchi husika. 

“Serikali  itapata makusanyo lakini kutakuwa na ugumu kwa wananchi. Biashara nyingi kwa sasa zinategemea mawasiliano na kumuongezea mwananchi tozo ni kumuongezea mzigo hivyo kushindwa kuona msaada wa Serikali katika kurahisisha biashara,” amesema Nguma.

Endapo mapendekezo hayo ya Serikali yatahidhinishwa na Bunge, yataanza kufanya kazi Julai mosi mwaka wakati mwaka mpya wa fedha wa 2021/22 utakapoanza.