Waziri wa afya Tanzania ahimiza uvaaji barakoa kwenye mikusanyiko
Barakoa ni kati ya njia ya kujikinga na magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya hewa ikiwemo Covid-19.
- Waziri Dorothy Gwajima amesema matumizi ya barakoa yatawasaidia Watanzania kujikinga na maambukizi ya wimbi la tatu la ugonjwa wa Corona.
Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Dorothy Gwajima amewataka Watanzania kutumia barakoa pale wanapokuwa katika maeneo yenye mikusanyiko ili kujikinga na maradhi yakiwemo ya Covid-19.
Uvaaji wa barakoa umekuwa ukisisitizwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na mashirika ya kimataifa kwa kuwa ni moja ya njia madhubuti za kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona.
“Naomba niwakumbushe kwamba katika mazingira kama hayo ambayo tunakuwa tumesongamana kidogo ni vema tukafanya matumizi ya barakoa,” alisema Dk Gwajima Juni13, 2021 jijini Mwanza.
Miongoni mwa shughuli za mikusanyiko mikubwa Tanzania ni mikutano, sherehe, makongamano na michezo. Tofauti na mataifa mengine ulimwenguni, Tanzania haikuzuia raia wake kufanya shughuli zao za kila siku kwa kutoweka zuio la kutoka nje yaani kwa kimombo “lockdown”.
Katikati mwa Machi 2020 baada ya kuripoti kisa cha kwanza cha Covid-19, Tanzania ilizuia shughuli za michezo, matamasha na kufunga shule na vyuo kabla ya kufunguliwa mwishoni mwa Mei mwaka huo.
Barakoa ni kati ya njia ya kujikinga na magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya hewa ikiwemo Covid-19. Picha DW.
Waziri Gwajima amesema matumizi ya barakoa yatawasaidia Watanzania kujikinga na maambukizi ya wimbi la tatu la ugonjwa wa Corona ambao bado unasumbua mataifa mengine zikiwemo nchi za Brazil na India.
“Sijakuambia ukienda shambani kulima uvae barakoa sijakuambia ukikaa kwenye hewa kubwa ambayo mzunguko wake ni mzuri uvae barakoa kwa sababu tunasema hivi, huwezi kuvaa barakoa masaa 24.
“Kuna mazingira ukishafika, unaona kabisa hapa kuna msongamano hewa haizunguki vizuri hapa lazima nivae barakoa. Tutembee nazo,” amesema Dk Gwajima ambaye ameweka wazi kuwa hata yeye anatembea na barakoa yake.
Msisitizo wa matumizi ya barakoa pia umekuwa ukitolewa na Rais Samia ambaye katika mkutano wake na Wazee wa jijini Dar es Salaam, Rais Samia alisema matumizi ya barakoa ni muhimu hususan katika mikusanyiko mikubwa ili kuwakinga watu waliopo hatarini kupata maradhi hayo wakiwemo wazee.
Rais Samia amekuwa mfano wa matumizi ya barakoa baada ya kuonekana kuvalia nyenzo hiyo katika maeneo mbalimbali ya mikusanyiko tangu Mei mwanzoni mwaka huu.
Mbali na hayo, njia zingine ambazo zinashauriwa kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa wa Corona ni pamoja na kunawa mikono kwa kutumia maji tiririka na sabuni, kutumia vitakasa mikono, kupeana umbali wa mita moja kati yako na mtu mwingine pamoja na kuepuka misongamano isiyo ya lazima.