November 24, 2024

Rais Samia ashtushwa gharama kubwa ujenzi jengo la BoT Mwanza

Jengo hilo lililopo Mwanza latumia bilioni 42 kujengwa huku Rais akieleza kuwa ataongea na BoT.

  • Jengo hilo lililopo Mwanza latumia bilioni 42 kujengwa huku Rais akieleza kuwa ataongea na BoT.

Mwanza. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameonyesha kushitushwa na gharama iliyotumika katika ujenzi wa jengo la Benki Kuu Tanzania (BoT) Kanda ya Mwanza baada ya kuelezwa kujengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh42 bilioni.

Kati ya fedha hizo kiasi cha Sh23.37 bilioni ni kwa ajili ya ujenzi wa jengo lenye gorofa tano kwenda juu na gorofa tatu kushuka chini huku kiasi cha Sh17.73 bilioni ni kwa ajili ya kuweka mifumo mbalimbali itakayosaidia kuendesha jengo hilo.

Hata hivyo, Rais Samia amesema atazungumza na uongozi wa benki kujua namna fedha hizo zilivyotumika huku akiwaeleza kazi iliyompeleka hapo ni kwenda kuzindua.

“Gharama za ujenzi wa jengo hili zimenisisimua mishipa ya damu ila tutajadiliana baadae kuona namna zilivyotumika,” amesema Samia.

Rais Samia yupo mkoani Mwanza katika ziara ya siku tatu ambapo atashiriki uzinduzi na ukaguzi wa miradi mbalimbali katika mkoa huo wa kanda ya ziwa.

Kiongozi huyo wa juu wa nchi amesema kukamilika kwa jengo hilo kutaongeza mandhari ya jiji la Mwanza na hivyo kulifanya jiji hilo kuwa kitovu cha uchumi wa kati kwenye nchi zenye maziwa makuu.

Pamoja na mambo mengine, Rais Samia ameiagiza BoT kuangalia namna ya kupunguza riba na masharti magumu ili kuwapa fursa wananchi waweze kukopa kwenye mabenki na kukuza uchumi.

“Tunataka machinga anayeuza barabarani leo, kesho awe majasirimali hivyo niombe BoT kushughulikia suala hilo na angalau riba iwe chini ya asilimia 10,” amesema Rais Samia akieleza kwa sasa riba zilizopo zipo juu sana.

Hadi sasa sehemu kubwa ya riba za mikopo ni zaidi ya asilimia 16 katika taasisi nyingi za kibenki Tanzania.

Rais huyo amesema changamoto nyingine inayokwamisha ukuaji wa uchumi ni kutoa kwa mikopo kwa muda mfupi hali inayosababisha wengi kushindwa kumudu hivyo ameagiza muda uogezwe ili kuwapa wakopaji muda mrefu wakiwemo wakulima na watu wenye viwanda vya madini.

Gavana wa BOT, Florens Luoga amesema jengo hilo ni miongoni mwa tawi la awali nchini lililojengwa miaka ya 1980 na linahudumia mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Ujenzi wa jengo hili jipya ulianza Juni 2015 na umekalimika Oktoba 2020 na Aprili mwaka huu walianza kuhamishia vitu na kwamba ndani ya jengo hilo kuna eneo la kuhifadhi na kuchakata noti pamoja na ofisi za watumishi na viwanja vya michezo.