October 6, 2024

Rais Samia ageukia kuongeza wanawake katika fursa za kidijitali Tanzania

Amesema serikali itajenga shule zakufundisha masomo ya sayansi kila mkoa kwa ajili ya wasichana.

  • Amesema watoto wa kike wanajitenga na masuala ya kiteknolojia ikilinganishwa na watoto wa kiume.
  • Amesema Serikali itajenga shule katika kila mkoa kwa ajili ya kufundisha wasichana masomo ya sayansi.
  • Pia amesihi jamii kuepukana na dhana potofu dhidi ya mwanamke.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewashauri wanawake kuchangamkia masuala ya kidijitali ili kuendana na kasi ya kiteknolojia ambayo inaendesha dunia kwa sasa na kupata fursa za kiuchumi sawa na wanazopata wanaume. 

Rais Samia amesema uwiano wa wanawake na wanaume katika masuala ya kidijitali bado hauridhishi kwa sababu wavulana wamechangamkia masuala hayo ya kisayansi na teknolojia kuliko watoto wa kike.

Hii ni mara ya kwanza kiongozi huyo wa juu anazungumzia kwa undani namna ya kuziba mwanya uliopo katika ya wanawake na wanaume katika kupata fursa za kidijitali (digital divide) ambalo ni tatizo linalokumba mataifa mengi ulimwenguni. 

“Leo hii unawakuta wavulana wapo vibandani bandani wamejiajiri kutumia mifumo hii ya kidijitali lakini wa kike nenda kawakute kwenye kuuza nyanya, kuuza michicha lakini kule ukiwakuta ni kidogo sana,” amesema Rais Samia wakati akizungumza na wanawake jijini Dodoma Juni 8 mwaka huu. 

Rais Samia amesema hata yeye anapokwama kitu kidogo katika matumizi ya simu yake mara nyingi husaidiwa na mjukuu wake wa kiume “Ibra” mwenye miaka 9 ambaye huitizama simu yake na kumsaidia.

Rais Samia ameisihi jamii kuachana na imani potofu juu ya wanawake na ushiriki wao katika mambo ya maendeleo. Picha| Ikulu Tanzania.

Hata hivyo, Rais Samia amesema mjukuu wake wa kike, “Samia”, mara zote hajui jinsi ya kumsaidia pale simu yake inapomsumbua na huwa anamshauri kumwita Ibra kumsaidia.

Mkuu huyo wa nchi amesema endapo wasichana watajihusisha na masuala ya kidijitali, itapanua wigo wa ajira na kuchochea maendeleo katika jamii.

Ili kukabiliana na uhaba wa wanawake katika masuala ya dijitali, Rais Samia amesema kuanzia mwezi Julai 2021, Serikali itaanza kutekeleza mradi wa kujenga shule moja ya sekondari yenye mabweni kwenye kila mkoa kwa ajili ya kufundishia masomo ya sayansi kwa wasichana ili kuongeza fursa za elimu na kuongeza idadi ya wasichana wanaojihusisha na masuala ya kidijitali.

Zaidi, Rais Samia ameisihi jamii kuachana na imani potofu juu ya wanawake na ushiriki wao katika mambo ya maendeleo ikiwemo umiliki wa ardhi na mali kwani wanawake nao ni viumbe wenye nguvu kama alivyokuwa mwanadamu yeyote chini ya jua.