November 24, 2024

Rais Samia kuzungumza na vijana Tanzania

Mazungumo hayo yanatarajiwa kufanywa Juni 15 mwaka huu katika siku ya tatu ya ziara yake atakayoifanya Mwanza kuanzia Juni 13, 2021.

  • Mazungumo hayo yanatarajiwa kufanywa Juni 15 mwaka huu katika siku  ya tatu ya ziara yake atakayoifanya Mwanza kuanzia Juni 13, 2021.
  • Ni muendelezo wa Rais Samia kuzungumza na makundi mbalimbali nchini baada ya kuanza kuzungumza na wazee jijini Dar es Salaam. 

Mwanza. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufanya mazungumzo na vijana jijini Mwanza ili waweze kubaini fursa mbalimbali za kiuchumi ikiwa ni moja ya shughuli atakazozifanya akiwa akiwa katika ziara ya kwanza mkoani humo tangu aapishwe kushika wadhifa huo.

Mazungumo hayo yanatarajiwa kufanywa Juni 15 mwaka huu katika siku ya tatu ya ziara yake atakayoifanya Mwanza kuanzia Juni 13 mwaka huu.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Albert Chalamila amewaambia wanahabari leo Juni 7, 2021 kuwa vijana wote wanapaswa kuhudhuria mkutano huo ambao watajulishwa eneo maalum utakapofanyika mkutano huo.

Mazungumzo hayo itakuwa ni muendelezo wa Rais Samia kuzungumza na makundi mbalimbali nchini hasa baada ya kuanza kuzungumza na wazee jijini Dar es Salaam na Juni 8 anatarajiwa kuzungumza na wanawake jijini Dodoma. 

“Niwaombe vijana wote, wawe wanasiasa au wenye dini na wasio na dini, kujitokeza kwa wingi kwenye eneo litakalopangwa ili waweze  kumsikia akisema nini kuhusiana na  fursa za ajira, biashara, kilimo na mikopo zitakazowasaidia vijana hao kukua kiuchumi,” amesema Chalamila.

Sanjari na mkutano huo na vijana, Chalamila amesema katika ziara hiyo Rais atazindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa mkoani humo.

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na wafanyabiashara wa baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Picha|Habari Maelezo. 

Miongozi mwa shughuli hizo ni kuzindua mtambo wa kuchenjua dhahabu uliojengwa jijini Mwanza wenye thamani ya Sh10.4 bilioni.

“Pia atazindua jengo la Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Kanda ya Ziwa shughuli ambayo itafanyika siku ya Juni 13 ambayo ataanza ziara yake ,” amesema Chalamila.

Shughuli nyingine itakayofanyika kwenye ziara hiyo ni kuzindua mradi wa maji wilayani Misungwi wenye thamani ya Sh13.7 bilioni, kuweka jiwe la ujenzi wa reli ya kisasa ya Stardard Gauge kutoka Mwanza kwenda Isaka mkoani Shinyanga mradi ambao utajengwa kwa gharama ya Sh3.067 trilioni.

Katika mradi huu tayari zaidi ya Sh300 bilioni zimeshatolewa kwa awamu ya kwanza  na hii ni awamu ya tano ya ujenzi wa reli hiyo ambayo ya kwanza ilianzia jijini Dar es Salaam

Rais Samia pia atatembelea mradi wa ujenzi wa daraja la JPM lenye thamani ya zaidi ya Sh669 bilioni.

“Niwaombe wakazi wa Mwanza kujitokeza kwa wingi wakiwa na mabango yao ya kumpokea waeleze shida zao kwa kuwa katika ziara hiyo pia atazungumza na wananchi,” amesema Chalamila na kuongeza kuwa hiyo itakuwa ni ziara yake ya kwanza toka Rais aingine madarakani.