October 6, 2024

Tanzania yatakiwa kukaza mwendo mapambano dhidi ya seli mundu

Inakadiriwa kwa mwaka, watoto zaidi ya 10,000 huzaliwa na ugonjwa wa seli mundu.

  • Kwa sasa watoto 11,000 wanazaliwa na ugonjwa wa seli mundu.
  • Watanzania wanashauriwa kupima ili kujua kama wamebeba vinasaba.

Dar es Salaam. Zawadi ambayo wanandoa wengi hutarajia baada ya kuoana ni kupata watoto na kujenga familia yenye furaha amani na yenye afya. 

Hata hivyo, baada watoto kuzaliwa katika familia, baadhi yao huzaliwa wakiwa na magonjwa ya kurithi ikiwemo kisukari na seli mundu (sicklecell). 

Mkazi wa shinyanga, Monica Meshack amesema, kwa zamani, magonjwa ya kurithi yalikuwa yakizingatiwa kabla ya watu kuoana lakini kwa sasa, watu wanazingatia Ukimwi tu.

“Zamani kabla watu hawajaona, wazazi walikuwa wanapeleleza kujua historia ya ukoo anaotoka mwanaume au mwanamke kabla hawajakubali kuendelea na taratibu za ndoa. Ilisaidia kupunguza magonjwa ya kurithi ikiwemo seli mundu,” amesema Meshack.

Hata hivyo, kwa sasa ugonjwa wa seli mundu ni kati ya magonjwa yanayowatesa Watanzania wengi huku maelfu wakiwa wabebaji wa vinasaba ambao hawafahamu hali zao.

Mratibu wa moja ya mradi wa seli mundu Tanzania kutoka Programu ya Seli Mundu (Sicklecell Programme) ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS), Dk Agnes Jonathan amesema kwa Tanzania, watoto 11,000 wanazaliwa wakiwa na ugonjwa wa seli mundu kila mwaka.

Pia, inakadiriwa ifikapo mwaka 2050, wagonjwa wa seli mundu wataongezeka kwa asilimia 10 kutoka asilimia 75 ya sasa sawa na kusema inakadiriwa watoto 400,000 duniani watakuwa wanazaliwa na ugonjwa huo kila mwaka. 

Amesema Seli mundu ni ugonjwa wa kurithi toka kwa wazazi wa pande zote mbili yaani baba na mama unaosababisha umbo la seli nyekundu ya damu kutoka umbo la duara na kua umbo la mundu.

Mtaalamu huyo wa masuala ya afya amesema pale mtu ambaye amebeba vinasaba vya seli mundu anapopata mtoto na mtu ambaye pia amebeba vinasaba vya seli mundu, kuna uwezekano wa kupata mtoto ambaye ana seli mundu.

Dk Jonathan ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz), pale mtu anapogundulika na wataalamu wa afya kuwa na ugonjwa wa seli mundu, anashauriwa kula chakula stahiki pamoja na kuhudhuria kliniki kwa ajili ya matibabu.

Kwa jijini Dar es Salaam, kliniki hizo zipo katika hospitali za rufaa ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Temeke, Mwananyamala na Mloganzila.

Hospitali zingine ni pamoja na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo na Hospitali ya Bugando (Mwanza). 


Soma zaidi:


Dk Jonathan amesema kazi inafanyika ili kliniki hizo zifike sehemu nyingi zaidi ili kuongeza kasi ya matibabu kwa wagonjwa wanaogundulika.

“Mgonjwa wa seli mundu anashauriwa ahudhurie kliniki, ale mboga mboga za majani, anywe dawa zake za “folic acid” kila siku, na ale vyakula vyenye madini chuma kama dagaa. Pia kipindi cha baridi ajikinge na baridi.” amesema Dk Jonathan akitaja namba za huduma kwa wateja wa seli mundu ni 0769680688.

Pia, daktari huyo ameshauri wagonjwa wa seli mundu kuwa na bima ya afya ili kuwawezesha kupata matibabu kwa urahisi na pale wanapoanza kusikia maumivu, ni vyema wakawahi katika kituo cha afya kwa ajili ya matibabu na wasisubiri siku ya kliniki tu.

Dk Agnes amesema, kwa ambaye haonyeshi dalili za seli mundu, apime kujua hali yake kama amebeba viñasaba au laa.