November 24, 2024

Kwanini mwanaume ufuatilie mzunguko wa hedhi wa mwenza wako?

Mzunguko wa hedhi huambatana na mambo mengi kwa wanawake. Ukifahamu mzunguko wa mwenzi wako itakusaidia kuishi naye vizuri akiwa kwenye siku zake za hedhi.

  • Itawasaidia kupanga uzazi na kuepuka mimba zisizotarajiwa.
  • Ni sehemu ya mwaanaume kuonyesha mahaba kwa ampendae.
  • Itamsaidia mwanaume kumuelewa mpenzi wake zaidi.

Dar es Salaam. Kuna siku niliomba simu ya mshikaji wangu kuangalia kitu na nilikuta programu (app) ya kufuatilia hedhi. Nilishtuka lakini niliendelea na kilichonipeleka na sikutaka kujua kwanini jamaa ana app ya kufuatilia hedhi. 

Baada ya wiki kadhaa, jambo hilo lilinijia tena akilini na sikutaka kupitwa, nilimuuliza mshikaji kwanini ana app hiyo kwenye simu yake ilhari mwananume hapati hedhi?

“Wanaume wengi huwa ni wasahaulifu wa masuala madogo madogo mfano tarehe za maadhimisho ya miaka ya mahusiano, tarehe za hedhi na rangi ambazo wapenzi wetu wanapenda. Hii app ni kwa ajili ya mpenzi wangu,” aliniambia jamaa huku akisema ni sehemu ya mawasiliano kati yake na mpenzi wake.

Jamaa alisema huwa anajaza taarifa za mpenzi wake kila siku ikiwemo jinsi anavyojisikia na vyakula anavyokula.

Sitaki kusema kuwa majibu yake yaliniridhisha lakini yalinipatia sababu ya kutaka kufahamu kama kweli jamaa aliniambia ukweli au alinipiga changa la macho.

Na haya ndiyo majibu ambayo wanawake kwa wanaume waliniambia pale nilipowauliza umuhimu wa wanaume kufahamu mzunguko wa hedhi wa wapenzi wao.

Iashauriwa Mwanaume kuwa karibu na mpenzi wako pale anapokuwa katika siku zake za hedhi ili kumfariji, Picha| Mtandao.

Kuepukana na mimba zisizotarajiwa

Pale mwanaume anapokuwa anauelewa  mzunguko wa hedhi wa mpenzi wake, inakuwa ni rahisi kuzifahamu siku za hatari za mpenzi wake ambazo endapo akijamiiana naye anaweza kupata ujauzito.

Hilo litawaepusha kuwa katika hali ya sintofahamu ya mwanamke kupata ujauzito ambao haujapangwa.

Ni sehemu ya kuonyesha mahaba yako

Inaweza kudhaniwa ninawaza kwa sauti lakini siyo maneno yangu, ni maneno ya wadau ambaoo nimeongea nao.

Kwa wanawake, hakuna kitu kinagusa moyo wao kama wenzi wao kukumbuka vitu vidogo vidogo. Endapo unafatilia mzunguko wa hedhi wa mpenzi wako, ni sehemu ya wewe kuonyesha kuwa unampenda kwa kumzawadia vifaa muhimu vya kujisitiri wakati wa hedhi zikiwemo taulo za kike.

Hilo na mambo mengine litasaidia katika kudumisha mapenzi yenu.


Soma zaidi:


Itakusaidia kumwelewa mpenzi wako

Mzunguko wa hedhi huambatana na mambo mengi kwa wanawake. Wapo ambao huumwa sana, wengine huwa na hasira zisizoeleweka na wengine hupenda kula. 

Endapo  ukiwa unafahamu kinachoendelea kwa mwenzi wako, itakuwa rahisi kwako kumfariji pale anapokuwa kwenye maumivu, kumvumilia pale anapokuwa na hasira na kumnunulia chakula wala kutokumsema endapo atazidisha kiwango cha chakula chake cha kawaida.

“Wapo ambao wakifikia kipindi cha hedhi wanakuwa na kisirani kama wajawazito, wapo ambao huwa na tabia ya kununa bila sababu ya msingi. Hedhi huambatana na mengi na inatofautiana kati ya mtu na mtu,” amesema mmoja ya watu niliooongea nao.

Inashauriwa Mwanaume kuwa karibu na mpenzi wako pale anapokuwa katika siku zake za hedhi ili kumfariji, kumwambia unampenda na pia kuonyesha kuwa upendo wako unaenda mbali zaidi ya kipindi akiwa sawa tu.


TANGAZO