November 24, 2024

Watumiaji wa mafuta ya taa wapungua zaidi ya mara mbili Tanzania

Wamepungua kutoka lita milioni 1 kwa mwezi mwaka 2016/17 hadi lita laki 4.5 mwaka 2020/21.

  • Wamepungua kutoka lita milioni 1 kwa mwezi mwaka 2016/17 hadi lita 450,000 mwaka 2020/21.
  • Matumizi ya mafuta ya taa yamepungua kutokana na kuongezeka kwa upatikanaji wa umeme vijijini.

Dar es Salaam. Kasi ya matumizi ya nishati safi na salama imezidi kuongezeka Tanzania baada ya idadi ya watumiaji wa mafuta ya taa nchini kupungua kwa zaidi ya mara mbili katika kipindi cha miaka minne iliyopita. 

Mafuta ya taa yanayotumiwa zaidi kama nishati ya mwanga katika maeneo yasiyo na umeme hasa vijijini yanatajwa kama moja ya vyanzo vya uzalishaji wa hewa ukaa na kuathiri kiafya kwa binadamu ikiwemo matatizo ya macho na mfumo wa upumuaji. 

Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani ameliambia Bunge kuwa matumizi ya mafuta ya taa hususan vijijini yamepungua kutoka lita milioni 1 kwa mwezi mwaka 2016/17 hadi lita 450,000 mwaka 2020/21.

Hiyo ni sawa na kusema watumiaji wa nishati hiyo wamepungua mara 2.2 ndani ya kipindi cha miaka minne iliyopita. 

Dk Kalemani katika hotuba yake ya bajeti kwa mwaka 2021/22 aliyowasilisha leo Juni 2, 2021 bungeni jijini Dodoma amesema matumizi yamepungua kutokana na kuongezeka kwa upatikanaji wa umeme vijijini.

“Hadi kufikia mwezi Aprili, 2021 jumla ya vijiji 10,312 vimeunganishiwa na umeme ikilinganishwa na vijiji 2,018 vilivyokuwa vimeunganishwa umeme mwaka 2015 sawa na asilimia 86 ya vijiji vya Tanzania Bara vimepata umeme,” amesema Kalemani.

Miaka ya nyuma mafuta ya taa mbali na kutumika kwa mwanga, yalikuwa yakitumika kwa ajili ya kupikia. Picha| Mtandao.

Sababu nyingine iliyochangia kushuka kwa matumizi ya mafuta ni kuongezeka kwa matumizi ya gesi ya mitungi (Liquefied Petroleum Gas – LPG) nchini ambayo imekuwa ikitumia zaidi katika shughuli za kupikia nyumbani kwa watu wa mjini. 

Miaka ya nyuma mafuta ya taa mbali na kutumika kwa mwanga, yalikuwa yakitumika kwa ajili ya kupikia. 

Kwa mujibu wa Kalemani, matumizi ya gesi hiyo yameongezeka  kwa asilimia 61.6 kutoka tani 106,301 mwaka 2019 hadi kufikia tani 171,828 mwaka 2020. 

Gesi ya mitungi inatajwa na wadau wa mazingira kuwa ni rafiki wa mazingira na haina madhara kwa afya ya binadamu kwa sababu ni salama na safi ikilinganishwa na mafuta ya taa.


Zinazohusiana: 


Bajeti ya nishati yaongezeka

Katika Mwaka 2021/22, Wizara ya Nishati inakadiria kutumia Sh2.4 trilioni ikilinganishwa na Sh2.2 trilioni iliyotengwa kwa mwaka 2020/21 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 8.

“Hadi kufikia mwezi Mei, 2021, Wizara ilikuwa imepokea jumla ya Sh1.4 trilioni Kiasi hicho kilichopokelewa na Wizara ni sawa na asilimia 61.5 ya bajeti yote ya Wizara (2020/21),” amesema Dk Kalemani. 

Kati ya fedha hizo zilizotengwa, Sh2.35 trilioni sawa na asilimia 98.9 ya bajeti yote ya wizara zitaelekezwa kushughulikia miradi ya maendeleo. 

Kwa mwaka 2021/22, Wizara ya Nishati itaendelea kutekeleza vipaumbele mbalimbali vikiwemo kuongeza uzalishaji wa umeme nchini kufikia megawati 5,000 katika kipindi cha miaka mitano  ijayo kwa kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo miradi mikubwa ya kimkakati na ya kielelezo ya Julius Nyerere (megawati 2,115), Ruhudji (megawati 358) na Rumakali megawati 222.