September 29, 2024

Rais Samia awaonya viongozi kujiingiza katika migogoroya ardhi

Amesema wasimamie maslahi ya Watanzania na kutatua kero zao.

  • Amesema wamechaguliwa kwa kazi maalumu hivyo watimize majukumu yao.
  • Amesema kwa watakaojihusisha na migogoro ya ardhi, vyombo vinaona na vitafanya kazi.
  • Dk Mpango amewashauri kuishi viapo vyao vya maadili kwa kuwatumikia Watanzania.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaonya viongozi wa Serikali kutokujihusisha na migogoro ya ardhi kwa sababu wanaweza kuchukuliwa hatua kali badala yake wasimamie haki za wananchi katika maeneo yao ya kazi.

Rais Samia amesema katika mikoa mbalimbali nchini, migogoro ambayo imekuwa ikishika kasi ni ile ya mirathi pamoja na ardhi. 

“Sitavumilia kusikia RAS (Katibu Tawala wa Mkoa), mkuu wa mkoa naye kaenda kajiingiza kwenye mgogoro wa ardhi. Kaingia kwenye mkoa kakuta ardhi ya watu wenyewe wapo kajimilikisha anaitumia yeye anaacha watu wanalalamika hapana!”. 

“Umepelekwa kwa kazi maalumu usiende kujishirikisha kwenye migogoro ya ardhi,” amesema Rais Samia leo  Juni 2, 2021 jijini Dodoma wakati akiwaapisha makatibu tawala wa mikoa na wakuu wa taasisi aliowateua wiki iliyopita.

Amesema kwa ambao watajiingiza katika mambo hayo, vyombo vipo vitaona na watachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Kila niliyemteua ana mtu nyuma anamfuata, na humjui ni nani. Nendeni kafanye kazi mjue nina jicho linakuangalia huku, na sitanii kwenye hilo,” amesema Samia huku akiwataka viongozi kupendana na kushirikiana kuwatumikia wananchi. 


Soma zaidi:


Aidha, amewataka viongozi walioapishwa leo wakasimie vizuri matumizi  fedha za maendeleo ambazo zinatolewa na Serikali katika maeneo yao ili ziwafaidishe wananchi. 

Kwa upande wake Makamu wa Rais, Dk Phillip Mpango amesema viongozi hao wanatakiwa kushirikiana na viongozi pamoja na taasisi zingine katika kuhakikisha wananchi wana sehemu ya kusemea kero zao na wanazitatua na siYo hadi wananchi wakutane na viongozi wakubwa.

“Nawapongeza sana wote mlioteuliwa, dhamana hii mliyopewa ni kubwa, mmeaminiwa kuwatumikia wananchi wa Tanzania, msimuangushe Mheshimiwa Rais aliyewaamini na Watanzania mnaoenda kuwatumikia,” amesema Dk Mpango.