October 6, 2024

Simulizi ya mwanamke aliyenusurika kifo na kupoteza watoto watatu baharini

Ni Misrah na wahamiaji wengine 55 waliopata dhuruba ndani ya mashua iliyomilikiwa na wasafirishaji waliokuwa wakivuka Ghuba ya Aden kuingia nchini Yemen kutoka Pembe ya Afrika kupitia Djibouti, Aprili 14 mwaka huu.

  • Ni mwanake aliyefahamika kwa jina la Misrah, mhamiaji aliyekuwa akielekea nchini Yemen akitokea Djibouti.
  • Alipoteza watoto watatu baada ya mashua kuzidiwa nguvu na mawimbi ya bahari.

“Nimepoteza kila kitu,” anasema Misrah, mwanamke mhamiaji kutoka Ethiopia aliyenusurika kifo na kupoteza watoto watatu baharini baada ya mashua waliyopanda kupinduka. 

Kwa mujibu wa wa Shirika la Umoja wa mataifa la Uhamiaji (IOM), Misrah (27) pamoja na mumewe na watoto wake: Aziza (5), Rachar (3) na Ikram (2) na wahamiaji wengine 55 walipata dhuruba hiyo ndani ya mashua iliyomilikiwa na wasafirishaji waliokuwa wakivuka Ghuba ya Aden kuingia nchini Yemen kutoka Pembe ya Afrika kupitia Djibouti,  Aprili 14 mwaka huu. 

Kutokana na mashua hiyo kujaza watu wengi na kusafiri usiku ilizidiwa nguvu na mawimbi na kupinduka baharini.

IOM inaeleza kuwa watoto 16 wakiwemo wa Misrah na takriban wahamiaji wengine 44 na wakimbizi walizama wakiwa wamenaswa chini ya chombo hicho. 

Yeye na mumewe Abdul Basit walikuwa ni miongoni mwa watu 14 tu walionusurika katika ajali hiyo. 

Katika mahojiano yake na Radio ya Umoja wa Mataifa (UN),  Misrah anasema anajipa nguvu na ujasiri kuelezea kisa hicho ambacho kimemuacha na majonzi mengi.

“Watoto wangu walikuwa wamelala wakati mashua ilipinduka. Nilikuwa nimemshika Ikram mikononi mwangu. Nilijua ninaweza kuogelea. Ndivyo nilivyonusurika. Kwa bahati mbaya, watoto hawakunusurika. Walikuwa wadogo sana; mawimbi ya bahari yaliwazidi nguvu,” anasema  mwanamke huyo.

Misrah aliogelea hadi ufukweni na kwa msaada wa mwendesha gari aliyekuwa anapita kwenda mji wa Obock, Djibouti, aliweza kufika na kukutana na wafanyakazi kutoka kituo cha kukabiliana na masuala ya uhamiaji cha IOM. 

“Nilipewa simu kumpigia mama yangu na ninajisikia vizuri kwa sasa. Baadaye pia walinisaidia kumpata mume wangu, ambaye alirudi Ethiopia, ” Misrah anasema katika mahojiano hayo. 

“Wafanyakazi wananijali, wakijaribu kunihakikishia usalama wangu na ningependa kumuona mama yangu kwani ndiye pekee anayeweza kunifariji sasa hivi,” anaeleza kwa uchungu. 

Misrah, mwanamke aliyepoteza watoto wake watatu waliofariki baharini wakati boti waliyokuwa wakisafiria kuzama kwenye Ghuba ya Aden. Picha| IOM 2021/Hawa Diallo.

Safari yake ya uhamaji

Mwaka 2012, Misrah aliondoka nyumbani kwake huko Derdawah, Ethiopia kwenda kutafuta kazi za ndani nchini Djibouti na baadaye alipata fedha ili aelekee Yemen.

“Nilitaka kutunza familia yangu, mama yangu na ndugu zangu,” anaelezea. “Nilifanikiwa kusafiri kwenda Djibouti ambako nilifanya kazi ya kijakazi. Pesa niliyopata kupitia hiyo kazi ilikuwa ndiyo nauli ya kusafiri kwenda Yemen kwa mashua. ” 

Maelfu ya wahamiaji kutoka Ethiopia hupitia Djibouti kwenda Yemen kila mwaka wakitarajia kufika Ufalme wa Saudi Arabia, ambapo kuna fursa nzuri zaidi za kazi na kipato cha juu kuliko nyumbani. 

Wengine kama Misrah wanakusudia kubaki Yemen ambapo, kabla ya mzozo na janga la Corona, kulikuwa na fursa kwa wafanyakazi wahamiaji.  

Polepole, Misrah alijenga maisha mapya katika jiji la Aden, kwa kazi ya usafishaji. Mwaka 2014 aliolewa na Abdul Basit, na wakaanzisha familia yao, anaeleza mwanamke huyo katika mahojiano na redio ya Umoja wa Mataifa. 


Soma zaidi: 


“Nilipenda maisha yangu nchini Yemen,” Misrah anasema. 

Misrah na mumuwe hawakuwa na hati rasmi za kukaa nchini Yemen au karatasi zilizohitajika kurudi nchini Ethiopia, na walilazimika kuwalipa wasafirishaji haramu dola 400 (Sh927,597) ili wasafiri kutoka Yemen kwenda Djibouti kwa mashua, awamu ya kwanza ya safari kwenda Ethiopia na hapo ndipo wakapata ajali ya baharini.

Katika mwaka uliopita, zaidi ya safari 11,000 kama hizo zilifanywa kutumia vyombo vya bahari visivyofaa na wahamiaji kutoka Pembe ya Afrika wakiwa na hamu ya kurudi nyumbani kutoka Yemen.  

Wengine, kama Misrah, wanarudi kwa dharura za kifamilia, wakati wengine walikuwa wamejaribu na wakashindwa kufika Ufalme wa Saudi Arabia.  

IOM inakadiria kuwa zaidi ya wahamiaji 32,000 wamekwama nchini Yemen kutokana na kuimarishwa na vizuizi vya COVID-19 ambavyo vinawazuia kwenda Saud Arabia.

Wahamiaji ambao walinusurika kwenye boti ya wasafirishaji haramu kwenye ghuba ya Aden walifikishwa ufukweni Obock Djibout pichani. Picha| IOM/Olivia Headon.

Apata msaada wa kisaikolojia 

Wafanyikazi wa IOM nchini Djibouti wanampa Misrah ushauri kutokana na mshtuko alioupata lakini pia atapata fursa ya kufanya kazi na IOM nchini Ethiopia ili kumsaidia kurudi nyumbani aweze kuungana tena na familia yake. 

 “Ninataka wahamiaji nchini Yemen waelewe kwamba safari hiyo ni hatari sana. Niko hai, lakini nahisi kama nimekufa,” anasema Misrah katika mahojiano hayo. 

Licha ya simulizi ya Misrah na hatari za kutishia maisha za safari za baharini, idadi ya wahamiaji wanaofika Djibouti kwa mashua inaendelea kuongezeka. 

IOM inaeleza kuwa mnamo mwezi Machi, zaidi ya wahamiaji 2,343 waliwasili kutoka Yemen kwa mashua, ikilinganishwa na 1,900 kwa mwezi wa Februari. 

IOM inafanya kazi na serikali na washirika wengine kukidhi mahitaji ya wahamiaji hao, kupunguza uhamiaji usio wa kawaida, na kuwalinda wahamiaji dhidi ya unyonyaji unaofanywa na wasafirishaji haramu na wauzaji wa binadamu.