September 29, 2024

Mabadiliko tabianchi yalivyoshusha uzalishaji wa mazao ya biashara Tanzania

Zaidi ya nusu ya uzalishaji wa mazao hayo kushuka kwa viwango tofauti kutokana na mabadiliko ya tabia nchi yaliyotokea kipindi hicho ikiwemo mvua nyingi.

  • Hali hiyo imechangiwa na kubadilika kwa unyeshaji wa mvua na wadudu wasumbufu.
  • Mabadiliko hayo yamechangia uzalishaji wa mazao matano ya biashara kushuka.
  • Serikali yasema imechukua hatua ikiwemo kuzalisha mbegu ili kuongeza uzalishaji.

Dar es Salaam. Unaweza kusema mwaka 2020/21 ulikuwa wa maumivu kwa wazalishaji wa mazao ya asili ya biashara Tanzania baada ya zaidi ya nusu ya uzalishaji wa mazao hayo kushuka kwa viwango tofauti kutokana na mabadiliko ya tabia nchi yaliyotokea kipindi hicho ikiwemo mvua nyingi.

Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, mazao asilia ya biashara yanayozalishwa Tanzania ni tumbaku, pamba, kahawa, chai, pareto, korosho, mkonge na miwa.

Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda katika hotuba ya wizara yake ya bajeti kwa mwaka 2021/22 amesema mazao matano sawa na asilimia 62.5 kati ya mazao hayo nane, uzalishaji wake ulishuka mwaka 2020/21. 

Mazao hayo ambayo uzalishaji wake umeshuka kwa viwango tofauti ni pamba, chai, pareto, korosho na mkonge. Tanzania huyachakata na kuyauza mazao hayo katika masoko mbalimbali duniani.

Kushuka kwa uzalishaji wa mazao hayo kumetokana na sababu moja kubwa ambayo ni mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yalishuhudiwa mwaka 2020/21 wakati wakulima wakiwekeza katika kilimo cha mazao hayo. 

Mkenda katika hotuba yake anasema katika msimu wa ununuzi wa 2020/21 tani 122,833 za pamba zilizalishwa na kuuzwa ikilinganishwa na tani 348,958 katika msimu wa ununuzi wa 2019/2020.

Upungufu huo, Prof Mkenda anasema umetokana na mvua nyingi pamoja na kushuka kwa bei katika soko la dunia kwa msimu wa ununuzi wa 2019/20 ambapo baadhi ya wakulima waliacha kulima pamba. 

Pamba ni zao muhimu ambalo kutumika kutengeneza bidhaa mbalimbali zikiwemo nyuzi na vitambaa ambavyo hutumika kutengenezea nguo na kufungia vituo mbalimbali.

Katika mwaka 2020/21 uzalishaji wa chai kavu umefikia tani 10,940 ukiwa umeshuka kidogo kutoka tani 11,185.8 za kipindi kama hicho mwaka 2019/20.

“Uzalishaji huo umeshuka kutokana na mabadiliko ya tabianchi na baadhi ya wawekezaji kusitisha uzalishaji kutokana na mlipuko wa homa kali ya mapafu (Covid-19),” anasema waziri huyo.

Mabadiliko hayo ya hali ya hewa hayakuliacha salama zao la korosho ambapo uzalishaji wake umeshuka hadi tani 206,718 kutoka tani 232,631 mwaka 2019/20. 

Kushuka kwa uzalishaji huo kumetokana na mabadiliko ya hali ya hewa yaliyosababisha kuzuka kwa magonjwa na visumbufu vya mimea na matumizi madogo ya pembejeo.

Mazao matatu yaliyobaki ya kahawa, miwa na tumbaku, uzalishaji wake umeongezeka katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kutokana na kuendana na mabadiliko ya hali ya hewa yaliyokuwepo na uhitaji wa mazao hayo katika soko la dunia. 

Mazao ya biashara yamekuwa yakitegemewa na wakulima na Serikali kwa ajili ya kuingiza fedha za kigeni ili kuongeza pato la Taifa.

Mabadiliko hayo ya tabianchi kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Kituo cha Kitaifa cha Kufuatilia Hewa Ukaa (NCMC) Profesa Eliakimu Zahabu yanatokana na uzalishaji wa gesi joto ambazo zinatokana na shughuli za kibinadamu ikiwemo ukataji wa miti, viwanda.


Zinazohusiana:


Amesema shughuli hizo huchangia kuzalisha hewa ukaa ambayo husababisha kuongezeka kwa joto la dunia na kusababisha kubadilika kwa vipindi vya mvua, jambo linathiri shughuli za kilimo. 

“Kasi ya uzalishaji wa hewa ukaa ni kubwa sana na ina athari nyingi isipodhibitiwa ikiwemo kilimo ambacho kinategemewa na watu wengi,” amesema Prof Zahabu.

Kushuka kwa uzalishaji wa mazao ya biashara kunasababisha kushuka kwa faida au mapato ambayo wakulima na Taifa wangepata katika mwaka wa 2020/21 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.


Nini kifanyike?

Kutokana na changamoto mbalimbali za uzalishaji zilizojitokeza mwaka 2020/21, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuongeza uzalishaji wa mazao yote ya biashara ikiwemo kuanzisha kilimo cha umwagiliaji ili kukabiliana na upungufu wa mvua.

“Bodi ya Chai imefufua shamba la Chama cha Ushirika cha MUVYULU lenye hekta 215 na shamba la Mlangali linalomilikiwa na Kampuni ya Dhow Mercantile (EA) Ltd lenye hekta 200 limeanza kutumia kilimo cha umwagiliaji,” amesema Prof Mkenda kuhusu kuinua zao la chai.

Sambamba na hilo ni upatinakanaji na uzalishaji wa pembejeo zikiwa mbegu bora zinazoweza kustahimili mabadiliko ya tabianchi ili zisambazwe kwa wananchi.

“Kufuatia hali hiyo, Bodi ya Korosho inasimamia mpango wa ununuzi wa pembejeo kwa pamoja kupitia Vyama vikuu vya Ushirika ili wakulima waweze kupata pembejeo kwa wakati na kwa bei nafuu,” amesema waziri huyo.