September 29, 2024

Fedha za maendeleo zamuweka pabaya kigogo Mwanza

Ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Bugando ambaye amesusiwa mkutano na wananchi wake wakitaka waelezwe Sh1.2 milioni walizochanga kwa ajili ya maendeleo ziko wapi.

  • Ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Bugando ambaye amesusiwa mkutano na wananchi wake.
  • Wananchi wa mtaa huo walisusa wakitaka waelezwe Sh1.2 milioni walizochanga ziko wapi.
  • Fedha hizo ni kwa ajili ya ujenzi wa barabara na ofisi ya mtaa. 

Mwanza. Wananchi wa Mtaa wa Bugando, Kata ya Igogo jijini Mwanza wamesusia  mkutano ulioitishwa na uongozi wa mtaa huo kujadili mandeleo ya mtaa huo ikiwemo ujenzi wa barabara kutokana na kukosekana kwa uwazi wa mapato na matumizi ya katika ofisi ya mtaa huo. 

Tukio hilo limetokea mwishoni mwa juma baada ya uongozi wa mtaa kushindwa kutoa maelezo ya kina kuhusiana na fedha zilizochangwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya mtaa huo yenye urefu wa mita 300.

Takribani mwaka mmoja uliopita, wakazi hao walichangishwa Sh16,000 kila mmoja kwa ajili ya kutengeneza barabara za mawe za mtaa na ujenzi wa ofisi ya Serikali ya Mtaa.

Kamati ya maendeleo ya mtaa huo ilifanikiwa kukusanya Sh1.2 milioni lakini tangu wakati huo matumizi ya fedha hizo hayajulikani, jambo lililowafanya kususia mkutano ulioitishwa na viongozi wao mpaka pale watakapojulishwa kuhusu fedha hizo.

Wakizungumza baada ya mkutano huo kutawanyika wananchi hao wamemtuhumu mwenyekiti wa mtaa huo kushindwa kusaini nyaraka kwa ajili ya kwenda kuchukua fedha benki ili zitekeleze kazi iliyokuwa imepangwa.

Jamhuri Mgaigwa ni mkazi wa eneo hilo amesema makubaliano ilikuwa ni kutengeneza barabara hiyo na baada ya fedha hizo kutolewa viongozi wameshindwa kusaini nyaraka ili kwenda kuchukuliwa fedha hizo  zifanye kazi.

“Wanamtaa wa Bugando wanataka fedha zao zitoke ili waendelee kufanya maendeleo tofauti na hapo hawatachanga na hawatafanya maendeleo,” amesema Mgaigwa.

Wakazi wa Mtaa wa Buagando wakiwa kwenye mkutano kwa ajili ya kuzungumzia miradi ya mandeleo ya mtaa huo Mei 29, 2021. Picha| Mariam John.

Naye Matiku Mwiteki amesema “tulichanga fedha zetu kwa ajili ya kutengeneza barabara na tukaamini ziko sehemu salama ili zitakapohitajika zikafanye ile kazi na sasa zinahitajika viongozi hawataki kuzitoa.”

Wakazi wa mtaa huo wanataka kufahamu kujua sababu zinazochangia fedha hizo kushindwa kutoka wakati zilichangwa kwa ajili ya maendeleo yao.

Mkazi mwingine wa mtaa huo Magarame Mshana anamtaka mwenyekiti huyo kutoa fedha hizo ili kuondoa sintofahamu iliyopo na itaaidia wananchi kuendelea na moyo wa kuchangia maendeleo.

“Tunapata shida, wagonjwa wakiumwa hulazimika kuwabeba kwakuwa gari haiwezi kufika huku, wajawazito wengine hujifungulia njiani, tunaomba viongozi watuonee huruma ili fedha zitoke ziweze kufanya kazi,” anasema Mshana.


Soma zaidi: 


Mwenyekiti atoa majibu

Mwenyekiti wa mtaa huo, Juma Masanja amewatoa hofu wakazi hao kuwa fedha zao zipo salama isipokuwa nyaraka chache zilikosewa kuandikwa ili kukamilisha zoezi la kuchukua fedha benki kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo.

Anasema ili fedha zichukuliwe kunahitajika kamati mbili za huduma za jamii na ile ya fedha kukaa na kukubaliana fedha hizo zitoke kisha mwenyekiti atasaini nyaraka hizo ili fedha zikachukuliwe benki.

“Mimi napokea kama kiongozi na kiongozi ukiona kila mtu anakwambia kuwa ni kiongozi mzuri basi ujue haufai kuwa kiongozi kwa maana kiongozi lazima upakwe matope,” amesema mwenyekiti huyo wakati akijibu hoja za wananchi.

Mwenyekiti anasema hakuna fedha iliyotumika kinyume na taratibu zilizopangwa na kwamba endapo wananchi wana wasiwasi waombe chombo chochote kilichojuu yake kinachojishughulisha na uchunguzi wa rushwa kifanye kazi yake na yeye  yupo tayari kuchunguzwa.

Akitola ufafanuzi wa fedha hizo, Mwenyekiti wa kamati ya fedha ya mtaa huo, Hassan Haji amesema jumla ya fedha ambayo inalalamikiwa na wananchi iliyopo benki ni Sh1.14 milioni.

Kinachopigiwa kelele leo ni kutokana na watu waliosaini nyaraka hizo kutohusika kwenye kamati ya maendeleo, na kwamba kinachofanyika kwa sasa tutakaa na viongozi wanaohusika akiwemo mtendaji wa mtaa ili siku ya jumatatu (Mei 31, 2021) fedha hizo zikatolewe ili ziweze kufanya maendeleo,” amesema Haji.