October 6, 2024

Saratani inavyowatesa wakazi wa Kanda ya Ziwa-2

Shughuli za kiuchumi kama ukaushaji wa samaki kwa moshi na uchimbaji holela wa madini zatajwa kuwa chanzo cha saratani kanda ya ziwa.

  • Saratani husababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo shughuli za uchimbaji madini.
  • Elimu ndogo na kutopatikana huduma za matibabu ya saratani kirahisi  kunasababisha wagonjwa wengi kukosa tiba wakiwa katika hatua ya kwanza. 
  • Serikali yasema inaimarisha huduma za matibabu ili kupunguza visa vya saratani nchini. 

Mwanza. Katika sehemu ya kwanza ya ripoti hii tuliangazia baadhi ya athari za kiafya zinazotokana na saratani walizopata watu wa mikoa ya Kanda ya Ziwa. Leo tunaendelea na sehemu ya pili kulitazama suala hilo kwa undani.

Chanzo cha saratani kanda ya ziwa

Mikoa ya Kanda ya Ziwa ukiwemo Mwanza anakoishi Kija ni miongoni mwa maeneo ya Tanzania ambayo watu wake wanakabiliwa na changamoto kubwa ya saratani ambapo husababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo shughuli za uchimbaji madini. 

Wataalamu wa afya wanasema uchimbaji holela wa madini na matumizi ya kemikali hatarishi  hasa zebaki (Mercury) inayotiririshwa kwenye vyanzo vya maji na mito inayomwaga maji yake kwenye Ziwa Victoria imekuwa akiathiri watu mbalimbali katika maeneo hayo.

Ukaushaji wa samaki kwa njia ya moshi pia unatajwa kuwa ni sababu ya ugonjwa huo ambapo inadaiwa wavuvi hutumia  mabaki ya nguo pamoja na matumizi ya taka za plasitiki  ambazo ni hatari kwa  afya ya binadamu.

Pia matumizi ya samaki waliovuliwa kwa sumu nayo huchangia kwa sehemu kubwa watu kupata saratani mwilini. 

“Shughuli hizi kwa ujumla wake zinasababisha kemikali ambazo ni  hatari kwa binadamu, wavuvi wanaovua samaki kwa kutumia sumu,” amesema Dk Ngombariga.

Shughuli za uchimbaji madini zinawafanya wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa kupata saratani kutokana na kemikali za zebaki ambazo zinatumika katika shughuli hizo. Picha| Mtandao. 

Kwa nini wagonjwa hugungulika hatua za mwisho? 

Elimu ndogo miongoni mwa Watanzania na kutopatikana huduma za matibabu ya saratani kirahisi  kunasababisha wagonjwa wengi kukosa tiba wakiwa katika hatua ya kwanza. 

Baadhi ya wakazi wa Mwanza wameiambia www.nukta.co.tz kuwa wengi hawafahamu dalili za awali za ugonjwa huo na wanahitaji elimu ili kuisaidia jamii kupunguza janga hilo ambalo linaweza kuleta athari kwa vizazi hadi vizazi.

Yohana Maliyatabu, mkazi wa Igogo jijini Mwanza, anaomba kutolewa kwa elimu kwenye jamii kujua viashiria vya ugonjwa huo ili kuweza kupata matibabu mapema.

Anasema pia wananchi wengi hawafahamu kama matumizi ya samaki waliokaushwa kwa moshi  kuwa ni chanzo cha ugonjwa huo  kwa kuwa hawaelewi  mazingira wanavyoandaliwa hadi kufika sokoni.

“Wengi tunaamini samaki hao hukaushwa kwa kutumia kuni na si matambara, kunahitajika elimu kwa wanaokausha pia,”anasema Yohana.

Mecktirida Boniphace, mkazi wa Kisesa,  anasema hafahamu chanzo cha ugonjwa wa saratani na kwamba wizara ya afya inaowajibu wa kuwatumia wataalam wake kuwaelimisha wananchi. 

“Nasikia ni ugonjwa hatari na gharama yake ya matibabu ni kubwa hali inayosababisha watu wenye kipato cha chini kushindwa kugharamia na hivyo kusababisha kifo,” anasema.

Dk Dk Ngombariga anasema kutokana na changamoto hiyo wagonjwa wengi hufika wakiwa wamechelewa hivyo kuwapatia matibabu inakuwa ni changamoto. 

Asilimia 30 ya watu wazima au watatu kati ya 10 wanaofika hospitalini hapo hupona ugonjwa huo huku watoto wamefikia asilimia 50.

Moja ya makundi ambayo yapo hatarini kupata ugonjwa huo ni pamoja na wanaoishi na virusi vya ukimwi. 

“Upungufu wa kinga ya mwili inaweza kuwa chanzo cha kupata ugonjwa wa saratani kuliko wale ambao kinga yao iko imara zaidi,” anasema.  


Soma zaidi:



Mikoa inayoongoza

Bila kutaja idadi kamili, Dakatari huyo ambaye ni Mkuu wa Idara ya saratani hospitalini hapo amebainisha kuwa mikoa yote ya kanda ya ziwa inaoongoza kwa kuwa na wagonjwa.

Anasema ongezeko la wagonjwa hawa iligundulika baada ya wagonjwa wengi kuripotiwa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kutokana na takwimu.

Anasema tunaweza kuzishinda saratani hizi endapo tutabaini dalili hizi mapema na kuzitibu na hiyo itapunguza gharama za matibabu kwa kuwa gharama ni kubwa.

Anasema zaidi ya Sh400 milioni kwa mwezi hutumika kwa ajili ya kununulia dawa za kutibu ugonjwa huo katika hospitali hiyo ya rufaa ya Bugando.

Daktari mbobezi wa ugonjwa wa saratani kutoka hospitali ya rufaa ya Bugando, Dk Bernad  Ngombagira akikagua mafaili wakati akizungumza na Nukta habari kuhusiana na ugonjwa huo. Picha| Mariam John.

Mikakati ya Serikali kukabiliana na saratani

Kutokana na ongezeko la wagonjwa wa saratani kila mwaka, Serikali inachukua hatua mbalimbali kukabiliana na ugonjwa huo ikiwemo kuimarisha huduma za afya na vipimo. 

Katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka 2020/21, Serikali inasema kwa kushirikiana na wadau na mashirika yasiyo ya kiserikali imeendelea kuhakikisha inapambana na magonjwa ya saratani, ambapo katika kukabiliana na hilo imefunga mashine mbili za kisasa za tiba ya saratani kwa njia ya mionzi aina ya LINAC katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ambazo zimeanza kutoa huduma tangu Septemba, 2018. 

Waziri wa wizara hiyo Dk Dorothy Gwajima hivi karibuni alisema Serikali imeanzisha vituo takribani 624 ambavyo huweza kugundua na kutibu mapema saratani ya mlango wa kizazi.

Aidha, Dk Gwajima alisema magonjwa ya saratani yanatibika iwapo tu mgonjwa atawahi kupata tiba katika vituo vya afya vinavyotoa huduma hiyo. 

“Nitoe rai kwa wananchi, tujenge tabia ya kupima afya zetu mara kwa mara ili ikibainika kuwa tuna changamoto za kiafya basi tuanze matibabu bila kuchelewa,” alisisitiza Dk Gwajima.