October 6, 2024

Mbinu zitakazowasaidia wafanyabiashara kukuza biashara mtandaoni

Ni pamoja na kuchagua mtandao sahihi kwa ajili ya biashara yako na kuuza bidhaa zenye ubora na kuimarisha kitengo cha huduma kwa mteja.

  • Ni pamoja na kuchagua mtandao sahihi kwa ajili ya biashara yako.
  • Kutoa bidhaa zenye ubora na kuimarisha kitengo cha huduma kwa mteja. 
  • Kujifunza tabia za wateja wa bidhaa za mtandaoni na mabadiliko yao. 

Kilimanjaro. Licha ya wafanyabiashara hasa vijana kuhamishia biashara zao mtandaoni ili kupata wateja wengi, imebainika bado baadhi yao hawaitumii kama inavyotakiwa, jambo linalowakosesha faida ambazo wanatakiwa wazipate ili kukuza biashara zao.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), watumiaji wa intaneti Tanzania wamefikia milioni 29.1 mwezi Machi mwaka huu.

Ongezeko hilo linachochea biashara kufanyika kwenye mitandao ya kijamii na majukwaa mbalimbali  ili kukidhi mahitaji ya hilo linalokua kila siku.

Hata hivyo, yapo baadhi ya mambo yanatakiwa kuwekwa sawa baina ya wanunuzi na wauzaji wa bidhaa ikiwemo suala la matangazo ili kuepuka changamoto zinazokwamisha biashara hiyo isikue kwa kasi Tanzania. 

Kuzipatia suluhu changamoto hizo, wadau wa ubunifu na wajasiriamali wamekutana pamoja mkoani Kilimanjaro kwenye mjadala wa jamii ya wabunifu ya Startup Grind Kilimanjaro uliofanyika Mei 21, 2021. 

Mwanzilishi Mwenza wa jamii ya Startup Grind Kilimanjaro, Dorcas Mgogwe amesema kuna makosa ambayo wafanyabiashara wanayafanya wakiwa wanatangaza kazi zao mtandaoni ikiwemo kutokufahamu tabia za wateja wao na kushindwa kuwahudumia vizuri. 

“Wengine siyo kwamba wanafanya makosa kwa kupenda, wengine hawafahamu kabisa wanalolifanya kama lina manufaa kwa wateja wake na ndiyo maana majukwaa kama haya yanaandaliwa kwa ajili ya kuelimishana,” amesema Mgogwe.

Kutoka Kulia, Afisa Mradi na Mkuu wa masuala ya utawala kutoka White Orange Youth (WOY) NoelaRebecca Mnyawa, Mkurugenzi wa Programu kutoka Asante Africa, Grolia Mushi na mwanasheria anayejishughulisha na haki za binandamu Florence Akara wakizungumza katika mjadala wa jamii ya wabunifu wa Startup Grind Kilimanjaro uliofanyika Mei 21, 2021. Picha| Rodgers George.

Hizi ni baadhi ya suluhu zilizopendekezwa katika mjadala huo ambao ulilenga kuongeza ubunifu miongoni mwa vijana hasa wanawake:

Kuzingatia ukweli katika biashara 

Kwa mitandao ikiwemo Instagram, Facebook na WhatsApp wafanyabiashara kadhaa wamekuwa wakiweka picha ambazo haziendani na uhalisia wa bidhaa wanazoziuza.

Afisa Mradi na Mkuu wa utawala kutoka shirika linalojishughulisha na afya za watoto la White Orange Youth (WOY), Noela Mnyawa amesema wapo wafanyabiashara ambao picha zao na bidhaa wanazokuletea ni vitu viwili tofauti.

“Unaona picha bidhaa ni inavutiwa ukiletewa ni tofauti na ulichokiona,” amesema Mnyawa na kuwataka wafanyabiashara kuuza tabia hiyo ya udanganyifu kwa sababu inachangia kuua biashara. 


Kufahamu muda wa kuweka matangazo

Licha ya kuwa unahitaji kuweka picha mpya za bidhaa au huduma kwenye mitandao ya kijamii au majukwaa ya biashara mtandaoni, unashauriwa kufahamu muda ambao unafaa kuweka picha au video hizo ili maudhui yako yawafikie watu wengi na kuleta matokeo yaliyokusudiwa. 

Mdau wa biashara kutoka kampuni ya Uhuru Gardens, Tumaini Maletho amesema inabidi mtu asome biashara na wateja wake wanapendelea kutembelea mitandao ya kijamii muda gani. 

Maletho amesema endapo biashara yako ni ya wafanyakazi, hauwezi kuweka picha muda wa kazini ukataka waione. Weka picha asubuhi watu wakiwa kwenye vyombo vya usafiri, mchana wakati wa chakula cha machana na usiku watu wakiwa majumbani.

“Kuna haja gani ya kupost kitu sa nne wakati kazi watu ndiyo zimepamba moto? Jua muda ambao wateja wako wapo online (mtandaoni),” amesema Maletho.


Zinazohusiana: 


Uharaka wa kujibu meseji za wateja

Katika mitandao yote, kuna sehemu ambayo mteja anaweza kutuma ujumbe kwa muuzaji kuulizia bidhaa kama ipo. Kwa baadhi ya wafanyabiashara aidha kwa kujua au kutokujua, wamekuwa wakishindwa kutoa majibu kwa wateja hao ndani ya muda ambao bidhaa inakuwa inahitajika.

“Unaweza ukawa unahitaji shati kwa ajili ya harusi leo, ukaingia Instagram kutafuta na ukapata. Ikija kwenye kumpata muuzaji sasa ndiyo changamoto. Utatuma ujumbe haupatikani, namba ya simu unaambiwa haipo au haipatikani,” amesema mmoja wa wachangiaji katika mjadala huo.

Baadhi ya washiriki wa mjadala wa jamii ya wabunifu ya Startup Grind Kilimanjaro uliofanyika Mei 21, 2021 mjini Moshi. Picha| Rodgers George.

Ubora wa maudhui unayoweka mtandaoni

Katika biashara ambayo mtu anauza bidhaa na hata huduma, ni muhimu kuwekeza katika kutumia vifaa bora vya uzalishaji maudhui ikiwemo kamera za kisasa ili maudhui yatakayoleta matokeo chanya kwa wateja.

Mwalimu wa vijana kutoka taasisi ya wasicha ya GLAMI, Lightness Godwin amesema picha ambazo mfanyabiashara anapiga na kuweka mtandaoni ndiyo  zinazotoa mshawasha wa mtu kununua bidhaa zake au laa.

“Mpige picha nzuri jamani siyo ilimradi picha iliyokuwa na kitu unauza. Tafuta mazingira mazuri upige picha yako,” amesema Godwin.

Mbali na hapo, wajasiriamali wameshauriwa kuwa wawazi na bei za bidhaa zao kwani wateja hukasirika pale wanapoulizia bei na wanajibiwa “njoo DM” 

Pia wafanyabiashara wametakiwa kuchagua mitandao ya kijamii michache wanayoweza kuitumia kutangaza na kuuza bidhaa zao. 

“Kila aina ya mtandao wa kijamii una akaunti zake. Biashara rasmi za kiofisi zinaweza kuwa katika mitandao ya Linkedin na Twitter na biashara za bidhaa zinaweza kuwa Instgram, Facebook na hata WhatsApp,” amesema mmoja wa wachangiaji katika mjadala huo.