September 29, 2024

Rais Samia afanya mabadiliko wakuu wa mikoa aliowateua

John Mongela aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, amepelekwa mkoani Arusha huku David Kafulila ambaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha amepelekwa mkoani Simiyu.

  • Amefanya mabadiliko kwa wakuu wa mikoa ya Arusha na Simiyu.
  • Amesema ni kutokana na uzoefu wa nafasi hizo miongoni mwa walioliokuwa wameteuliwa.
  • Amewasisitiza aliowaapisha leo kufuata uadilifu na maadili ya kazi zao.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko ya uteuzi wa wakuu wa mikoa wawili aliowateuwa wiki iliyopita kwa kuwahamisha vituo vya kazi kabla hawajaanza majukumu yao.

John Mongela aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, amepelekwa mkoani Arusha huku David Kafulila ambaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha amepelekwa mkoani Simiyu.

Mabadilikoo hayo yanakuja baada ya uteuzi uliofanywa na Rais Samia Mei 15 mwaka huu ambapo alifanya mabadiliko makubwa ya wakuu wa mikoa 26 wa Tanzania Bara huku baadhi wakibadilishiwa vituo, wakiondolewa na kuingiza wapya. 

Rais Samia amefanya mabadiliko hayo leo (Mei19, 2021) Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akiwaapisha wakuu wa mikoa na wakuu wa taasisi akiwemo Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mkuu wa Mashtaka (DPP).

Mabadiliko hayo yamefanyika kutokana na  kutofautiana kwa uzoefu wa viongozi hao katika nafasi za uongozi hasa ngazi ya mikoa. 

“Nimeamua Mongella utakwenda Arusha kwa sababu ulikua unaongeza mkoa mkubwa na ambao unaendelea kuwa jiji na Arusha ni jiji. Na Kafulila kwa sababu ndiyo anaanza alikuwa RAS (Katibu Tawala wa Mkoa) ndiyo anaanza kuwa mkuu wa mkoa, wewe utakwenda Simiyu,” amesema Mama Samia.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akimuapisha Amos Gabriel Makalla kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam katika hafla iliyofanyika leo tarehe 19 Mei, 2021 Ikulu Jijini Dar es Salaam. Picha| Ikulu.

Rais Samia amewaapisha wakuu wa mikoa 10 wapya akiwemo Amos Makalla  ambaye ataongoza Mkoa wa Dar es Salaam, Omary Mgumba (Songwe), Steven Kagaigai (Kilimanjaro), Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge (Ruvuma), Charles Nyerere (Manyara) na Meja Jenerali Charles Mbuge (Kagera).

Wengine ni David Kafulila kwenda Simiyu, Rosemary Nyamule (Geita) Mwamvua Mrindoko (Katavi) na Queen Sendiga anaenda kuongoza Mkoa wa Iringa.

Wakuu wa mikoa wengine 16 waliobaki wamebadilishiwa vituo na tayari waliaapishwa.

Rais Samia amewaasa viongozi hao kuzingatia wajibu wao katika maeneo ya kazi pamoja na maadili ya nyadhifa walizo nazo.


Kibarua walichonacho wakuu wa mikoa walioteuliwa

Makamu wa Rais Dk Phillip Mpango amesema wakuu wa mikoa walioteuliwa wanatakiwa kukumbuka kuwa kiongozi ni lazima awe hodari wa kazi na pia mfano kwa tabia kwa watu anaowaongoza. 

“Sitarajii kwamba kutakuwa na walevi kati yenu sitarajii kama kutakuwa na orodha ya wazinzi ambao watafika katika ngazi zetu na mengine maovu katika jamii,” amesema Dk Mpango.

Makamu huyo wa Rais amesema kuwa kazi ambayo wakuu wa mkoa wanayo ni kusimamia vyema uchumi wa mikoa kwa kuongeza uzalishaji kwenye kilimo, viwanda na kusimamia tija kwa wananchi.


Soma zaidi


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewashauri viongozi hao kujua majukumu yao na kujifunza kile ambacho kinahitajika katika kazi zao kwa kujua mipaka yao na wanaotakiwa kufanya nao kazi.

“Wakuu wa mikoa ni wakuu wa Serikali kwenye maeneo yao ni matarajio yetu mtashirikiana na wale waliopo chini yenu kujua nini kinapaswa kufanyika, mnakwenda kuwatumikia wananchi nendeni mkawasikilize na mtatue changamoto zinazowakabili,” amesema  Majaliwa.

Kwa Mkurugenzi wa Takukuru Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Salum Hamduni, Spika wa Bunge Job Ndugai amemshauri kusimamia uwajibikaji na kuhakikisha ofisi yake inatenda haki kwa wananchi wote.

“Kumekua na uonezi na maonezi makubwa sana katika taasisi ya Takukuru ni vizuri mkajiangalie upya sisi ambao tunawakilisha wananchi tunaona. Si mahali pa kusema lakini waziri na wenzake watawasaidieni kwa upande mwingine. Si vizuri kuonea watu, haipendezi hata kidogo,” amesema Spika Ndugai.