September 29, 2024

Kamati yashauri Serikali kuwapatia Watanzania chanjo ya Corona

Kamati maalum ya iliyoundwa na Rais Samia Suluhu kuchunguza hali ya ugonjwa wa Corona nchini imependekeza kuwa Serikali iruhusu matumizi ya chanjo dhidi ya ugonjwa huo kwa Watanzania kwani ni salama na zimekidhi viwango vya kisayansi.

  • Yataka Watanzania waruhusiwe kupata chanjo kwa uhuru.
  • Yapendekeza kipaumbele kiwe kwa wahudumu wa afya na wazee.

Dar es Salaam. Kamati maalum ya iliyoundwa na Rais Samia Suluhu kuchunguza hali ya ugonjwa wa Corona nchini imependekeza kuwa Serikali iruhusu matumizi ya chanjo dhidi ya ugonjwa huo kwa Watanzania kwani ni salama na zimekidhi viwango vya kisayansi. 

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Profesa Said Aboud aliyekuwa akiwasilisha ripoti ya kamati yake kwa wanahabari Ikulu jijini Dar es Salaam leo (Mei 17, 2021) amesema kamati ilifanyia kazi hadidu za rejea 12 zilizohusu maeneo mbalimbali ya tathmini ya mwenendo wa ugonjwa pamoja na afua za udhibiti wa COVID-19 ikiwemo chanjo hapa nchini, kikanda na kimataifa.

“Tangu kuingia kwa ugonjwa wa COVID-19 nchini mwezi Machi 2020, Tanzania imekumbwa na mawimbi mawili makubwa na hivi sasa kutokana na mwenendo wa ugonjwa huo katika mataifa mengine duniani na kuna tishio la kutokea kwa wimbi la tatu hapa nchini,” amesema Prof Aboud. 

Prof Aboud amesema ili kujikinga na ugonjwa huo, kamati yake imependekeza mambo 19 ambayo Serikali inapaswa kuchukua ikiwemo kuruhusu utolewaji wa chanjo dhidi ya COVID-19 kwa Watanzania. 

“Kamati inashauri Serikali kwa kutumia vyombo vyake iendelee na hatua kuelekea kuruhusu matumizi huru ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 kwa kutumia chanjo zilizoorodheshwa na Shirika la Afya Duniani ili kuwapa fursa ya kinga wananchi wake kwa kuwa kupitia uchambuzi wa kamati, chanjo hizo zina ufanisi na usalama unaokubalika kisayansi,” amesema.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akipokea ripoti ya kamati maalum aliyoiunda kwa ajili ya kufanya tathmini ya ugonjwa wa Corona nchini kutoka kwa Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Said Aboud Ikulu Jijini Dar es Salaam leo. Picha| Ikulu.

Makundi ya kupewa kipaumbele

Kamati hiyo iliyoundwa Aprili mwaka huu, imependekeza kipaumbele cha utoaji wa chanjo dhidi ya COVID-19 nchini kiwe kwa wahudumu katika vituo vya kutolea huduma za afya na watumishi walio katika mstari wa mbele wa utoaji wa huduma, mathalani watumishi sekta ya utalii, hoteli, mipakani, viongozi wa dini na mahujaji. 

Makundi mengine yanayotakiwa kupatiwa kipaumbele ni wazee na watu wazima kuanzia umri wa miaka zaidi ya 50, watu wazima wenye maradhi sugu mengine kama kisukari, shinikizo la damu, maradhi ya mfumo wa upumuaji, magonjwa ya figo. 

Wengine ni watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama; na wasafiri wanaokwenda nje ya nchi.

Hata hivyo, Prof Aboud amesema pamoja na mapendekezo ya utoaji chanjo nchini, Kamati Huru ya Kitaifa ya Ushauri wa Chanjo (NITAG) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ziendelee kushirikishwa katika kutoa ushauri na kudhibiti chanjo hizo.  

Mapendekezo mengine ya kamati hiyo ni Serikali kufanya uhamasishaji na maandalizi ya upokeaji, utunzaji, usafirishaji na utoaji wa chanjo na wananchi wawe huru kuamua kuchanja au la na  Serikali iratibu upatikanaji wa chanjo kwa watumishi wa taasisi za kimataifa walioko nchini.

“Serikali ya Tanzania ijiunge na COVAX Facility kwa kuwasilisha andiko la kupatiwa chanjo, kwa kutumia fursa inayotolewa na GAVI,” amesema mtaalam huyo wa afya kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).


Soma zaidi: 


Huenda mapendekezo hayo ya kamati yakifanyiwa kazi na Serikali yatasaidia kuimarisha afya za Watanzania na kuwakinga dhidi ya janga hilo ambalo linaitesa dunia kwa sasa na kufungua milango ya upatikanaji wa taarifa sahihi za ugonjwa huo.

Tanzania iliacha kutoa taarifa za COVID-19 kwa umma Aprili 2020 ambapo hadi wakati huo kuliripotiwa visa 509 na vifo 21.

Hata hivyo, kamati hiyo imeshauri Serikali kuanza tena kutoa takwimu hizo kwa umma na Shirika la Afya Duniani (WHO).

“Serikali itoe takwimu sahihi za ugonjwa wa COVID-19 kwa umma na Shirika la Afya Duniani ili wananchi wapate taarifa sahihi toka Mamlaka za Serikali na kuheshimu makubaliano na kanuni ambazo nchi iliridhia,” amesema Prof Aboud.