September 29, 2024

Mikopo kwa sekta binafsi yaongezeka Tanzania

Mikopo kwa sekta binafsi nchini Tanzania imeongezeka kwa Sh465 bilioni hadi kufikia Sh20.5 trilioni katika mwaka unaoishia Machi 2021.

  • Imeongezeka hadi kufikia Sh20.5 trilioni katika mwaka unaoishia Machi 2021.
  • Kasi ya ukuaji wa mikopo hiyo imepungua kutoka asilimia 8.6 hadi asilimia 2.3.
  • Imechangiwa na athari za Corona kwenye shughuli za biashara. 

Dar es Salaam. Mikopo kwa sekta binafsi nchini Tanzania imeongezeka kwa Sh465 bilioni hadi kufikia Sh20.5 trilioni katika mwaka unaoishia Machi 2021 huku kasi ya ukuaji wake ikiwa chini kidogo ikilinganishwa na mwaka uliopita kutokana na athari za ugonjwa wa Corona katika shughuli za kibiashara.

Ripoti ya Mapitio ya Uchumi ya mwezi Aprili 2021 (Economic Monthly Review) iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) hivi karibuni inaeleza kuwa mikopo kwa sekta binafsi imeongezeka kwa asilimia 2.3 kwa mwaka unaoishia Machi 2021 sawa na ongezeko la Sh465 bilioni katika kipindi cha mwaka mmoja.

Kasi ya ukuaji huo bado  ipo chini kwa mara tatu zaidi ikilinganishwa na kasi ya ukuaji ya asilimia 8.6 iliyorekodiwa katika kipindi mwaka unaoishia Machi, 2020. 

BoT katika ripoti hiyo imesema, hali hiyo imesababishwa na janga la Corona ambalo limeathiri mwenendo wa biashara na shughuli za uchumi duniani. 

“Ukuaji huo usioridhisha kiwango cha mikopo kwa sekta binafsi imechangiwa kwa kiasi kikubwa na madhara ya COVID-19 kwa baadhi ya biashara hasa zile ambazo zinafanyika kimataifa,” imeeleza BoT katika ripoti hiyo. 

Biashara zilizoathirika ni za usafirishaji wa bidhaa za utalii na mazao ya biashara nje ya nchi. 


Zinazohusiana:


Hata hivyo, ripoti hiyo inaeleza kuwa sehemu kubwa ya mikopo kwa sekta binafsi imeendelea kuelekezwa kwa shughuli za watu binafsi au kaya ambazo zilipata wastani wa asilimia 35.6 ya mikopo yote (Zaidi ya theluthi ya mikopo yote) ikifuatiwa na shughuli za biashara zilizokuwa na wastani wa asilimia 15.4. 

Ukuaji wa mikopo katika shughuli zote kubwa za uchumi umeendelea kuongezeka, isipokuwa kwa shughuli za uchimbaji madini, uzalishaji viwandani, kilimo, biashara na ujenzi.

Mikopo inayoelekezwa katika sekta binafsi imekuwa chachu ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi nchini kwa sababu hutumika kutunisha mtaji na ununuzi wa malighafi na utoaji huduma katika shughuli mbalimbali. 

Hata wakati mikopo kwa sekta binafsi ikipungua, riba inayotozwa na benki za biashara imepungua kidogo, jambo ambalo linaweza kuwapa ahueni wakopaji. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, riba iliyotozwa kwenye mikopo iliyotolewa na benki mwaka unaoishia mwezi Machi 2021 ilikuwa asilimia 16.6 ikishuka kutoka asilimia 16.7 katika kipindi kama hicho mwaka jana.