November 24, 2024

Mafuta ya kula yachangia kupaa mfumuko wa bei Tanzania

Kasi ya mfumuko wa bei wa Taifa imeongezeka hadi kufikia asilimia 3.3 katika mwaka ulioshia Aprili 2021 kutoka asilimia 3.2 iliyorekodiwa Machi mwaka huu ikichangiwa zaidi na kupaa kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula ikiwemo mafuta ya kula.

  • Umeongezeka hadi kufikia asilimia 3.3 katika mwaka ulioshia Aprili 2021 kutoka asilimia 3.2 ya Machi mwaka huu.

Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei wa Taifa imeongezeka hadi kufikia asilimia 3.3 katika mwaka ulioshia Aprili 2021 kutoka asilimia 3.2 iliyorekodiwa Machi mwaka huu ikichangiwa zaidi na kupaa kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula ikiwemo mafuta ya kula.

Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na zinazotumiwa na kaya binafsi nchini. 

Taarifa ya mfumuko wa bei iliyotolewa Mei 10 2021 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaeleza kuwa bidhaa za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili mwaka huu zikilinganishwa na Aprili mwaka jana ni pamoja na ngano kwa asilimia 8.9, nyama (asilimia 4.2) na samaki wabichi kwa asilimia 28.1.

Bidhaa zingine ni dagaa wakavu kwa asilimia 22, mafuta ya kula (asilimia 24.6), matunda (asilimia 24.6), viazi mviringo (asilimia 5.7), viazi vitamu (asilimia 14.7), ndizi za kupika (asilimia 7.6), maharage (asilimia 6.4) na mihogo mikavu kwa asilimia 18.7. 


Zinazohusiana: 


Miezi ya hivi karibuni watumiaji wa mafuta ya kupikia wamekuwa wakilalamikia kupanda kwa kasi kwa bei ya bidhaa hiyo muhimu katika mapishi ya chakula majumbani. 

Katika maeneo mbalimbali hasa jijini Dar es Salaam, lita tano ya mafuta ya kula yanauzwa kati ya Sh26,000 hadi 29,000 kutoka bei ya awali ya Sh20,000 huku lita moja ikiuzwa mpaka Sh5,000 tofauti na bei iliyokuwepo ya Sh3500 kabla bidhaa hiyo haijapanda.

“Mfumuko wa bei za bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili 2021 umeongezeka hadi asilimia 4.8 kutoka asilimia 4.2 kwa mwaka ulioashia Machi 2021,” imeeleza taarifa ya NBS. 

Mfumuko huo wa bei umeongezeka kidogo baada ya kushuka kutoka asilimia 3.6 ya mwaka ulioishi mwezi Februari 2021 hadi asilimia 3.3 mwezi Machi mwaka huu.