October 6, 2024

Rais Samia aeleza sababu barakoa kutawala mkutano wa wazee Dar

Rais Samia Suluhu Hassan amesema yeye na watu waliohudhuria mkutano wa wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam wameamua kuvaa barakoa ili kuwakinga wazee dhidi ya ugonjwa wa Corona ambao unaitesa dunia kwa sasa.

  • Ni kuwakinga dhidi ya ugonjwa wa Corona.
  • Amesema katika mkusanyiko huwezi kujua nani ana maambukizi. 

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema yeye na watu waliohudhuria mkutano wa wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam wameamua kuvaa barakoa ili kuwakinga wazee dhidi ya ugonjwa wa Corona ambao unaitesa dunia kwa sasa.

Katika mkutano huo uliofanyika leo Mei 7 katika ukumbi wa Mlimani City jijini hapa, karibu wahudhuriaji wote walikuwa wamevaa barakoa ambazo ni moja ya kifaa tiba kinachovaliwa na kufunika eneo la pua na mdomo kwa lengo ya kuzuia maradhi mbalimbali ya kupumua hasa Corona. 

Rais Samia amesema wazee wako katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa huo na hivyo tahadhari ya kuwakinga popote walipo ni muhimu sana.


Zinazohusiana:


“Na mkusanyiko huu iliopo hapa ni mkubwa. Kwa hiyo ili tuwakinge wazee wetu tumeamua leo tuvae barakoa kwa sababu mkusanyiko huu ni mkubwa na tumeshindwa kuwaweka mbalimbali mmekaa pamoja. 

“Tulidhani kuvaa barakoo kutatusaidia kuwakinga wazee wetu na maambukizi kwa sababu huwezi kujua nani anayo, huwezi kujua nani hana,” amesema Rais Samia katika mkutano huo ambao umehudhuriwa na viongozi wa Serikali akiwemo Makamu wa Rais Dk Philip Mpango. 

Kiongozi huyo mkuu wa nchi amewaomba radhi wazee kwa sababu vijana na viongozi wa Serikali wanazunguka katika maeneo mbalimbali ikiwemo nje ya nchi na huenda wakapata maambukizi, hivyo kujikinga ni muhimu. 

“Sisi watoto wenu tunazunguka sana huko nchi zingine hatuwezi kujua kwa hiyo ni vema kujikinga sisi pamoja na nyie. Naomba mtuwie radhi sana kwa mba ule uhuru wa kuvuta hewa leo umebanika kidogo,” amesema Rais. 

Tahadhari nyingine ya kujikinga na Corona ambayo inapendekezwa na wataalam wa afya ni kunawa mikono mara kwa mara, kutumia kitakasa mikono na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima. 

Kwa mujibu wa mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge, wazee waliohudhuria mkutano huo ni zaidi ya 1,000 wakiwakilisha wazee ambao hawajafika ukumbini hapo.