October 6, 2024

Corona ilivyosaidia kupunguza magonjwa ya mlipuko Mwanza

Tahadhari ya kunawa mikono kwa maji na sabuni na kutumia vitakasa mikono ili kujikinga na ugonjwa wa Corona imeleta matokeo chanya baada ya kusaidia kupunguza magonjwa ya mlipuko kikiwemo kipindupindu katika Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza.

  • Ni tahadhari ya kunawa mikono yasaidia kupunguza kasi ya magonjwa hayo.
  • Magonjwa hayo ni kuhara na kipindupindu. 
  • Wananchi watakiwa kuendelea kuchukua tahadhari. 

Mwanza. Tahadhari ya kunawa mikono kwa maji na sabuni na kutumia vitakasa mikono ili kujikinga na ugonjwa wa Corona imeleta matokeo chanya baada ya kusaidia kupunguza magonjwa ya mlipuko kikiwemo kipindupindu katika Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza. 

Tangu kuibuka kwa ugonjwa Corona mwaka 2019, wataalam wa afya na viongozi wa Serikali wamekuwa wakisisitiza watu kuchukua tahadhari dhidi ya Corona kwa kuwataka watu kunawa mikono mara kwa mara. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Ilemela John Wanga amesema  wataendelea kusisitiza wananchi kufuata utamaduni huo kwa sababu umeonyesha matokeo mazuri katika mapambano ya magonjwa mengine yatokanayo na uchafu. 

“Mpango wa afya wa kunawa mikono umesaidia sana si tu kujikinga na vimelea vya ugonjwa wa corona, bali pia umepunguza wagonjwa wa kuhara na kipindupindu tofauti na ulivyokuwa miaka iliyopita,” amesema Wanga katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika leo Mei 7, 2021.

Bila kutaja takwimu, Wanga amesema kwa sasa kasi ya utoaji wa dawa za kutibu magonjwa yanayotokana na uchafu imepungua kutokana na  wagonjwa wanaokwenda katika vituo vya afya kupungua. 

Anasema kipindi cha nyuma magonjwa wa kuhara na kipindupindu yalilipotiwa kwa wingi katika manispaa hiyo, lakini kwa sasa hali ni tofauti.

Amewataka watendaji kuendelea kuwaelimisha na kuwasisitiza wananchi umuhimu wa kunawa mikono mara kwa mara. 

“Pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan kuunda tume ya wataalam watakaoshughulikia ugonjwa wa corona niombe kupitia hadhara hii kuwasisitiza mwendelee kuwataka wananchi kuzingatia mpango huo, ” amesema Wanga.


Zinazohusiana:


Janga la Corona bado linaitesa dunia kwa sasa ikizingatiwa kuwa maambukizi yanaongezeka kila siku. 

Awali Diwani wa viti maalum Kata ya Pasiansi,  Rosemary  Mayunga aliomba mwongozo baada ya ndoo zilizokuwa zimewekwa kwenye maeneo ya umma kwa ajili ya kunawa mikono kuondolewa. 

Rosemary amesema  ni vema mpango huo uendelee ili kujikinga na vimelea mbalimbali vya magonjwa yatokanayo na uchafu. 

Hoja hiyo pia iliungwa mkono na Andrew Nginila, diwani wa Gata ya Nyamhongolo ambaye alisema vifaa vyote  vilivyokuwa vimewekwa maeneo  ya stendi na maofisini virudishwe na vifanye kazi. 

“Asiwepo mtu anaingia ofisini au kwenye chombo cha usafiri pasipo kunawa mikono au kupaka kitakasa mikono, “amesema Nginila.