October 6, 2024

Utumie muda gani kuingia kwenye mahusiano mapya?

muda sahihi ni pale moyo wako unapokuwa umekubali kuendelea na maisha yako baada ya mahusiano yako ya awali kuvunjika.

  • Hakuna nambari ya maajabu ya kusema lini moyo wako utakuwa tayari kwa safari mpya.
  • Kinachotakiwa ni kuusikiliza moyo wako na kujua sababu ya nini unahitaji katika mahusiano.
  • Unaweza kutumia muda wako kwa kujipenda mwenyewe kwanza.

Dar es Salaam. “Sitokuja kupenda tena” ni baadhi ya maneno ambayo watu husema baada ya mahusiano yao ya kimapenzi kwenda kombo lakini jambo la kushangaza baada ya muda mfupi watu hao huingia kwenye mahusiano mapya na kusahau yote yaliyopita.

Ni kweli haipo namba ya maajabu inayotoa muongozo wa lini uingie katika mahusiano mapya baada ya mahusiano yako ya awali kuvunjika na kukuacha ikiwa na vipande vya moyo wako lakini ukiusikiliza moyo wako, nambari hiyo unaweza kuipata.

Wengine huchukua wiki, wengine miezi na wengine miaka huku wengine tayari wakiweza kuwa na mahusiano mapya ndani ya siku moja tu pale ya zamani yanapokufa na hivyo kuharakisha kuponya nafasi zao.

Hata hivyo, wakati ngalawa ya mahusiano yaliyoharakishwa ikiweza kusafiri katika bahari ya huba iliyo na mawimbi kufikia lengo, baadhi ya mahusiano yamekuwa yakishindwa kufikia safari iliyodhaniwa.

Moyo uliovunjika kuuvunja mwingine

Safari iliyoanza na mtu kuingia katika mahusiano mapya wakati bado moyo wake una maumivu ya mahusiano yaliyopita, huwa na changamoto nyingi. 

Katika hali hiyo, ni vigumu mtu kupenda “mazima” na hata kumruhusu mwenzi wake ampende kama anavyotaka kumpenda. Ni katika hatua hiyo ambapo neno “nakupenda”  na “nakupenda pia” husemwa na kujibiwa kwa mazowea.

Na juhudi za mtu kuonyesha kuwa anampenda mwenziwe zinaweza kuwa ni za bure kwani huenda mwenzi huyo ameshawahi kufanyiwa yote hayo na bado akaishia kuvunjika moyo.

Wawili hao wanakuwa katika mzunguko wa sintofahamu na labda ambazo zinaweza kumsababisha mmoja wao siku moja kuikatisha safari hiyo ambayo imeshindwa kuliona jua la asubuhi. Ni penzi lingine limevunjika na huenda limeacha moyo mwingine ukiwa umevunjika.

Kabla ya kuamua kuingia kwenye mahusiano mapya, hakikisha haufungamani na mahusiano yako ya zamani. Picha| Marriage.com

Imani juu ya mahusiano kushuka na mahusiano kuwa mchezo wa pata potea

Mtazamo wa vijana wengi wenye mahusiano kwa sasa umebadilika, baadhi wanasema soko ni gumu na ukimpata anayekupenda, mshikilie kwani mapenzi ya dhati kwa sasa “hayapo”.

Unaweza ukawa na mpenzi wako ambaye ana mpenzi wake mwenye mpenzi wake mwingine. Ni sawa na kusema upo  katika mnyororo ambao haujui mwisho wake lakini kwa baadhi huamua kutulia humo humo kusikilizia upepo unavyoenda. 

Hali hiyo inafanya imani juu ya mahusiano kwa sasa kupungua na wengi kutumia mahusiano kama uwanja wa kuwachezea wengine ambao mioyo na mapenzi yao yanakuwa ya dhati na yapo tayari kupata mtu mmoja tu kati ya mabilioni wa kuchangia naye muda mchache ambao upo duniani.


Soma zaidi:


Kumpata mmoja kati ya mabilioni waliopo duniani

Unaweza kusema ni kupitia ndoa lakini hata ndoa nazo huvunjika. Kumpata mtu mmoja ambaye atakuwa tayari kukukubali kwa jinsi ulivyo na yeye kuwa tayari kumpenda na madhaifu yake inachukua muda na moyo wako kuvunjika katika vipande ambavyo ni vigumu kurudishiwa.

Kwa wengine wana bahati kwa kukutana na mtu mmoja ambaye inakuwa ni kama wawili hao wametengenezwa mahususi kwa ajili yao. Kwa baadhi safari huwa ni ndefu kidogo.

Hata hivyo, kumpata mtu huyo siyo kwamba haiwezekani bali inakuhitaji kuwa tayari, kuwa na uvumilivu kwani unatakiwa kukubali ya kuwa hakuna binadamu ambaye amekamilika na kuambatana na sifa zote ambazo wewe unahitaji mtu awe nazo.

Hivyo pale unapoingia katika mahusiano mapya, jiulize, ni kipi umejifunza katika mahusiano yako yaliyopita na kuna sababu gani wewe kuingia katika mahusiano mapya kwa muda huo. 

Usiende kuuzunguka ulimwengu ukivunja mioyo ya watu ambao wapo tayari kukupenda.