November 24, 2024

Tanzania yazuia ndege kutoka India kujikinga zaidi na Corona

Imetangaza kusitisha ndege zote zinazotoka na kwenda India kuanzia Mei 4 mwaka huu ili kujikinga na ongezeko la maambukizi ya ugonjwa huo yanayozidi kuongezeka nchini humo.

  • Hatua hiyo ni kutokana na kuongezeka kwa maambukizi nchini humo. 
  • ATCL nayo yazuia ndege zake kwenda India.
  • Huu ni waraka wa pili kutolewa ndani ya Saa 24.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imezidi kuchukua hatua zaidi za kujikinga na ugonjwa wa virusi vya corona (Covid-19) baada ya kutangaza kusitisha ndege zote zinazotoka na kwenda India kuanzia Mei 4 mwaka huu ili kujikinga na ongezeko la  maambukizi ya ugonjwa huo yanayozidi kuongezeka nchini humo.

Hatua hiyo inakuja ndani ya saa 24 baada ya Serikali kutangaza hatua zaidi za kujikinga na virusi hivyo kwa kuweka masharti zaidi kwa wageni wanaoingia nchini ikiwemo kujiweka karantini na kuwa na cheti chenye majibu hasi ya Covid-19.  

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kwa siku ya jana pekee India imeripoti maambukizo mapya 357,229 idadi iliyofanya taifa hilo kurekodi jumla ya visa vya Corona milioni 20.3 na vifo 222,408 tangu ugonjwa huo uripotiwe mwaka juzi. 

Kwa idadi hiyo, India inakuwa nchi ya pili duniani yenye maambukizo ya juu ya Covid-19 duniani baada ya Marekani.

Katika waraka mpya kwa wasafiri (Travel advisory), Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Profesa Abel Makubi amesema wameamua kuzuia usafiri wa ndege kutoka India ili kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa huo ikizingatiwa kuwa maambukizi na vifo katika nchi hiyo yanazidi kuongezeka.

“Kutokana na hali ya sasa ya janga hili India, ndege zote za kuingia na kutoka India zimesitishwa. Zuio hili litadumu mpaka itakapotangazwa tena,” amesema Prof Makubi katika waraka namba sita wa Serikali kuhusu wasafiri wa kimataifa wanaokuja nchini. 

Hata hivyo, Prof Makubi amesema zuio hilo halitahusu ndege za mizigo na zile zilizopo kwenye kazi maalum ikiwemo za misaada na diplomasia zilizothibitishwa na maamlaka. 


Soma zaidi: 


Wasafiri wote wanaotokea nchini India au waliopitia India ndani siku 14 zilizopita bila kujali njia waliotumia watatakiwa kupimwa ugonjwa huo katika maeneo wanayoingilia, watafuatiliwa watu waliokutana nao na kujikarantini kwa gharama zao kwa siku 14. 

Prof Makubi amesema Watanzania wanaorudi kutoka India kwa ajili ya masomo, shughuli za kibiashara ama kwa ajili ya matibabu, watalazimika kufuata taratibu zilizoanishwa katika waraka huo. 

Amesema katika viwanja vya ndege, bandarini na mipaka, tahadharia zote zitaendelea kuchukuliwa ikiwemo kuweka vifaa vya kunawia mikono, vitakasa mikono, kukaa umbali wa mita moja kutoka mtu mmoja kwenda mwingine na kuhimiza watu kuvaa barakoa. 

Tanzania inakua ni miongoni mwa mwa nchi mbalimbali za Afrika ambazo zimezuia ndege kutoka India. Nchi zilizoweka zuia hilo ni pamoja na Uganda, Djibouti na Nigeria.  

Wakati Serikali ikitoa mwongozo huo, Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) nalo limetangaza kusitisha safari zake kwenda nchini India kuanzia Jumanne hii mpaka hadi hapo itakapotoa taarifa nyingine ya kurudisha safari hizo.

“ATCL itaondoa faini zote kutokana na mabadiliko haya, itatoa tiketi nyingine au kuwarudishia nauli zao abiria waliokuwa wamekata tiketi,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Ladislaus Matindi katika taarifa yake iliyotolewa Mei 4.

Abiria wote wenye tiketi za ATCL, Matindi amewashauri kuwasiliana na ofisi za ATCL au mawakala wao kwa taratibu za kubadilisha tiketi ili zitumike pindi safari zitakaporejea. 

Mwezi uliopita, Rais Samia Suluhu Hassan alitangaza kuwa ameunda kamati ya wataalamu itakayomshauri juu ya hatua za kuchukua kukabiliana na Covid-19 inayozidi kusumbua mataifa mbalimbali ulimwenguni. 

Rais Samia mara kadhaa amekuwa akiwataka Watanzania kuchukua tahadhari zote zinazopendekezwa na wataalam wa afya  za kujikinga na ugonjwa huo.