October 6, 2024

Bei ya vifaa vya kujipima VVU yashuka kwa asilimia 50

Vifaa hivyo vinavyotumiwa na mtu binafsi kujipima Virusi Vya Ukimwi (VVU) sasa vitauzwa chini Sh4,600 duniani.

  • Vifaa hivyo vinavyotumiwa na mtu binafsi kujipima  Virusi Vya Ukimwi (VVU) sasa vitauzwa chini Sh4,600 duniani.
  • Kwa sasa Watanzania wanaruhusiwa kisheria kujipima wenyewe VVU.
  • Wataalam wa afya wasema bei hiyo itasaidia watu wengi kujua hali zao za kiafya. 

Dar es Salaam. Huenda kasi ya watu kufahamu na kuwa na uhakika wa afya zao ikaongezeka Tanzania baada ya kuripotiwa kushuka kwa bei ya vifaa vya kujipima Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Shirika la kimataifa la kufanikisha uwepo wa tiba nafuu duniani (Unitaid) limetangaza ongezeko la upatikanaji katika soko na kushuka kwa bei ya vifaa vinavyotumiwa na mtu binafsi kujipima  Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwa asilimia 50.

Kuanzia sasa vikasha vya kujipima VVU vinavyotumia damu vitauzwa kwa chini ya Dola za Marekani 2 (chini ya Sh4,637) kila kimoja katika nchi 135 zinazokidhi vigezo.

Mwaka jana Bunge la Tanzania lilirasimisha sheria ya wananchi kuweza kujipima wenyewe maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na sasa vifaa vinauzwa kwenye maduka, pia kugawiwa bure katika baadhi ya maeneo.

Unitaid ambayo iko chini ya Shirika la Afya Duniani (WHO), limesema hatua hiyo inafuatia makubaliano yaliyofanywa baina yake na kampuni binafsi ya huduma za afya ya Viatris kupitia kampuni mamaMylan. 

“Kitendo cha mtu kupata vifaa vya kujichunguza mwenyewe VVU kimetambuliwa kuwa kigezo muhimu katika kufikia lengo la kimataifa la asilimia 90 ya watu kufahamu iwapo wameambukizwa VVU au la. 

Katika kipindi cha miaka 6 iliyopita ,kiwango hicho cha kutambua hali ya VVU kwa mtu kilikuwa kimeongezeka kutoka asilimia 45 hadi 81,” amesema Msemaji wa Unitaid, Herve Verhoosel katika taarifa yake iliyotolewa Aprili 29, 2021.  


Zinazohusiana:


Shirika hilo limesema kifaa hicho ni muhimu zaidi kwa nchi za kipato cha chini na kati, ambako unyanyapaa umeshamiri na changamoto za huduma za afya zinaweza kuwa vikwazo. 

Kwa mujibu wa Verhoosel, kupanuka kwa soko la vifaa hivyo kunaweza kuwasaidia watu milioni 8 ambao wanakadiriwa kutofahamu hali yao ya VVU duniani. 

Tangu mwaka 2015, wawekezaji wa Unitaid wamewezesha kusambazwa kwa vifaa hivyo milioni 5, ambapo vikasha milioni 21 vinatarajiwa kuwa vimesambazwa kati ya mwaka 2020 hadi 2023. 

Zaidi ya hapo tayari nchi 85 zimejumuisha vifaa hivyo vya kujipima VVU katika sera zao za afya za nchi zao.