Rais Samia aanika vipaumbele vyake akilihutubia bunge
Kiongozi huyo amesema serikali itatilia mkazo katika uwekezaji na kuboresha sekta za kilimo, utalii na ufugaji.
- Kiongozi huyo amesema serikali itatilia mkazo katika uwekezaji na kuboresha sekta za kilimo, utalii na ufugaji.
- Pia, amesema Serikali anayoiongoza haitoacha nyuma teknolojia kwa maendeleo ya nchi.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameanika vipaumbele mbalimbali ambavyo Serikali inayoingoza itavitekeleza katika kipindi cha miaka mitano ijayo ikiwemo kukuza uchumi wa nchi, kuboresha sekta ya kilimo na viwanda ili kufungua fursa mbalimbali za ajira kwa Watanzania.
Rais Samia ameyasema hayo Bungeni leo (Aprili 22, 2021) jijini Dodoma huku akiweka wazi kuwa vipaumbele hivyo ni vile ambavyo vilianza kutekelezwa na Serikali iliyokuwa akiongozwa na Hayati John Magufuli.
Katika nyanja ya uwekezaji na biashara, Rais Samia amesema Serikali itapitia upya sera za uwekezaji ili kuondoa vikwazo ambavyo vinafanya wawekezaji wasije kuja kuwekeza nchini.
Vikwazo vitafanyiwa kazi ni pamoja na ugumu wa kupata vibali vya kufanya kazi nchini, upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya kuwekeza, mlundikano wa kodi na tozo kwa wafanyabiashara
“Mwelekeo utakuwa ni kurudisha imani ya wawekezaji na kutoa vivutio kwa wawekezaji mahiri ikiwa ni pamoja na kuwezesha uwekezaji kufanyika kwa haraka,” amesema Rais Samia.
Kiongozi huyo wa nchi amesema Serikali itafanya mapitio katika utendaji wa sekta mbalimbali ambazo imewekeza ikiwemo Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) na kuhakikisha linafanya kazi kwa tija.
“Katika miaka mitano ijayo tunahitaji uwekezaji mkubwa sana katika sekta za uzalishaji na zinazotoa ajira kwa wingi,” amesema Rais Samia.
Amesema Serikali itashughulikana vikwazo vitafanyiwa kazi na tozo kwa wafanyabiashara. Picha| Daniel Samson.
Miundombinu na mawasiliano
Serikali ya Rais Samia itaendelea na ujenzi wa miundombinu zikiwemo babarabara, viwanja vya ndege ili kurahisisha shughuli za biashara na utoaji wa huduma za kijamii.
Kwa upande wamawasiliano, Rais Samia amesema Serikali itaongeza watumiaji wa intaneti na kufikisha huduma za mawasiliano ya simu kwa Watanzania wengi zaidi.
“Kufikia hilo ni pamoja na kuongeza wigo wa matumizi ya mawasiliano ya kasi (broadband) kutoka asilimia 45 ya sasa hadi asilimia 80 ifikapo mwaka 2025,” amesema Mama Samia.
Aidha, Rais Samia amesema ataangazia kupanua wigo wa vivutio vya utalii kwa kujenga miundombinu ya kuwezesha meli za kitalii kuzuru nchini na kuhamasisha wawekezaji kuwekeza kwenye miundombinu ya utalii ikiwemo mahoteli ili kupunguza gharama za malazi.
“Tunajipanga kusomesha vijana wengi katika taaluma ya utalii ili waweze kuendesha maeneo mbalimbali ya sekta hiyo bila kutegemea wataalamu kutoka nje,” amesema Rais ambapo malengo ni kufikisha watalii milioni 5 ifikapo 2025.
Soma zaidi:
- Rais Samia atoa onyo kali kwa wanaofanya uchonganishi mtandaoni
- Huu ndiyo mwelekeo wa Serikali ya awamu ya sita Tanzania
Ataimarisha huduma za afya na maji
Amesema Serikali itaendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa kujenga miundombinu na kuongeza watumishi, vifaa tiba, dawa na vitendanishi na kuendeleza juhudi za kupunguza vifo kwa wajawazito na watoto.
“Huwa nasikitika sana kuona kina mama wanakufa wanapojifungua kwa sababu ambazo zinaweza kuzuilika,” amesema Rais Samia huku nguvu zaidi itaelekezwa katika kinga na tiba kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanayoigharimu Serikali fedha nyingi.
Katika sekta ya maji ambayo pia ina mchango mkubwa katika maendeleo, Rais Samia amesema Serikali inaanza kushughulika na miradi ambayo usimamizi wake ni mbovu ambayo imetumia fedha nyingi kuijenga.
“Hapa niseme, nakwenda kufanya mabadiliko makubwa ya mainjinia (wahandisi) wa maji huko kwenye mikoa. Kwa maeneno ambayo hayana kabisa vyanzo vya maji, tunakwenda kuchimba mabwawa ya kuvuna maji ya mvua,” amesema Rais Samia.
Jitihada zigine ni pamoja na kuongeza watumiaji wa intaneti, kuboresha miundombinu na kuongeza uwajibikaji kwa watumishi wa umma. Picha| Daniel Samson.
Kilimo na mifugo havitaachwa nyuma
Rais Samia amesema sekta hizi licha ya kuajiri Watanzania wengi, bado hazifanyi kazi kwa tija kwa sababu zinaendeshwa kwa mazoea na hivyo Serikali inaenda kuwekeza nguvu kubwa katia upatikanajiwa teknolojia ya kisasa na matumizi ya mbegu bora za kilimo na ufugaji wa kisasa.
“Tutabadilisha kosaafu (breed) ya mifugo yetu ili kuwawezesha wafugaji kuwa na mifugo michache yenye sifa za uzalishaji mkubwa uwe wa nyama au maziwa na kuongeza tija,” amesisitiza Rais.
Serikali pia ina mpango wa kununua meli 8 za uvuvi ili zitumike katika uvuvi wa bahari kuu na kuwaongeze tija wavuvi na Serikali.
Pia kuimarisha mahusiano ya kimataifa, wahisani, vyama vya upinzani, kutumia balozi zilizopo kibiashara ikiwa ni pamoja na kutangaza utalii.
Serikali pia inakusudia kufanya mapitio ya sera ya mambo ya nje ya mwaka 2000 ili iendane na mahitaji ya sasa ya dunia, hiyo ni hatua ya ushiriki wa Tanzanaia kwenye shughuli za kImataifa ili kulinda amani duniani.
Rais Samia pia amesema Serikali itaangazia maslahi ya watumishi wa umma ikiwa ni pamoja na kuwapandisha vyeo na kuongezea mishahara kwa wale wanaostahili.
Serikali haitoacha kupambana vikali na viongozi wabadhirifu, wizi na wanaotumia mali za umma kwa maslahi yao.
Katika sekta ya nishati, Samia amesema serikali itaangalia uwezekano wa kuwekeza katika miradi ya nishati jadidifu inayotokana na jua, upepo, na jotoardhi.