November 24, 2024

Ubakaji unavyotumika kuhalalisha ndoa duniani

Nchi 20 duniani zikiwemo sita za bara la Afrika bado zinawaruhusu wabakaji kuwaoa wanawake au wasichana waliowabaka ikiwa ni njia ya kuepuka kutiwa hatiani, ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) imeeleza.

  • Ni sheria za nchi 20 duniani ikiwemo Libya zinawaruhusu wabakaji kuwaoa wanawake au wasichana waliowabaka.
  • Hiyo ni moja ya sharti la kuepuka adhabu ya kwenda jela.
  • Jumuiya za kimataifa zalaani sheria zataka zibadilishwe.

Dar es Salaam. Nchi 20 duniani zikiwemo sita za bara la Afrika bado zinawaruhusu wabakaji kuwaoa wanawake au wasichana waliowabaka ikiwa ni njia ya kuepuka kutiwa hatiani, ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) imeeleza.

Ripoti hiyo ya hali ya idadi ya watu duniani iliyotolewa Aprili 14, 2021 imejikita kupima nguvu za wanawake kufanya  maamuzi yao wenyewe kuhusu miili yao na kiwango ambacho sheria za nchi zinaunga mkono au zinaingilia haki ya mwanamke kufanya maamuzi. 

Angola na Libya ni miongoni mwa nchi hizo ambazo sheria zao zinaruhusu mtuhumiwa wa ubakaji kukiri kukosa na kuachiwa kwa masharti ya kukubali kumuoa na kuishi na mtu aliyembaka. 

“Katika baadhi ya nchi, ndoa inaweza kuchukuliwa ni halali kuponya ubakaji kwa kuwaruhusu wahalifu kuwaoa waathirika ili kuepuka adhabu ya uhalifu wao,” imeeleza sehemu ya ripoti hiyo

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa katika nchi zinazoendelea ambazo taarifa zinapatikana ni asilimia 55 pekee ya wanawake wamepewa uwezo kamili wa kisheria wa kufanya uchaguzi juu ya huduma za afya, uzazi wa mpango na uwezo wa kusema ndiyo au hapana kwenye tendo la ndoa. 

UNFPA imeeleza kuwa ukosefu huo wa uhuru wa mwili una athari kubwa kwa  wanawake na wasichana kwani inaenda mbali zaidi kuvuruga uzalishaji wa uchumi, kupunguza ujuzi, na kusababisha gharama za ziada kwa huduma za afya  na mifumo ya kimahakama.

“Ukiukwaji wa haki hauwezi kufunikwa na sheria. Sheria za “Kuolewa na mbakaji” zinaamisha mzigo wa tuhuma kwa mwathirika na kujaribu kutakasa hali hiyo ambayo ni kosa,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA, Dk Natalia Kanem wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo. 

Nchi zingine ni Urusi, Serbia, Thailand na Venuzuela. 

Mwaka 2017, shirika lisilokuwa la kiserikali la kimataifa la  Equality Now lilifanya utafiti wa kina kuhusu ndoa hizo zinazotokana na makosa ya ubakaji na kubaini kuwa nchini Iraq, ikiwa mtuhumiwa wa ubakaji akimuoa mwanamke aliyembaka, mashtaka dhidi yake yanabatilishwa. 

Hata kama hukumu imetolewa inaondolewa lakini mtuhumiwa anaweza kuhukumiwa tena akiwa aliyemuoa atampa talaka ndani ya miaka mitatu.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa nchini Urusi, kama mbakaji amefika umri wa miaka 18 na akamnajisi msichana aliye na miaka chini ya 16, ataepuka hukumu ya kufungwa jela kama atakubali kumuoa. 


Zinazohusiana:


Pia nchini Thailand, ndoa inaweza kutumika kusuruhisha kesi ya ubakaji ikiwa mtuhumiwa ana miaka zaidi ya 18 na aliyebakwa ana miaka zaidi ya 15. Ndoa itafungwa na wawili hao kama mahakama itakubali aliyebakwa aolewe kwa ridhaa yake. 

Jumuiya za kimataifa ikiwemo UNFPA zimeeleza kuwa huo ni ukiukwaji mkubwa wa haki za wanawake na wasichana na imezitaka nchi hizo kufanya mabadiliko ya sheria zinazowalinda wanawake na siyo kuwakandamiza.