Zaidi ya Sh121 bilioni kutumika kutangaza utalii Tanzania
Serikali imetenga Sh121.9 bilioni katika mwaka wa fedha wa 2021/22 ambazo zitatumika kuboresha miundombinu na kutangaza vivutio vya utalii ili kuongeza mapato na idadi ya watalii wanaokuja Tanzania.
- Serikali imetenga zaidi ya Sh121.9 bilioni kutangaza na kuboresha miundombinu ya sekta ya utalii nchini kwa mwaka 2021/22.
- Pia inapanga kujenga chuo cha masuala ya utalii kwa ajili ya kufua wadau wa utalii ili kuifanya sekta hiyo kuwa imara zaidi.
- Hadi sasa Tanzania ina chuo kimoja tu cha masuala ya utalii.
Dar es Salaam. Serikali imetenga Sh121.9 bilioni katika mwaka wa fedha wa 2021/22 ambazo zitatumika kuboresha miundombinu na kutangaza vivutio vya utalii ili kuongeza mapato na idadi ya watalii wanaokuja Tanzania.
Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mary Masanja aliyekuwa akizungumza leo Aprili 16, 2021 Bungeni jijini Dodoma, amesema fedha hizo zitatumika katika kuboresha miundombinu na kuhakikisha kuwa vivutio vya utalii nchini vinatangazwa kwa nguvu zote ili kuvutia utalii wa ndani na wa kimataifa.
Masanja amesema kati ya fedha hizo, Sh46.5 bilioni zitatumika kwa ajili ya utangazaji wa vivutio vya utalii ili kuvutia utalii wa ndani na hata wa kimataifa.
“Kwenye utangazaji bila kuimarisha miundombinu inakuwa changamoto. Tumetenga Sh75.4 bilioni ambazo zitaimarisha miundombinu iliyopo kwenye hifadhi hizo,” amesema Masanja wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Rita Kabati aliyetaka kujua mikakati ya Serikali katika kutangaza vivutio vya utalii.
Endapo matangazo hayo yatafanyika, itasaidia kuimarisha sekta ya utalii ambayo imeathiriwa na janga la Corona ambalo limesababisha baadhi ya nchi kuweka vikwazo vya usafiri wa ndege na raia wake kwenda nchi za nje.
Soma zaidi:
- CAG alivyobaini ‘matundu’ mfumo wa Tehama wizara ya maliasili na utalii
- Sekta ya utalii ilivyoimarika wakati wa uongozi wa Magufuli
- Serikali kuanzisha utalii wa meli Ziwa Victoria
Aidha, Masanja amesema Serikali imepanga kuboresha elimu miongoni mwa Watanzania juu ya masuala ya utalii kwa kujenga chuo cha utalii.
“Serikali ina mpango mkubwa wa kuanzisha vyuo ambazo vitakuwa ni kampasi. Tunaanzisha kampasi ya Mweka lakini pia kutakuwa na chuo cha mambo ya utalii ambacho kitaanzishwa kama kampasi ya Iringa,” amesema Masanja ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum.
Kuanzishwa kwa chuo hicho kutasaidia kuongeza idadi ya wataalam wa masuala ya utalii ambao wanahitajika kutoa huduma mbalimbali wa watalii wanaotembelea vivutio vya utalii nchini.
Hadi sasa, Tanzania ina chuo kimoja cha Utalii cha Taifa ambacho kinatoa kozi mbalimbali za utalii.