November 24, 2024

Wafanyabiashara wadogo kuruhusiwa kufanya biashara saa 24 Tanzania

Ni baada ya kujiridhisha kama miundombinu inayohakikisha usalama wao na mali zao ipo katika maeneo husika.

  • Ni baada ya Serikali kujiridhisha kama miundombinu inayohakikisha usalama wao na mali zao ipo katika maeneo husika.
  • Miundombinu hiyo ni pamoja na taa za barabarani, kamera na sehemu za kufanyia biashara zao.
  • Serikali yaahidi kusaidia halmashauri ambazo zitaanza kujenga miundombinu kwa ajili ya kuwasaidaia wafanyabiiashara hao.

Dar es Salaam. Kufuatia uhaba wa maeneo ya kufanyia biashara, Serikali imesema inaangalia uwezekano wa kuwaruhusu wafanyabiashara wadogo wadogo kufanya biashara zao kwa saa 24 endapo miundombinu itakuwa rafiki.

Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) David Silinde Silinde amesema tayari yapo baadhi ya maeneo ambayo yanaendesha biashara hadi usiku ili kuwezesha Serikali kupata mapato kupitia shughuli hizo. 

“Yameanzishwa masoko ya usiku yanayoendeshwa kwa kufunga baadhi ya mitaa nyakati za jioni hadi usiku kwa kupisha wafanyabiashara wadogo kuendesha biashara zao,” amesema Silinde leo Aprili 13, 2021 katika kipindi cha maswali na majibu bungeni jijini Dodoma. 

Baadhi ya halmashauri ambazo zina utaratibu huo ni pamoja na Jiji la Dodoma, Jiji la Dar es Salaam na Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Endapo wafanyabiashara wataruhusiwa kufanya kazi zao kwa saa 24, kutasaidia kuimarisha uchumi wao na pia kuongeza kipato kwa taifa. Picha Quartz.

Aidha, Silinde amesema utaratibu huo unaweza kutumika katika maeneo mengine nchini ikiwa kutakuwa na miundombinu ya kutosha hasa inayowezesha usalama wa wafanyabiashara na mali zao ikiwemo taa, kamera maalum na maeneo ya kuhifadhia bidhaa. 

“Ili kuwa na usalama wa uhakika katika masoko, kunahitajika ulinzi wa polisi au askari wa akiba kwa maana ya mgambo hususan nyakati za usiku,” amesema Silinde wakati akijibu swali la Mbunge wa Mafinga Mjini, Kosato Chumi.

Chumi katika swali lake alitaka kufahamu kama Serikali iko tayari kuwaruhusu wafanyabiashara wadogo wadogo wanaoishi kwenye miji iliyo kando ya barabara kuu kufanya biashara kwa saa 24.

“Sisi kama Halmashauri (ya Mafinga) tuko tayari kujenga baadhi ya miundombinu lakini Je Serikali ipo tayari kutusaidia japo taa za barabarani katika maeneo muhimu?,“ ameuliza chumi katika swali kuhusu wafanyabiashara wa jimbo lake.


Soma zaidi:


Hiyo siyo mara ya kwanza kwa viongozi wa Serikali kutoa tamko ya kuwawezesha wafanyabiashara kuendesha shughuli zao kwa saa 24 lakini kinachokosekana ni utashi na miundombinu rafiki itakayofanikisha azma hiyo ambayo inaweza kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi. 

Mwaka 2019, aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliahidi kuweka kamera maalum za usalama na taa katika mitaa ya Dar es Salaam ikiwemo Kariakoo ili kuwawezesha wafanyabiashara kuendelea na kazi hata nyakati za usiku.

Lakini mpaka leo suala hilo halijafanyiwa kazi. 

Licha ya kuwa jambo hilo ni zuri, katika maeneo ambayo wafanyabiashara wanafanya shughuli zao usiku kumeibua changanoto ya foleni na msongamano wa watu hasa kwenye barabaraba ambazo vyombo vya usafiri vinapita. 

Usimamizi wa jambo hili ukiwekewa mikakati mizuri utasaidia kuongeza kasi ya ufanyaji biashara nchi na hivyo kuingozea Serikali mapato.