November 24, 2024

Tuhuma za ubadhirifu zinavyotishia miaka 27 ya bosi wa bodi ya utalii Tanzania

Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Damas Ndumbaro amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Devota Mdachi kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu zinazomkabili.

  • Ni Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Devota Mdachi aliyesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu.
  •  Amehudumu katika taasisi hiyo kwa takriban miaka 27 sasa.

Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Damas Ndumbaro amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Devota Mdachi kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu dhidi ya mama huyo aliyehudumu katika taasisi hiyo kwa takriban miaka 27 sasa.

Mdachi, aliyejiunga TTB mwaka 1994 kama ofisa anayeshughulikia habari kwa watalii, anatuhumiwa kufanya ubadhirifu wa fedha pamoja na masuala ya utawala yanayohusu rasilimali watu katika ofisi yake.

Mama huyo ni moja ya watumishi waliohudumu kwa muda mrefu zaidi TTB akipanda vyeo kwa nyakati tofauti hadi kufikia cheo hicho cha juu kwenye taasisi hiyo.

Kufuatia kutengeliwa kwa Mdachi, Dk Ndumbaro amemteua Betrita Lyimo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) kukaimu nafasi hiyo hadi uchunguzi utakapokamilika.

Tuhuma hizo, zilizoelezwa na Dk Ndumbaro hazihusiani na ripoti ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), zinakiweka kibarua cha Mdachi shakani ikizingatiwa kuwa amehudumu TTB tangu ikiwa na mwaka mmoja tu kuanzishwa kwake.


Zinazohusiana


Mdachi alikuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo katika taasisi hiyo ya utalii baada ya kuteuliwa na Rais wa nne wa Tanzania Jakaya Kikwete, Oktoba 2015. Kabla ya uteuzi wake, Mdachi (55) alikuwa Mkurugenzi wa Masoko wa TTB.

Iwapo atakwepa mishare ya uchunguzi huo mpya wa wizara, Mdachi atakuwa na kibarua cha kupangua hoja nyingine zilizoanishwa katika ripoti ya CAG ya mwaka wa fedha wa 2019/20.

CAG Charles Kichere, miongoni mwa mambo mengine, ameeleza kuwa TTB “haina mpango-mkakati katika kutangaza na kukuza utalii wa ndani bali ilikuwa na mpango-mkakati wa kutangaza utalii wa Tanzania nje ya nchi.”

“Aidha, Dk Ndumbaro ameielekeza Bodi ya Wakurugenzi ya TTB kuwasimamisha kazi watumishi wengine wanaohusika na tuhuma hizo kwa kuwa suala hilo chini ya mamlaka yao ili waweze kupisha uchunguzi dhidi ya madai yanayowakabili,” inaeleza taarifa ya wizara ya masiliali na utalii iliyotolewa Aprili 10 mwaka huu.