Mbinu tano za kubaini habari feki WhatsApp
Mbinu hizo ni pamoja kufahamu mtu aliyetengeneza ujumbe na ukweli kuhusu habari iliyotolewa.
- Mbinu hizo ni pamoja kufahamu mtu aliyetengeneza ujumbe na ukweli kuhusu habari iliyotolewa.
- Mbinu hizo zitakuepusha na madhara yatokanayo na COVID-19.
Dar es Salaam. Licha ya WhatsApp kuwa miongoni mwa mitandao ya kijamii inayokua kwa kasi duniani, bado unakabiliwa na changamoto ya baadhi ya watu kuutumia kusambaza habari za uongo hasa zinahusu COVID-19.
Mtandao huo ambao uko chini ya kampuni ya Facebook Inc ya Marekani una zaidi ya watumiaji bilioni 2 katika nchi 180 duniani.
Kutokana na madhara yatokanayo na habari za uzushi za COVID-19 zinazosambazwa katika mtandao huo, kuna kila haja ya kuendeleza mapambano dhidi ya habari hizo kwa namna tofauti.
Leo tunaangazia mbinu tano ambazo zitakusaidia wewe mtumiaji wa WhatsApp kubaini na kukabiliana na habari za uzushi unapotumia mtandao huo ili ujiweke salama na rafiki zako.
Mbinu hizi tano zimekuwa zikitumiwa na taasisi mbalimbali duniani zinazohusika na uthibitishaji habari ikiwemo Africa Check.
Unatakiwa kufahamu nani aliyetuma ujumbe
Ujumbe mwingi wa uongo unaosambaa WhatsApp mara nyingi huwa hauonyeshi nani aliyeandika ujumbe huo hasa kama umesambazwa kwa zaidi ya mtu mmoja.
Kama huna uhakika nani ameandika ujumbe husika unashauriwa usichukue hatua yoyote ikiwemo kuusambaza kwa watu wengine. Jipe muda wa kutafakari vyanzo vya ujumbe husika.
Ukimfahamu aliyetuma ujumbe WhatsApp ni rahisi kufahamu kama ujumbe wake una mashiko au la!. Picha|Mtandao.
Unatakiwa ujiulize kama unaweza kuthibitisha ujumbe au madai hayo?
Mara nyingi ujumbe wa uongo unaotumwa WhatsApp hautoi vyanzo vya madai yao au hutumia vyanzo visivyoaminika kama tovuti za habari za uwongo.
Jumbe hizo zao uongo wakati mwingine husema zinatoka katika kwa chanzo kinachoaminika, kama tovuti halisi ya habari, wakati siyo kweli.
Ukiwa huna uhakika na habari hizo, jambo la kufanya ni kuzithibitisha kama chanzo cha habari kilichonukuliwa kabla ya kuamua kuisambaza. Nenda katika vyanzo hivyo kuangalia kama wameripoti kuhusu habari iliyotolewa na wanayoisambaza.
Taarifa sahihi kuhusu Corona hutolewa na mamlaka za afya za nchi na Shirika la Afya Duniani (WHO) na wakati wote ujumbe wanaotoa unakuwa umejitosheleza.
Je! Maelezo yanaibua hofu au hasira?
Habari nyingi za uongo zinazotolewa na kusambazwa kwenye makundi ya WhatsApp hujaribu kuwafanya watu waogope au kukasirika juu ya jambo fulani.
Wakati mwingine unaweza kuwa ni ujumbe wa kushangaza juu ya tukio fulani. Hivyo unatakiwa kuwa mwangalifu kabla ya kusambaza ujumbe huu kwa kutazama dhamira ya kweli ya mtengenezaji wa ujumbe.
Umakini wako utasaidia kupunguza madhara ya kisaikolojia na kiuchumi yatokanayo na janga la Corona.
Zinazohusiana:
Ujumbe huo anahusisha picha za kutisha, video au sauti?
Mara zote jumbe habari za uongo hutumia picha, video au sauti zilizohaririwa zinazodanganya kwa lengo la kupotosha.
Wakati mwingine hutumia matukio halisi ambayo hayahusiani na kinachozungumzwa ili kufanikisha uharifu wao. Mfano wanaweza kutumia kipande cha video katika moja ya filamu ambacho kinatisha na wakasema hayo ni madhara ya Corona.
Kabla ya kusambaza habari, thibitisha habari husika kama zinaendana na tukio linalozungumziwa kwa kutumia zana mbalimbali za kidijitali ikiwemo TinEye na Google Image Reverse.
Una uhakika wa habari hiyo ni ya kweli?
Ili kuthibitisha ukweli wa habari mtandaoni kuna zana za kidijitali, taasisi na mashirika kama AfricaCheck.org na First Draft ambayo yamejikita katika kazi ya kuthibitisha habari.
Ukipitia tovuti na mitandao ya kijamii ya wathibitishaji habari, inaweza kukusaidia kwa sehemu kubaini taarifa zote za uongo na uzushi ambazo zimetolewa ufafanuzi.
Ukitumia mbinu hizo kwa makini wakati unatumia WhatsApp, hakika utajiweka katika nafasi nzuri ya kukwepa madhara ya habari za uzushi kuhusu Corona na kuwalinda unaowasiliana nao katika mtandao huo.