October 6, 2024

Wakazi Mwanza watakiwa kujitokeza kumuaga Magufuli Machi 24

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amewataka wakazi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kumuaga Hayati Rais Magufuli katika uwanja wa CCM Kirumba Machi 24 mwaka huu.

  • Mwili wa Dk Magufuli utaagwa uwanja wa CCM Kirumba Machi 24 mwaka huu.
  • Watakiwa kuliombea Taifa na Rais Samia Suluhu Hassan. 

Mwanza. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amewataka wakazi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kumuaga Hayati Rais Magufuli katika uwanja wa CCM Kirumba Machi 24 mwaka huu huku akiwataka kuwa watulivu na kuliombea Taifa katika kipindi hiki cha maombolezo.

Mongella amesema mkoa huo umepata heshima ya kipekee kwa wananchi wake kupewa fursa ya kumuaga mpendwa wao Dk Magufuli aliyefariki dunia Machi 17 mwaka huu katika Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam.

“Kama mkoa tumepata heshima ya kuuga mwili wa Hayati John Magufuli ambao utawasili asubuhi (Machi 24)  katika viwanja vya CCM Kirumba na utakuwa hapo kwa siku nzima.

“Hivyo nitumie wakati huu kuwaomba wakazi, viongozi wa kada na taasisi mbalimbali za kidini na kijamii  kujitokeza kuja kumsindikiza mwenzetu kabla ya mwili huo kupelekwa Chato,” amesema Mongella kwenye kikao cha viongozi wa kamati ya amani na ile ya ulinzi ya Mkoa wa Mwanza leo Machi 20, 2021.

Mkuu huyo wa mkoa pia ametumia fursa hiyo kuwaomba viongozi dini na waumini kuendelea kumwombea Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ameapishwa kuendeleza mikoba ya Hayati Magufuli. 

“Nina wasiwasi kwamba yeye ndiye anapitia wakati mgumu zaidi pamoja na familia,  ukiangalia yeye ndiye anaenda kukalia kiti cha hayati aliyekuwa akishirikiana naye,  ndiye ataongoza shughuli zote za msiba na ndiye atasimama kuwaongoza Watanzania na kuwaapisha viongozi wengine atakaowateua,” amesema Mongella kwenye kikao hicho.

Mongella amesema toka msiba huu utokee ameshuhudia juhudi za viongozi wa madhebu mbalimbali ya kidini na waumini wakisimama kuliombea Taifa na kwamba huo ndiyo uzalendo wa kweli. 

Mwili wa Dk Magufuli aliyefariki kwa maradhi ya moyo unaagwa leo na kesho Dar es Salaam na kisha utapelekwa jijini Dodoma, Zanzibar, Mwanza na kisha utazikwa Chato mkoani Geita Machi 26, 2021. 


Soma zaidi: 


Viongozi wa dini wamtaja Magufuli

Sheikh wa Mkoa wa Mwanza,  Hassan Kabeke amesema akiwa kama kiongozi wa Waislam mkoani hapo atakuwa mchoyo wa fadhila kama hatomshukuru Magufuli kwa yale aliyoyafanya kwa Waislam nchi nzima.

Sheikh Kabeke amesema kiongozi huyo amekuwa akiwaunganisha Wakiristo na Waislam wote na kufanikisha kujenga misikiti ambayo hawakuwa nayo.

“Hayati Magufuli ndiye aliyesababisha tunapata msikiti wa Bakwata hapo Dar es Salaam,  aliweza kujenga msikiti mwingine makao makuu ya nchi Dodoma,  na akajenga msikiti mwingine Chato,  haya hayakuwa matakwa yake isipokuwa ni Mungu aliyekuwa naye ndani yake,” amesema Kabeke.

Kufariki kwa Rais Magufuli kumemfanya aliyekuwa makamu wake Mama Samia Suluhu Hassan kuapishwa na kuwa Rais wa sita wa Tanzania ambaye atahudumu katika wadhifa huo mpaka 2025. 

Mwenyekiti wa makanisa ya African Inland Church (AICT),  Philipo Mafuja amesema pamoja na maombi yote lakini pia waOmbee kamati ya CCM Taifa ambayo itakayopendekeza jina la atakayekuwa makamu wa Rais. 

“Tanzania tunapitia wakati mgumu ila Mungu hatatuacha na kwamba tuendelee kuombea kamati ya CCM Taifa ipendekeze jina litakalopata kibali cha kuwa msaidizi wa Rais na wote wafanye kazi ya kuendeleza Hayati Magufuli alipoishia, “amesema Mafuja.