November 24, 2024

Sekta ya utalii ilivyoimarika wakati wa uongozi wa Magufuli

Tangu kuingia kwa Hayati Rais Magufuli mwaka 2015 alifanya mambo mbalimbali kukuza utalii ikiwemo kuongeza mazao ya utalii na kuboresha miundombinu .

  • Tangu kuingia kwa Hayati Rais Magufuli mwaka 2015 alifanya mambo mbalimbali kukuza utalii ikiwemo kuongeza mazao ya utalii.
  • Pia Serikali yake imenunua ndege na kuanzisha tamasha kubwa la kila mwaka la kuangazia urithi wa Tanzania. 

Dar es Salaam. Rais Magufuli amewaacha Watanzania katika huzuni na majonzi baada ya safari yake duniani kufikia tamati Machi 17 mwaka huu wakati akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa moyo katika hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam.

Hata hivyo, kifo chake kimeacha alama muhimu katika sekta ya utalii Tanzania ambayo huenda ikachukua muda mrefu kufutika, ikizingatiwa kuwa alichukua hatua mbalimbali ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya utalii. 

Siku za uhai wake, Rais John Magufuli alisisitiza sana Wizara ya Maliasili na Utalii kuweka mikakati madhubuti ya kukuza sekta ya utalii Tanzania ikiwemo kushughulikia changamoto ya gharama na usafi katika hoteli wanazofikia watalii.

“Napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kuendelea kujipanga vizuri na kuweka mikakati madhubuti ya kuongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini,” alisema Hayati Dk Magufuli Julai 9, 2019 wakati akizindua hifadhi mpya ya Taifa ya Burigi Chato iliyopo Wilaya ya Chato mkoani Geita ambayo ni ya tatu kwa ukubwa baada ya Ruaha na Serengeti.

Alisema pamoja na jitihada zinazofanyika na mafanikio yaliyopatikana, ni wazi kuwa bado mamlaka husika zinahitaji kuongeza bidii zaidi kuvutia watalii wengi ikizingatiwa kuwa Tanzania ina vivutio vingi vya utalii. 

“Naiagiza Wizara kupanua wigo wa utalii nchini kwa kuongeza mazao ya utalii sambamba na utalii wa wanyama pori. Ingefaa iweke mkazo zaidi katika utalii wa fukwe na meli, utamaduni na kadharika,” alisema Magaufuli katika uzinduzi huo.

Licha ya msisitizo huo, Magufuli alifanya kwa vitendo kuikuza sekta hiyo kwa kufanya mambo mbalimbali ambayo aliamini yanaweza kuiweka Tanzania kwenye ramani ya dunia.

Kuongezeka kwa vivutio vya utalii

Katika utawala wake, kulishuhudiwa kupanuliwa kwa mazao ya utalii ambayo ni Hifadhi za Taifa kutoka 16 hadi 22 baada ya baadhi ya mapori ya akiba kupandishwa hadhi.

Ongezeko hilo lilitokana na kupandisha hadhi kwa mapori ya akiba ya Burigi, Biharamulo, Kimisi na Rumanyika na kuwa Hifadhi za Taifa za Burigi Chato, Ibanda na Rumanyika ambazo ziko kanda ya ziwa. 

Pia sehemu ya Pori la Akiba la Selous lilimegwa na kuwa hifadhi ya Taifa Nyerere, sehemu ya Pori la Akiba Ugalla kuwa Hifadhi ya Taifa Mto Ugalla na Pori la Akiba Kigosi kuwa Hifadhi ya Taifa Kigosi.

Magufuli kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii alilenga  kuyafanya maeneo ambayo hayajafikiwa na watalii yaboreshwe ili kukuza pato la Taifa. 

Reli ya kati, ununuzi wa meli Ziwa Victoria na uboreshaji wa sekta ya anga kulisaidia sana kukuza sekta ya utalii wakati wa utawala wake hasa kanda ya ziwa.

Kuanzishwa kwa Chaneli ya utalii

Kabla ya utawala wa Hayati Magufuli, Tanzania haikuwa na chaneli rasmi ya kutangaza utalii wake. Mara nyingi vivutio vya Tanzania vilirushwa kupitia chaneli za kimataifa.

Lakini katika kipindi cha uongozi wake alifanikisha uanzishwaji wa chaneli ya televisheni ya Safari (Tanzania Safari Chaneli) ambayo ni mahususi kwa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania.

Chaneli hiyo inayoendeshwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) inapatikana katika ving’amuzi mbalimbali kikiwemo cha Startimes.

Uanzishwaji wake ulikuwa ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alilolitoa alipozuru makao makuu ya shirika hilo Mei 16 2019 na kuelekeza uongozi wa TBC uangalie uwezekano wa kuanzisha chaneli ya utalii kwa kushirikiana na Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa).

Chaneli hiyo imesaidia kufungua milango ya ajira kwa watu mbalimbali wakiwemo wananchi ambao watanufaika na shughuli na biashara ya utalii katika maeneo mbalimbali yenye vivutio nchini.

Ajira hizo zinajumuisha pia wafanyakazi watakaokuwa wanazalisha maudhui ya vipindi vya chaneli hiyo ambayo inarusha matangazo yake kwa saa 24 kwa wiki.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wa wakati huo, Paul Makonda alisema ni jambo la kujivunia kuanzishwa kwa chaneli hiyo lakini nguvu zaidi ya mitandao ya kijamii itumike kutangaza vivutio vya utalii na kutumia maeneo ya wazi kuwafikia watu wengi.

Uimarishaji wa Shirika la ndege la Tanzania

Wakati Magufuli anaingia madarakani mwaka 2015, Shirika La Ndege la Tanzania (ATCL) lilikuwa na ndege moja tu. 

Kwa mujibu wa Wizara ya Fedha na Mipango, ATCL inatarajiwa kuwa na ndege mpya tatu ifikapo Julai mwaka huu na kulifanya shirika hilo kuwa na  ndege mpya 11 sawa na idadi ya ndege 12 ndani ya kipindi cha utawala wa Magufuli.

Usafiri wa ndege umekuwa kiungo muhimu katika sekta ya utalii kwa sababu hutumika kuwasafirisha watalii wa ndani na wa kimataifa kuja nchini ili kushuhudia vivutio mbalimbali ambavyo Tanzania imebarikiwa kuwa navyo. 

Ndege hizo siyo tu hutumika kusafirisha watalii bali zinasaidia kutanua wigo wa fursa za kibiashara kwa Watanzania na nchi za nje. 


Soma zaidi


Uboreshaji wa viwanja vya ndege na miundombinu

Katika utawala wake, Dk Magufuli alisimamia ujenzi na uboreshaji wa viwanja mbalimbali vya ndege akiamini kuwa nchi kuwa na ndege nyingi ambazo haziwezi kutua katika viwanja mbalimbali ni bure. 

Kutoka kujenga uwanja wa ndege wa Chato hadi kujenga jengo la tatu la uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) ambao umekuwa ni lango kuu kwa wageni kuingia nchi kutokana na uwezo wake wa kupokea ndege kubwa.

Kwa sasa, jengo la tatu la abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) linatumiwa kama kitovu cha shughuli za utalii jijini Dar es Salaam.

Jengo hilo lina uwezo wa kuhudumia abiria milioni 6 kwa mwaka na linauwezo wa kuhudumia ndege 17 hadi 19 zikiwemo kubwa kwa wakati mmoja huku likiwa na sehemu kubwa ya kuegeshea magari. 

Viwanja vingine vya ndege vilivyokarabatiwa wakati wa uongozi wa Magufuli ni pamoja na Shinyanga, Tabora, Sumbawanga na Kigoma ili viwe na kiwango cha kimataifa. 

Viwanja hivyo vimesaidia maeneo mbalimbali ya nchi kufikika kirahisi sambamba na ujenzi wa barabara mbalimbali nchini. 

Muonekano wa jengo la la tatu JNIA ambalo ni kituo muhimu kwa watalii wanaotoka nje ya nchi. Picha|Mtandao.

Tamasha la Urithi Wetu

Tamasha la Urithi wetu ambalo lilianzishwa mwaka 2018 ni alama nyingine aliyoiacha Dk Magufuli katika sekta ya utalii kwa sababu ni mahususi kwa ajili ya kuvitangaza vivutio vya utalii hasa vya utamaduni ambavyo vinalezea asili ya Mtanzania. 

Tamasha hilo linalofanyika kila mwaka katika mikoa yote Tanzania, mwaka 2018 lilifanyika mikoa minne ya Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na visiwa vya Zanzibar ambapo lilifungua fursa kwa makampuni ya utalii ya ndani na nje kunufaika na fursa zilizojitokeza katika kipindi chote cha tamasha hilo. 

Shughuli zinazofanyika katika tamasha hilo ni ngoma na muziki wa asili, mapishi ya vyakula vya kitanzania, maonyesho ya zana za utamaduni na vivutio vingine vya utalii.