November 24, 2024

Maelfu wajitokeza barabarani kumuaga Magufuli

Wakazi wa maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dar es Salaam wamejitokeza katika barabara ambapo mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli ulipopita kuelekea katika uwanja wa Uhuru.

Wakazi mbalimbali wa jijini Dar es Salaam waliojitokeza kuaga mwili wa Hayati John Magufuli katika uwanja wa Uhuru wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan. Picha|BBC


  • Kanga, maua, majani zikiwa zimetandikwa barabarani kuonyesha umuhimu wa kiongozi huyo.
  • Maombolezo, huzuni na simanzi ni maneno yasiyotosha kuelezea hisia zao.
  • Kutokea Kanisa la St Peters, Osterbay hadi Uwanja wa Uhuru, maelfu walijipanga barabarani kuaga mwili wa Hayati Dk Magufuli.

Dar es Salaam. “Parapanda italia parapanda…” ni kati ya nyimbo ambazo maelfu ya Watanzania waliojipanga barabarani kuaga mwili wa Hayati John Magufuli wakati ukielekea katika uwanja wa Uhuru kwa ajili ya kuagwa na wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Mwili wa Rais aliyefariki dunia Machi 17 mwaka huu ulifanyiwa misa takatifu katika Kanisa la St Peters, Osterbay na baadaye mwili wake umepelekwa katika uwanja wa Uhuru.

Msafara uliobeba mwili wake na wafiwa ulipokuwa ukipita barabarani, maelfu ya wakazi wa jiji hilo wamejitokeza kuonyesha heshima zao za mwisho kwa kipenzi cha mioyo yao huku shughuli mbalimbali hasa za usafiri zikisimama kwa muda.  

Simanzi, huzuni, maombolezo yanabaki kuwa maneno yasiofikia uhalisia wa hisia za Watanzania. 

Wapo ambao walibeba mabango yenye ujumbe mbalimbali ili kuonyesha hisia zao kwa kiongozi huyo mkuu wa nchi aliyeaga dunia kwa maradhi ya moyo.

Moja ya bango lilibobebwa na mwananchi katika eneo la Magomeni linasema  “RIP chuma cha wanyonge Tanzania” huku wengine wakibubujikwa na machozi na kujifuta kwa leso.

Licha ya kujifuta kwa vitambaa na leso, bado machozi na huzuni hazikumalizika katika nyuso za wakazi hao ambao wamepata fursa ya mwisho kumuaga mpendwa wao.

                   

Vijana, wazee na watoto walioshikilia majani ya miti, mashati, kanga, vitenge na mitandio ikiwa imetandikwa barabarani kuuaga mwili wa Hayati Rais Magufuli kudhihirisha kuwa ameacha alama isiyofutika katika mioyo yao.

Kusimama katika kuta kuona msafara huo uliopita barabara mbalimbali kutokea kanisa la Mtakatifu Peter kuelekea Uwanja wa Uhuru haikuwa tabu kwa wengi. Kusimama madarajani bila hofu ya kuanguka haikuwa tatizo kwa wengi.

Zote hizo ni juhudi za Watanzania wanaohuzunishwa na kuondoka kwa Hyati Rais Magufuli.

Imezoeleka bodaboda na bajaji kupiga nyimbo za shangwe barabarani lakini leo ni tofauti, ni nyimbo za huzuni tu huku wadau hao wa usafiri wakifanya kila linalowezekana kukimbizana na msafara uliobeba mwili wa Magufuli kwa mafuta ambayo huenda wangelibebea wasafiri.

Hata mwili huo ilipowasili katika uwanja wa uhuru, vilio vilizidi kutokana na umati mkubwa watu waliojaza uwanja huo kumuaga mpendwa wao. 

“Kwaheri baba, kwaheri jembe, kwaheri chuma cha Watanzania na kwa heri pengo ambalo halitozibika.” walisikika baadhi ya watu uwanjani hapo kudhihirisha amemaliza kazi aliyoitiwa duniani na sasa amepumzika. 

Hayati Magufuli ataagwa kwa siku mbili katika uwanja wa Uhuru kabla mwili wake haujasafirishwa kuelekea jijini Dodoma kwa ajili hatua inayofuata.