October 6, 2024

Magufuli alivyoacha alama isiyofutika jijini Mwanza

Ni ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja, kiwanja cha ndege na meli ambayo imerahisisha shughuli za biashara na usafirishaji kwa wakazi wa jiji hilo.

  • Ni ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja, kiwanja cha ndege na meli.
  • Miundombinu hiyo imesaidia kurahisisha shughuli za biashara na usafirishaji kwa wakazi wa jiji hilo.

Dar es Salaam. Mkoa wa Mwanza ni miongoni mwa mikoa minne ya Tanzania ambayo wananchi wake watapata fursa ya kuuga mwili wa Hayati Rais John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17 mwaka huu. 

Kwa mujibu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Dk Magufuli ataagwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza na Chato mkoani Geita ambako atapumzishwa katika nyumba yake ya milele Machi 25 mwaka huu. 

Fursa ya wananchi wa Mwanza kumuaga Dk Magufuli aliyefariki akiwa na umri wa miaka 61, huenda inatokana na mapenzi aliyokuwanayo rais huyo kwa mkoa huo.

Wakati wa uongozi wake, Magufuli alipenda kuiona Mwanza inakuwa kitovu cha shughuli za utalii na uchumi kwa mikoa ya kanda ya Ziwa kutokana na rasilimali zilizopo kwenye mkoa huo.

Ili kufanikisha azma hiyo, Hayati Rais Magufuli aliyefariki katika hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam alijenga miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara na vyombo vya uchukuzi ili kuupaisha mkoa huo kiuchumi. 

Moja ya alama alizoacha katika mkoa huo ni Serikali yake kujenga  daraja la waenda kwa miguu la Furahisha lililogharimu zaidi ya Sh4.1 bilioni fedha ambazo zilitokana na mapato ya ndani.

Daraja hilo ambalo lilizinduliwa mwaka 2018 na Magufuli mwenyewe, linawasaidia wakazi wa kukabiliana na foleni kwa sababu chini yanapita magari na watembea kwa miguu kwa upande wa juu. 

Mbali na ujenzi wa daraja hilo, Hayati Magufuli pia aliweza kutoa zaidi ya Sh9 bilioni kwa ajili ya upanuzi wa barabara za njia nne kutoka uwanja wa ndege wa Mwanza hadi Makongoro jijini Mwanza.

Barabara hiyo iliyokamilika mwaka 2018 ni muhimu kwa wasafiri wanaotumia uwanja wa ndege wa Mwanza kwa shughuli mbalimbali ikiwemo biashara na usafirishaji wa bidhaa.

Daraja la waenda kwa miguu la Furahisha lililogharimu zaidi ya Sh4.1 bilioni fedha ambazo zilitokana na mapato ya ndani. Picha|GSengo.

Ujenzi wa daraja la Kigongo- Busisi

Katika kuimarisha sekta ya  uchukuzi katika Mkoa wa Mwanza, Dk Magufuli mapema mwaka 2019 aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi ambao ujenzi wake unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh699.2 bilioni fedha zinazotokana na mapato ya ndani.

Daraja hilo lenye urefu wa kilometa 3.2 na upana wa mita 28.45 litakapokamilika litakaunganisha mawasiliano ya barabara kati ya mikoa ya Mwanza na Geita kwa kukatisha Ziwa Victoria na litapunguza adha ya usafiri wa majini kwa wakazi wa mikoa hiyo na nchi jirani za Afrika Mashariki na Maziwa Makuu.

Ndani ya hilo daraja kutakuwa na mita 5 kwa ajili ya waenda kwa miguu sambamba na sehemu za kuegeshea magari kwa kila upande wa daraja ambapo ujenzi wake utakamilika mwaka 2023 na kwa mujibu wa Hayati Magufuli ndiyo litakauwa daraja refu kupita yote barani Afrika.

Akizungumza wakati wa kuweka jiwe la msingi eneo la Kigongo wilayani Misungwi, Hayati Magufuli alisema ujenzi wa daraja hilo ni kielelezo kingine kwamba Tanzania ina uwezo wa kutekeleza miradi yake yenyewe  kwa kutumia fedha zake za ndani bila kutegemeawafadhili  kutoka nje ya nchi.

Kukamilika kwa miradi hiyo utakuwa umetoa fursa za ajira 1,600 kwa wakazi wa maeneo jirani na utapunguza changamoto ya usafirishaji waliyokuwa wanaipata wananchi


Zinazohusiana:


Meli Mpya  na ukarabati wa meli zingine mbili

Katika shughuli za utiaji saini huo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Huduma za Meli nchini (MSCL), Erick Hamiss alimweleza Hayati Magufuli kuwa meli hiyo inajengwa kwa fedha za ndani zaidi ya Sh89.7 bilioni.

Meli hiyo itakuwa na urefu wa mita 92.6 upana mita 17 na itakuwa na madaraja matatu ya abiria ambapo daraja la kwanza litakuwa na uwezo wa kubeba abiria 50, daraja la pili 316 na daraja la tatu 834. 

Meli hiyo ina uzito wa tani 3,500 na ina uwezo wa kubeba abiria 1,200 na mizigo tani 400. Meli hiyo pia ina uwezo wa kubeba magari makubwa matatu na mengine madogo 20 .

Meli hiyo baada ya kukamilika itakuwa  inaenda Bukoba mjini na jijini Mwanza na kwamba inajengwa na kampuni ya Kikorea na itakamilika ndani ya miezi 24 kuanzia mwaka 2019 ilipoanza kujengwa.

Mbali na ujenzi wa meli hiyo, awamu ya tano chini ya Hayati Magufuli kupitia sekta ya uchukuzi ilikamilisha ujenzi wa chelezo ulioenda sambamba na ukarabati wa meli za Mv Victoria na  Mv Butiama.

Ukarabati wa meli hizo pamoja na ujenzi wa chelezo uliigharimu Serikali zaidi ya Sh153 bilioni  na kwamba tayari meli zimeanza kufanya kazi kati ya Mwanza-Bukoba na Mwanza Ukerewe.

Meli ya MV Butiama ni kielelezo tosha cha ukuaji wa jiji la Mwanza. Picha|Mtandao

Upanuzi wa uwanja mpya wa ndege na rada ya kuongezea ndege

Usalama wa anga ni moja ya malengo yaliyotekelezwa kivitendo na Rais Magufuli ili kuhakikisha anga la Tanzania linakuwa salama na kuwezesha ndege ya aina yeyote kutua nchini.

Serikali imetumia zaidi ya Sh15 bilioni kwa ajili ya upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza uliohusisha ujenzi wa jengo jipya la abiria, kuendelea na upanuzi wa maegesho ya ndege, ujenzi wa jengo la mizigo, uzio wa kiwanja pamoja na maegesho ya ndege za mizigo na ujenzi wa jengo la kuongozea ndege.

Pia kujenga kituo cha umeme, maegesho ya magari, kusimika taa za kuongozea ndege na ujenzi wa mfumo wa kuondoa maji ya mvua kiwanjani ambapo shilingi bilioni 15.55 fedha za ndani zimetengwa.

Rais John Magufuli alitia saini ujenzi wa jengo hilo Julai 15 mwaka 2019 na kuwaangiza wakandarasi kuhakikisha wanakamilisha mradi huo kwa wakati.

Miradi hiyo iliyotekelezwa jijini Mwanza ni wazi kuwa wakazi wake wataendelea kumkumbuka Rais huyo ambaye anatarajiwa kuzikwa Machi 25 mwaka huu wilayani Chato, Mkoa wa Geita.