October 6, 2024

Sauti za wasanii zamlilia Rais Magufuli

Baadhi ya wasanii wa muziki wa kizazi kipya wamemuelezea Hayati Rais Magufuli kwa namna tofauti ili kuenzi utumishi wake kwa umma ikiwemo uzalendo kwa nchi yake.

  • Wasanii wa Tanzania wamesema wamepoteza kiongozi makini.
  • Wasanii wa nchi za jirani wamesema Magufuli hakuipigania Tanzania pekee bali Afrika kwa ujumla.

Dar es Salaam. Maombolezo ya msiba wa Rais John Magufuli yanaendelea kila kona ya Tanzania. 

Viongozi wa Serikali na Watanzania wako katika huzuni na tafakari nzito kuhusu kifo cha mpendwa Hayati Dk Magufuli ambaye amefariki dunia jana Machi 17 mwaka huu mkoani Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu. 

Katika mitandao ya kijamii, emoji za majonzi ni sehemu ya watu kuonyesha hisia zao kwani hata maneno hayawezi kuonyesha kile wanachojisikia juu ya kuondoka kwa kiongozi mkubwa wa nchi ambaye kwa wengi anatambulika kama “mtetezi wa wanyonge”.

Baadhi ya wasanii wa muziki wa kizazi kipya wamemuelezea Hayati Rais Magufuli kwa namna tofauti ili kuenzi utumishi wake kwa umma wakati akiwa hai. 

Msanii wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul (Diamond Platnumz) ameelezea majonzi yake kwa maneno mawili yanayofuatiwa na emoji 16 za machozi. 

Diamond kupitia mtandao wa Instagram ameandika, “Dah! Jamani.” huku picha aliyopakia msanii huyo ikifuatiwa na maoni ya watu zaidi ya 12,400 wakiwemo wasanii wengine wa kimataifa waliotoa pole kwa Watanzania.

Kati yao ni msanii wa muziki wa Reggae kutoka Jamaica, Morgan Heritage ambaye ametoa pole kwa Watanzania kufuatia msiba huo.

Wasanii wengine wameuchukua msiba huo kama kazi ya Mungu isiyo na makosa na wamesema katika kipindi hiki, Watanzania wanatakiwa kuwa wamoja na kuweka pembeni tofauti zao.

Mwanamuziki Vanessa Mdee kupitia ukurasa wake wa Instagram amesema muda wa wanadamu duniani anayeufahamu ni Mungu peke yake.  Kwa Vanesa hana mengi zaidi ya kushukuru huku akielekeza maombi yake  kwa Watanzania wote.

“Pumzika Salama Baba 🙏🏽” ameandika Vanessa Mdee katika ukurasa wake wa Instagram. 

Elias Barnabas (@barnabaclassic) yeye amebadili hadi picha yake katika mtandao wa Instagram (profile picture) na kuweka picha ya Hayati Magufuli.

Msanii huyo amesema kupokea taarifa za kifo hicho kumemnyima usingizi na majaribio ya kuandika wimbo kwa ajili ya msiba huo hayajafua dafu.

“Nimeshindwa kabisa Kwa mara ya kwanza. Nimeshindwa kabisa 😭😫 Ukweli nimekua na roho nyepesi leo. Sijawahi kabisa kuwa hivi In my life, nimeshtuka sana hakika wewe (Magufuli) ulikua mpiganaji wa vita za wote wanyonge, nimekosa nguvu kabisa kabisa narudia tena!,” amesema Barnabas.

Kwa Barnaba, wafuasi wake wameonyesha kuungana naye kwa kutuma maoni yao wakielezea hisia zao kwa emoji ya kuvunjika moyo na kububujikwa machozi (💔😭).


Soma zaidi:


Kwa wasanii, maombolezo hayajaishia kwa Watanzania pekee bali yamevuka mipaka na kuwagusa wasanii mbalimbali duniani.

Msanii mkongwe kutoka Uganda, Joseph Mayanja almaarufu kama Jose Chameleone amesema kuwa Hayati Rais Magufuli ni mwanamapinduzi wa kiafrika aliyapenda maendeleo halisi ya Afrika.

Naye Msanii Zarinah Hassan (Zari) kutoka Uganda ambaye kwake Magufuli ni baba ameandika kwenye mtandao wa Instagram kuwa “Sleep well Father in law🙏😭.”

Kwa msanii Tanasha Donna wa Kenya, Magufuli hakugusa Tanzania peke yake bali bara zima la Afrika. Katika ukurasa wake Tanasha amesema kuondoka kwa Magufuli ni pigo kwa AfriKa.

“Afrika imepoteza kiongozi Mkubwa sana. Pumzika kwa amani Rais John Pombe Magufuli.” ameandika Tanasha.

Wasanii hasa wa nyimbo za kizazi kipya watamkumbuka jinsia alivyokua karibu nao hasa katika shughuli za kiserikali na majukwaa ya kisiasa ambapo aliwapa fursa ya kuonyesha vipaji vyao na kutoa burudani kwa Watanzania.

Mathalan, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, wasanii mbalimbali walijotokeza kwenye kampeni za Chama Cha Mapinduzi kumnadi Rais Magufuli wakizunguka maeneo mbalimbali ya nchi.